Ni vita ya Jaja, Okwi dimbani

Muktasari:
Tangu Ligi Kuu ianze msimu huu, Okwi ameifungia Simba bao moja, Jaja hajafunga.
Dar es Salaam. Pambano la watani wa Jadi, Yanga na Simba litafanyika Oktoba 18 huku ubishani mkubwa ukiwa nani ataibuka bora uwanjani kati ya mshambuliaji Genilson Santos ‘Jaja’ wa Yanga na Emmanuel Okwi wa Simba.
Wachezaji hao waliingia midomoni mwa watu kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili baada ya Okwi kuzua mgogoro na klabu yake ya zamani Yanga baada ya kujiunga na Simba.
Okwi alijiunga na Simba baada ya kuona viongozi wa Yanga hawamjali ingawa aliibua makundi mawili moja likitaka abaki kuichezea klabu hiyo na lingine likitaka aachwe.
Hata hivyo, baadaye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ilimuhalalisha Okwi kuichezea Simba.
Wakati Ligi Kuu Bara ikiingia raundi ya nne, Jaja bado hajatupia nyavuni bao lolote katika mechi tatu alizocheza huku mwenzake Okwi akiwa amefunga bao moja.
Jambo hilo limewapa moyo mashabiki wa Simba ambao wanaona kama wameibuka kidedea kwa kumsajili Okwi kutokana na mambo anayoyafanya uwanjani wakati Jaja bado hajawafurahisha Yanga mpaka sasa.
Mechi zote Jaja ameanza kikosi cha kwanza lakini bado hajaonyesha ubora wake ambao ulitetewa na kocha wake Marcio Maximo wakati wa usajili.
Tangu afunge mabao mawili na kuipa Yanga ubingwa kwenye mechi ya ngao ya jamii, Jaja raia wa Brazil ameichezea timu hiyo dakika 270 katika mechi tatu za Ligi Kuu Bara, lakini hajafunga bao, wakati Okwi amefunga bao moja pia ametoa pasi zilizozaa mabao mawili kwa timu yake.