Zijue sababu za kuku kunyonyoka manyoya

Muktasari:
Baada ya kutazama magonjwa yanayoshamiri zaidi wakati wa mvua kwenye makala yaliyopita, ni wito wangu kwa wafugaji wote kufuata kanuni za ukingaji magonjwa hasa kila inapotokea mabadiliko ya hali ya hewa.
Karibu tena katika ukurasa wa ufugaji wa kuku, ili ujue mengi kuhusu sekta hii inayopendwa na walio wengi.
Baada ya kutazama magonjwa yanayoshamiri zaidi wakati wa mvua kwenye makala yaliyopita, ni wito wangu kwa wafugaji wote kufuata kanuni za ukingaji magonjwa hasa kila inapotokea mabadiliko ya hali ya hewa.
Tuliona magonjwa mengi hulipuka wakati wa mvua, kipindi ambacho maeneo mengi yanajiandaa kutoka kuingia kwenye Kiangazi. Natumai msomaji wangu unafuatilia na kutunza kumbukumbu zinazokusaidia katika hatua za ufugaji.
Baadhji ya kumbukumbu muhimu ni pamoja na kutunza kalenda ya utoaji chanjo kwa magonjwa hatari ya kideri na gumboro.
Kideri na gumboro ni magonjwa ambayo husumbua sana nyakati zote na huenea haraka wakati wa kiangazi.
Kuku kunyonyoka manyoya
Makala ya leo yatajikita katika kuonyesha sababu zinazochangia kuku kunyonyoka manyoya.
Kwa kawaida kuku huwa hawanyonyoki manyoya wakiwa wadogo hadi wazeeke. Hivyo sababu ya kwanza kunyonyoka manyoya kwa kuku ni umri.
Kuku akiwa mzee, manyoya huharibika na kunyonyoka iwe mtetea au jogoo. Kunyonyoka kwa umri hutokea baada ya kipini kirefu cha kutaga kama ni mtetea baadaye kupumzika.
Manyoya huanza kunyonyoka kuanzia shingoni, mgongoni, mkiani na sehemu nyingine. Kunyonyoka huku hufuatiwa na kuota manyoya mengine.
Tatizo hili halina njia ya kulizuia; kama kuku wamefikia hatua hiyo, mfugaji anaweza kuwapa chakula bora cha kutosha na matunzo safi ili wawahi kutoka kwenye hali hiyo.
Kabla ya kuwapa huduma nzuri unaweza kuanza kwa kuwapunguzia chakula taratibu au kuwapa chakula chenye protini kidogo wapate mshituko na kuwahi kunyonyoka kwa pamoja.
Utatakiwa kuwapa huduma bora na chakula chenye protini kwa wingi zaidi kama vifaranga kwa muda wa wiki mbili na kuwarudisha kwenye chakula chao cha kawaida baada ya kuota manyoya mapya kwa asilimia 80. Kubadilisha chakula kufanyike taratibu sio ghafla, huku ukifuata kanuni za uzoeshaji wa chakula kila unapotaka kubadilisha kama ilivyoelezwa kwenye makala zilizopita.
Pili, kuku wanaweza kunyonyoka kwa kukosa virutubisho aina ya protini kwenye chakula chao.
Kuku wenye upungufu wa protini hunyonyoka manyoya sawa na kuku wazee hata kama ni kuku wadogo walio katika rika la kukua bila kujali mitetea au majogoo.
Kuku hunyonyoka manyoya ya mgongoni na mkiani kisha huanza kudonoana kama wanaishi kwenye sakafu bandani.
Kuku wanaoishi kwenye vizimba (cages) ni vigumu kudonoana kutokana na mazingira ya vizimba kutoruhusu kudonoana.
Suluhisho la tatizo hili ni kuhakikisha unawapa kuku chakula chenye makundi yote ya chakula kwa kiwango kinachatakiwa.
Katika mchanganyiko wa chakula cha kuku, weka walau vyakula vyenye protini itokanayo na wanyama na mimea.
Protini itokanayo na wanyama unaweza kuipata kwenye damu ya mifugo iliyokaushwa, dagaa au uduvi.
Protini ya mimea unaweza kuipata kwenye mashudu ya alizeti, pamba, karanga, mawese na mazao mengine ambayo hukamuliwa mafuta na kubaki mashudu.
Soya pia ni protini safi kwa mifugo ambayo husifika na kutumika hata bila ya protini itokanayo na wanyama kama itatumika vizuri, changamoto yake ni bei kuwa juu na upatikanaji wake pengine ni mgumu.
Lengo la kutumia mashudu au makapi ya vyakula, ni kupunguza gharama za uzalishaji wa zao la kuku.
Tatu, mitetea kupandwa na majogoo mara kwa mara husababisha manyoya ya kichwani, shingoni kunyonyoka kutokana na majogoo kuparua mgongo wa mtetea kwa makucha na mdomo kushika kichwani.
Weka idadi isiyozidi kiwango kwenye mitetea, jogoo mmoja anatosha kuhudumia mitetea tisa hadi 10. Kuweka majogoo mengi ni kusababisha fujo bandani na mitetea kupandwa bila kupumzika.
Epuka kuweka majogoo wenye rika tofauti kwenye banda moja. Majogoo wadogo watapigwa na jogoo wakubwa.
Kama unafuga kuku kwa ajili ya mayai pekee bila kuangulisha, hutakiwi kuweka jogoo yoyote bandani; waache mitetea wakae wenyewe watage bila bugudha.
Nne, kubadilisha chakula mara kwa mara. Chakula pia ni sababu ya kuku kunyonyoka manyoya kutokana na mpishano wa lishe katika vyakula hivyo.
Kama unatengeneza chakula chako mwenyewe ni vema kupima kiwango cha lishe yote kwenye chakula cha kuku wako, kwani maabara za kupima chakula cha mifugo zipo karibu sehemu nyingi na gharama zake ni nafuu.
Unaweza kuchukua sampuli ya chakula chako ulichochanganya na kwenda kupima kila kitu kikaonekana na kupata ushauri wa kitaalam.
Tano, joto kali, kubanana na kukosa hewa safi bandani husababisha mshituko na maisha yasiyo na furaha.
Mshituko wa muda mrefu, kukosa maji ya kutosha na chakula kwa kugombania, ni sababu za kuku kunyonyoka manyoya. Zingatia mahitaji bora ya kuku bandani, nafasi, hewa chakula na maji ya kutosha.
Sita, wadudu waishio juu ya ngozi ya kuku kama vile viroboto, chawa na utitiri husababisha kunyonyoka manyoya endapo wataishi nao kwa muda mrefu bila suluhisho.
Safisha mara kwa mara kwa kuondoa vumbi kwa maji na kupiga dawa kabla hujaingiza kuku wapya kwenye banda. Tumia dawa za kuua wadudu hao mara baada ya kuona dalili zao katika kuku wako.