Tamu, chungu kufutwa kwa darasa la saba

Wanafunzi wa shule moja ya msingi wakishangilia jambo shuleni kwao. Kwa mujibu wa mapitio ya Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 2014, kuna uwezekano Tanzania ikaanza kutumia mfumo wa elimu ya msingi kuwa miaka sita.
Muktasari:
- Serikali imedokeza uwezekano wa wanafunzi wa elimu ya msingi kusoma kwa miaka sita badala ya saba.
Serikali imedokeza uwezekano wa wanafunzi wa elimu ya msingi kusoma kwa miaka sita badala ya saba.
Dokezo hilo lilikuwa sehemu ya hotuba ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga aliyoitoa hivi karibuni katika uzinduzi wa mkutano wa saba wa mwaka wa wahandisi wa viwanda uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)
Kauli ya Kipanga, imekuja wakati wizra hiyo ikikamilisha mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na mitalaa, ikiwa ni utekelezaj wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan.
Mara kadhaa Rais Samia amekuwa akisisitiza mfumo wa elimu kujikita katika utoaji wa ujuzi badala ya taaluma kama ilivyo sasa.
‘’…ndio maana sasa tunabadilisha mtalaa wa elimu Tanzania. Nadhani mmeshuhudia mikutano kadhaa pande zote mbili za Muungano za kutaka maoni ya wananchi kwenye mtalaa wa Tanzania, mchakato unaendelea, utakapofikia mwisho tutafanya vikao vya mwisho kushirikisha watu, tuone kwamba huu ndio mtalaa tunaokubaliana nao,’’ alisema Rais Samia alipozungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu mapema mwaka huu.
Kwa mujibu wa dokezo la Waziri Kipanga, Serikali itaweka utaratibu wa elimumsingi kuwa ya lazima kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, ambapo elimu hiyo itatolewa kwa miaka 10.
Alisema kupitia sera hiyo, kutakuwa na mikondo miwili darasa la sita, yaani wale watakaokuwa wakipata ujuzi wa ufundi na wengine watakaojikita kupata maarifa ya darasani.
Lengo la kufanya hivyo alieleza kuwa ni kuwafanya wanafunzi wanaohitimu masomo kuajirika na kujiajiri wenyewe katika nyanja mbalimbali.
Wasemavyo wadau
Japo tamko la sera ya elimu ya mwaka 2014 kuhusu elimu ya msingi kuishia darasa la sita halijtekelezeka, wadau wa elimu wamepokea dokezo la Serikali kwa mitazamo tofauti.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Christian Bwaya anasema, kupunguzwa kwa idadi ya miaka ambayo mwanafunzi atasoma elimu ya msingi, kumefanywa kwa nia njema.
“Naona ni kurekebisha mfumo wa elimu ambayo itakuwa lazima. Miaka ambayo mtoto ataitumia kwenye elimu ya msingi na sekondari imekuwa 10 faida yake hatutakuwa na watoto wa miaka 12 na 13 watakaotolewa nje ya mfumo wa elimu,”anaeleza.
Bwaya anafafanua kuwa mtoto anapokatishwa masomo kwa kigezo cha kushindwa mtihani ukiwamo wa darasa la saba, hurudi nyumbani na pengine anaweza kujiunga na kundi la watoto wa mitaani, hivyo hatua hiyo ya kisera itawasaidia kumaliza shule wakiwa na miaka kuanzia 17 na 18, umri anaosema tayari wanajitambua.
Kuhusu kuondolewa kwa mtihani wa darasa la saba, anasema ni faida kubwa, kwani mitihani hutengeneza ushindani usio wa lazima kwa watahiniwa hao.
“Kumekuwa na presha kubwa sana, watoto wadogo wanafanyishwa mitihani mara kwa mara, tafsiri yake imekuwa tunachanganya mitihani na elimu, yaani watoto ni mitihani kuanzia wanapoanza hadi wanapomaliza.Sasa tunawaondolea presha ambayo wakati mwingine inawaathiri, ”anaeleza Bwaya.
Bwaya ambaye ni mtalamu wa saikolojia, anasema, kazi kubwa itakuwa kwa walimu kujikita kuwalea wanafunzi ili waelewe kikamilifu.
“Mtoto anapokuwa anasoma kwa sababu ya mitihani na wakati mwingine anaambiwa umefeli, huwezi au umefeli maisha, hilo si sawa. Kwa hiyo haya ni mafanikio makubwa kujenga elimu ya watoto bila kuwaingiza kwenye ushindani usio wa lazima,”anasema.
Hata hivyo, hoja yake inakosolewa na Mkurugenzi mstaafu wa shirika Uwezo Tanzania Zaida Mgalla anayesema, pamoja na upimaji uliopo katika ngazi za elimu, bado kuna watoto wanaomaliza kidato cha nne, huku wakiwa hawawezi kusoma.
“Je, tutakapowaacha tangu wananza darasa la kwanza hadi la 12 tutakuwa na watoto wa namna gani.Kama hakutakuwa na upimaji, tutawabeba wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika. Mpaka sasa tuna wanafunzi wasiojua kuandika hata majina yao na walichujwa darasa la nne; kuna wanafunzi wanamaliza darasa la saba wapo kidato cha kwanza hawajui kusoma,”anaeleza Zaida ambaye shirika lake hilo limekuwa likijkita katika kufanya tathmini za uwezo wa wanafunzi wa shule za msingi kujifunza stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.
