‘No reforms, no election’ ya Chadema kuendelea Dar, Pwani

Muktasari:
- No reforms, no election (bila mabadiliko, hakuna uchaguzi) yenye lengo la kuelimisha umma kuhusu hatua ya chama hicho ya kuishinikiza Serikali kubadilisha mfumo wa uchaguzi ili kuwepo kwa haki sawa kwa vyama vyote, ilianza Machi 23 hadi 29, 2025 katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa, Songwe na Njombe.
Dar es Salaam. Baada ya ajenda ya No reforms, no election ya Chadema kukabiliana na vikwazo katika Kanda ya Kusini, hatimaye viongozi wa chama hicho wameibukia Kanda ya Pwani inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Ajenda ya No reforms, no election (bila mabadiliko, hakuna uchaguzi) yenye lengo la kuelimisha umma kuhusu hatua ya chama hicho ya kuishinikiza Serikali kubadilisha mfumo wa uchaguzi ili kuwepo kwa haki sawa kwa vyama vyote ilianza Machi 23 hadi 29, 2025 katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa, Songwe na Njombe.
Baada ya mikoa hiyo, ziara za viongozi wakuu wa chama hicho, ilihamia mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kuanzia Aprili 4 hadi 10, 2025 ambapo ilikumbana na kikwazo katika mkutano wa kuhitimisha ziara hiyo baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma kusitisha vibali vya mikutano yote mkoani humo.
Baada ya misukosuko hiyo, hatimaye chama hicho, kimetangaza kuanza kwa kampeni hiyo katika Kanda ya Pwani kesho Aprili 16, 2025 itaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), John Heche, Naibu Katibu Chadema (Bara), Aman Golugwa na viongozi wengine wa mabaraza ya chama hicho.
Wengine ni wajumbe wa Kamati Kuu, akiwemo Boniface Jacob ambaye pia ni mwenyekiti wa kanda hiyo.
Kuendelea kwa kampeni hiyo kunakuja katika kipindi ambacho mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu yupo rumande akisubiri kukamilika kwa upelelezi wa shitaka la uhaini lililofunguliwa na Jamhuri dhidi yake.
Kampeni hiyo inaibuka tena katika nyakati ambazo chama hicho kimepigwa rungu la kutoshiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, baada ya kususia kusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, zilizosainiwa jijini Dodoma Aprili 12, 2025.
Taarifa ya INEC imeibua mjadala wa wadau wa siasa na sheria, wakihoji inawezekanaje chama kilazimishwe kusaini siku iliyopangwa na tume, ilhali sheria haikuweka ukomo wa siku kwa wanaotakiwa kutia saini.