Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mfumo wa BVR na changamoto zake

Muktasari:

Wataalamu na wazoefu wa utumiaji wa mfumo huu wanasema kwamba unawezesha kupunguza wizi wa kura, kwa sababu mtu mmoja hawezi kupiga kura zaidi ya mara moja, kwani atakapoingiza tu alama zake za vidole kwenye mashine itaonekana kama ameshapiga kura au la.

BVR ni mfumo wa uandikishaji wapigakura ambao unakusanya taarifa muhimu zote za mtu na kuweza kuziainisha tofauti na taarifa za mtu mwingine. Ni mfumo unaowezesha kuandikisha wapigakura kwa mamilioni tena kwa muda mchache.

Wataalamu na wazoefu wa utumiaji wa mfumo huu wanasema kwamba unawezesha kupunguza wizi wa kura, kwa sababu mtu mmoja hawezi kupiga kura zaidi ya mara moja, kwani atakapoingiza tu alama zake za vidole kwenye mashine itaonekana kama ameshapiga kura au la.

Pia, hata kama atabadilisha mfumo wake wa majina, mashine itagundua kuwa alama hizo za vidole zimeshatumika kwa mtu mwenye jina tofauti na hilo hivyo kumzuia asipige kura mara ya pili.

BVR ina uwezo wa kutambua alama za vidole, kiini cha jicho na sauti. Pia ina uwezo mkubwa wa kuweka usalama wa taarifa za mtu kwani ni vigumu kuchezea au kuharibu taarifa.

Kuwa na mfumo unaoweza kumtambua mpigakura halali ndiyo sifa kubwa ya uchaguzi ulio huru na wa haki.

Watumiaji wa BVR wanapaswa kuwa na ujuzi gani?

Kwanza ni kuwa na elimu ya awali ya kompyuta ikitiliwa umuhimu katika suala la kupata takwimu, kuzifanyia kazi na kuzidhibiti. Wafanyakazi pia wanapaswa wawe na ujuzi wa kupanga na uwezo wa kutafsiri takwimu.

Kadhalika ni muhimu kuwapo kwa watu wenye uwezo wa kuzitengeneza mashine hizo pale zinapokwama au kuharibika. Lakini ili yote hayo yawezekane, kunahitajika muda wa kutosha wa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi.

Changamoto za uendeshaji wa mfumo wa BVR

Moja ya matatizo yanayoweza kujitokeza ni mashine yenyewe kuathiriwa na mazingira kama vile hali ya joto, unyevunyevu na mvua. Pia mara nyingine inakuwa vigumu kupata alama za vidole kwa baadhi ya watu.

Kwa upande wa kiufundi inaweza kupatikana hatari ya uharibifu wa programu za kompyuta, kukosa kifurushi cha intaneti hasa katika maeneo ya vijijini pamoja na kuwa na mfumo duni wa kukamata alama za vidole.

Mara nyingine mfumo wa BVR na huu wa kukamata alama za vidole, haviwezi kufanya kazi kwa pamoja, kwa sababu ya kuwa mifumo hiyo inatokana na watengenezaji tofauti.

Tahadhari

Katika kutumia mfumo huu, ni vyema kuhakikisha kwamba yeyote anayepewa zabuni ya kuleta mashine za anapaswa kuelekeza jinsi inavyotumika na kuhakikisha urahisi wa utumiaji na uharaka wake.

Utafutaji wa aina sahihi ya mashine ya kuchukua alama za vidole pia ni jambo muhimu sambamba na kuwa na kamera za kisasa kwenye kompyuta na mashine ya kuchapia.

Wakati wa kuzifanyia majaribio mashine hizo ni muhimu kuhakikisha kuwa teknolojia inayotumika inaruhusu kufanyiwa marekebisho na kuondosha upungufu wowote utakaojitokeza.

Kuwa na uchaguzi huru na wa haki ndiyo dhamira kubwa katika kuhakikisha kuwa demokrasia ya ukweli inapatikana, lakini hiyo imekuwa ni changamoto ya muda mrefu hasa katika nchi zenye demokrasia changa.

Kutafuta suluhisho la changamoto hiyo ndiko kulikoibua mahitaji ya kuwa na mifumo ya kiteknolojia itakayosaidia utekelezaji wa dhamira hiyo.

Kwa sasa mfumo ulioidhinishwa ulimwenguni kuwa una uwezo wa kukabiliana na changamoto za uchakachuzi wa matokeo ya kura ni mfumo wa BVR.