Anashauri Serikali iweke vigezo vikali vya kuwapima watoto na si kuwaacha hadi kumaliza kidato cha nne, huku akionyesha wasiwasi kuwa kama hilo halitaangaliwa, Taifa linaweza kupata hasara.
Anasema Taifa lisione faraja kwa kila mwanafunzi kwenda shule, wakati hakuna wanachojifunza. Kitendo hicho anasema ni sawa na kuwaburuza, kwani kinachopaswa kuzingatiwa ni ubora wa elimu.
Anaeleza kuwa jambo linalopaswa kufanywa kabla ya utekelezaji wa sera hiyo, ni kufanywa tathmini ya mambo yanayopaswa kufundishwa kwa wanafunzi katika ngazi ya msingi ili yawajengee msingi wakifika sekondari.
Sera nzuri lakini…
Mpango wa elimu ya msingi kuishia darasa la sita, ulishatajwa katika sera ya elimu ya mwaka 2014, lakini haikuwahi kutekelezwa hasa baada ya kuingia kwa utawala wa awamu ya tano.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk Faraja Christomus anasema, hayati John Magufuli alisitisha utekelezaji wa sera hiyo, kutokana na kuangalia uwezo wa Serikali kuwahudumia wanafunzi wa madarasa mawili tofauti watakaohitimu kwa mwaka mmoja.
“Hiyo ndio changamoto iliyokuwepo, kutakuwa na madarasa mawili yanayohitimu elimu ya msingi (watakaohitimu darasa la saba na wanaofika darasa la sita), matokeo yake, kidato cha kwanza wanafunzi watakuwa wengi, Serikali ijiandae,”anaeleza.
Pamoja na hilo, ana hofu kuwa uamuzi wa elimu ya msingi kuishia darasa la sita unaweza pia kukumbana na changamoto ya miundombinu.
Anasema nchi yetu imekuwa na tatizo la uwekezaji wa miundombinu na makadirio ya wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza. Ana hofu na uwekezaji wa Serikali na hata taasisi binafsi.
“Serikali iweke mkakati unaotekelezeka, tumekuwa tukilalamika mara nyingi Serikali kushtukiza kufanya mambo. Sasa hivi wanafanya uamuzi elimumsingi itakuwa lazima, je, wanaweka mikakati ya kuanza kujiandaa kidogo kidogo kwa ajili ya mwaka 2029 wanafunzi watakapokuwa wengi kuingia kidato cha kwanza au tutaona mwaka 2028 ndio wanaanza kufanya mipango ya zimamoto ya kujenga madarasa kuhimili ongezeko la wanafunzi?”anahoji.
Kwa upande wake aliyewahi kuwa Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Suzan Lyimo (Chadema) anasema utekelezaji wa sera hiyo, utakuwa ana matunda mazuri kwani itapunguza ajira za utotoni.
“Kwa sababu wanafunzi wanaanza shule wakiwa wadogo, tunataka waende hadi kidato cha nne, wakimaliza watakuwa na uelewa mpana ukilinganisha na yule wa darasa la saba, na pia tayari atakuwa anaajirika shida kubwa itakuwa kwenye utekelezaji,”anaeleza.
Changamoto anayoiona Suzan ni miundombinu, ambalo ni tatizo kubwa nchini akijumuisha na upungufu wa walimu kwa ngazi zote mbili.
Anasema wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka mmoja hawazidi laki tano, hivyo wakipelekwa wanafunzi milioni tatu hawatakuwa na walimu wa kuwafundisha wala vyumba vya madarasa vya kutosha.
Hoja si miaka…
Mdau wa elimu Mustapha Puya anasema kuwa changamoto iliyopo sasa si miaka ambayo mwanafunzi anasoma, bali vitu anavyopaswa kufundishwa.
“Mtoto anafundishwa hadi darasa la saba hana mwelekeo wa kusema hizi taka niziokote nizitupe. Anachofundishwa ni kwa ajili ya kujibia mitihani. Tatizo hilo linachangiwa na sisi kutokuwa na maono ya taifa tunalotaka kulijenga,”anasema.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Sera Umoja wa Wamiliki na Mameneja wa Taasisi Binafsi za Elimu Tanzania (Tamongsco ), Benjamin Nkonya anasema, hakuna shida mwanafunzi kusoma miaka mingi, ila la msingi ni elimu inayotolewa iwe na tija.
“Unanifundisha jiografia ya sayari ya Jupita inisaidie nini? Mimi nataka kujua kitu ambacho nitakitumia, elimu ni mtaji mtu aitumie kujipatia fedha. Mtu asome hata miaka mitano lakini atoke anaeeleweka. Kuna mtu ameniandikia kesi yangu kuhusu watu waliovamia ardhi yangu kaandika vitu vya ajabu mpaka hakimu amenishangaa, unampa mtu gari alitengeneze, analiharibu,”anasema .
Anasema tatizo lililopo wanafunzi wanaozalishwa hawana uwezo wa kushindana kwenye soko la ajira kutokana na mfumo mbovu wa elimu.