Ndani ya boksi: Wasanii na jamii tupo 'Fildi' moja na shetani

Je, unaifahamu stori ya wimbo unaoitwa Gloomy Sunday? Uliosababisha vifo vya watu zaidi 100? Rezso Seress, aliandika mashairi ya wimbo huo, baada ya kupigwa chini na mpenzi wake. Kisha kugeuka kuwa wimbo wa ‘Israeli’ mtoa roho za watu.

Hakuishia kuandika shairi tu, hata ala za muziki huo wenye huzuni sana, alipiga yeye mwenyewe. Ukiusikiliza hata sasa hivi utaelewa kwa nini ngoma hii ilifanya watu wengi kujiua. Haswa walioachwa na wapenzi wao. Jamaa kamsimanga mtu humo balaa.

Ongozeko la vifo kutokana na wimbo huo, likasababisha upigwe marufuku kuchezwa nchini Hungary. Ajabu ni kwamba hata ulipotafsiriwa kwa lugha zingine, ulileta madhara yaleyale na hivyo kupigwa marufuku tena nchini Uingereza mwaka 1968. Noma na nusu. Mpenzi aliyetungiwa wimbo huo alijiua na mtunzi wa wimbo pia akajiua baada ya kusikia ‘eksi’ wake kajiua. Je, huamini kama muziki una nguvu ya ziada kwenye mwili wa mwanadamu? Bila shaka hisia na akili zako zinakupotosha sana. Muziki ndio kila kitu.

Esma, dada wa ‘janki’ milionea Diamond Platnumz. Kashindwa kabisa kulivumilia pini la ‘Am Singo’ la Konde Boy. Dunia yote inatambua, Mondi na Konde haziivi. Lakini dada mtu hakujali hilo, kajirekodi akiimbia goma hilo na kutupia ‘klip’ insta. Bonge moja la pini. Afrika Kusini, wakati ule wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi wa makaburu. Ni muziki uliowakutanisha, uliowaliwaza na uliowatia mori na ari ya mapambano. Pia uliwafariji sana. Hata leo wakiimba ‘toni’ yao ina upekee kama wanahuzunika hivi.

Mwanzoni mwa uhuru wetu. Wasanii kama Mzee Moses Nnauye (apumzike kwa amani). Ni moja ya watu waliofanya Taifa zima la Tanzania liimbe. Kuanzia kwenye viunga vya shule, mchakamchaka, mitaani na majumbani. Ni nyimbo zilizofanya tumuone mkoloni kama kitu kibaya sana, tumchukie sana Idd Amin Dada. Tukamuona kama joka kuu linalokula nyama za watu na tujue ubora wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Kila ubongo wa mwanadamu bila kujali umri hupokea muziki anaoupenda. Wengi husikiliza muziki kwa matumizi tofauti. Kama vile kusoma huongeza umakini kwa baadhi ya watu. Hata mazoezi utafanya zaidi muziki ukiwepo.

Katika kila jamii unayoifahamu duniani ina aina yake ya muziki. Kiroho, kimila, matambiko, kuifikishia ujumbe kuonyana na kufundisha. Kanisani nyimbo husaidia watu kuhama kabisa na kufika katika ulimwengu wa kiroho.

Muziki hukumbusha matukio tuliyopitia. Huleta hisia kali sana. Ukiwa na mawazo, ukasikiliza wimbo wa huzuni, badala ya kuliwazwa utaongeza ‘stresi’. Ukitemwa na pisi kali yako, kisha ukasikiliza dude la ‘Hayakuwa Mapenzi’ la Sugu. Utalia.

Lakini ngoma za kizazi cha Kikwete hiki. Kuzisikiliza ni kama kumkaribisha ibilisi ‘geto’. Kuna ngoma unatamani usikilize kwa ‘iafoni’ mwanao asisikie. Huku wewe akilini ukipanda mbegu ya ibilisi. Kuanzia lugha na maana ya wimbo wenyewe.

Siyo kila kumbukumbu ni nzuri. Kuna ‘taimu’ ngoma huleta ‘memori na filingsi’ mbaya. Ndio maana kuna watu wakisia wimbo fulani huishia kulia. Kwenye huu muziki kuna hasi na chanya. Kazi kwako kusikiliza kinachojenga au kubomoa. Asilimia kubwa ya nyimbo za sasa hivi utapata changamoto kwenye maudhui. Madogo wanakosa ‘kontenti’ na lugha flani hivi ya staha. Siwezi kusema wote lakini asilimia kubwa wana wenge hilo. Msanii anakuimbia chomeka, chomoa, chomeka, chomoa. Kweli?

Siyo zamani, ni juzi tu hapa (wasanii), wanamuziki walikuwa wanafanya kwa ‘pasheni’. Hata ‘fani bezi’ yao ilihitaji zaidi ujumbe. Na miundombinu haikuwa vizuri ukilinganisha na sasa. Leo wamejikita kwenye muziki wa kucheza sababu kumbi za starehe ni nyingi. ‘Long taimu’ walikuwa na pini flani zina maadili na zinaelezea stori flani. Ngoma zilikuwa kali maana zilijaa ubunifu wa kipekee. Tatizo kubwa wasanii walikuwa hawaingizi mtonyo mwingi. Tofauti na masela wa sasa. Kizazi cha 2000, wana ‘vaibu’ tu, mambo ya kuelimishana ‘hayapogo’. Wanaenda kama kuku aliyekatwa ‘hedi’ na kuachwa atapetape tu. Na wasanii nao wananata na ‘biti’ la akili mbovu za kizazi hiki. Soko linawatuma kuimba mitusi mkurabita na mkukuta. Ngona zimejaa maneno ya shombo na ovyoovyo. Ichomeke, inama, panua, kwa mpalange, nina hamu. Na upuuzi kibao ila wasanii wanapiga pesa kinomanoma kupitia ngoma hizohizo. Unataka masela waimbe ufugaji wa bata mzinga na nyuki wadogo? Tuna wakati ngumu sana. Mtoto wa leo anajua neno ‘Sitaki’ litamkwe ‘Chitaki’. Na kibaya zaidi hata matendo ya kila siku ya wanamuziki wa sasa ni ya ovyoovyo. Na yanaonekana kirahisi kwa sababu wapo katika uso wa dunia iliyo wazi kama vazi la kahaba. Watoto wanaona. Mastaa wengi wa muziki, filamu na fani mbalimbali, wana mashabiki wengi mitandaoni. Ukitaka kujua mastaa hao wanafuatiliwa na watu wa rika gani nenda kasome ‘komenti’ zao. Miandiko inakupa picha kuwa ni vijana wadogo.

Vipi miaka 10 ijayo tutakuwa na kizazi cha aina gani? Kama kizazi cha sasa tu kimeweka kambi moja na ibilisi. Kifupi kizazi cha sasa kipo ‘pri-siizoni’ na ibilisi kwa ligi ya miaka kumi ijayo. Wameweka kambi pamoja kwa kutaka ama kutotaka kabla ya kuingia ‘fildi’ rasmi. Ukweli ni kwamba. Kama sisi tulisaidiwa na muziki kuelewa dunia ilivyo. Sioni ni vipi kizazi hiki kitasaidiwa na muziki huu kuuelewa ulimwengu wetu. Ni dhahiri kabisa muziki wa sasa siyo tu hauna kitu cha kuiweka sawa jamii, bali hata hapa unatuondoa. Madhara ya sauti za wanamuziki hawa wa sasa, huwezi kuyaona kesho. Miaka kumi ijayo tutakapokuwa na makaka na madada wa ovyo. Hili siyo tatizo la wanamuziki wetu pekee, ni jamii nzima imekuwa ya ovyo mno. Maombi yanahitajika.

Achana na nyakati zile za Nuhu, mpaka wakati wa Nabii Rutu na Sodoma yake. Leo hii wanadamu tupo ‘fildi’ moja na shetani. Yaani kuna ‘kakorabo’ flan hivi na ibilisi tunakafanya.