Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima haivumi lakini imo

Mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo, Dk Fidelice Mafumiko

Muktasari:

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1960, imekuwa na mchango mkubwa kwa wananchi katika nyanja mbalimbali

Ni miongoni mwa taasisi kongwe za elimu nchini zilizovuma kwa kiwango kikubwa miaka ya 1970 na 1980.

Utashi wa kisiasa na misaada hasa kutoka kwa Mwalimu Julius Nyerere ulikoleza mafanikio ya taasisi hii.

Hii ni Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), ambayo moja ya mafanikio makubwa katika historia ya uhai wake ni kusaidia harakati za Serikali ya awamu ya kwanza kuhakikisha Watanzania wanajua kusoma.

Ni kweli kwani miaka hiyo zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa Tanzania walijua kusoma, kitendo kilichoifanya nchi itunukiwe tuzo maalumu na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).

Hata hivyo, takriban miongo mitatu baada ya mafanikio haya ya kupigiwa mfano duniani, idadi ya Watanzania wanaojua kusoma imepungua hadi kufikia asilimia 68.

Aidha, TEWW ambayo ni mdau mkuu wa harakati za Watanzania kujua kusoma, kinaonekana kuwa chombo kigeni kwa wananchi wengi.

Hii ni kwa kuwa kwa kizazi cha sasa, dhana ya elimu ya watu wazima ni ngeni. Kwa mfano, wengi wamekuwa wakiinasibisha elimu ya watu wazima na mpango wa kisomo cha ngumbaru uliokuwa maarufu zamani.

Wasichokifahamu ni kuwa elimu ya watu wazima ni eneo pana la elimu linalojumuisha elimu ya msingi, sekondari, elimu ya kujiendeleza, ufundi, elimu ya juu na hata elimu kwa maendeleo ya fani fulani.

Mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo, Dk Fidelice Mafumiko anasema TEWW ipo imara na itaendelea kusimamia falsafa za Mwalimu Nyerere zilizosukuma kuanzishwa kwa taasisi hiyo na pia kutoa fursa ya elimu hasa kwa makundi ya wananchi wanaokosa fursa hizo ndani ya mfumo rasmi wa elimu.

“TEWW haijashindwa kupanga na kutoa huduma kama hapo awali, bali jamii na asasi zake zimeshindwa kuitumia asasi hii muhimu hasa katika kipindi hiki cha ushindani mkubwa wa kiuchumi na kimaisha,” anaeleza.

“Malengo yaliyofanya Serikali ya Tanzania kuanzisha na kusimamia uendeshaji wa TEWW bado yanakidhi mahitaji ya jamii ya sasa ya Watazania.”

Kuhusu umuhimu wa dhana ya elimu ya watu wazima ambayo inawezekana ndiyo sababu ya chombo hicho kuangaliwa kwa jicho la pembeni na jamii, anasema dhana hiyo imejengwa katika falsafa imara kuwa mwanadamu anapaswa kujifunza katika hatua zote za maisha yake.

“Ukweli wa jambo hili ndiyo uliomfanya Mwalimu Nyerere kukazia utoaji, usimamizi na ufanyaji wa tathmini ya elimu ya watu wazima. Elimu hii inahitaji na inapaswa kuhimizwa na asasi zote za kiserikali kwa uzito ule ule kama ilivyo kwenye mfumo rasmi wa elimu,” anafafanua.

Ukuzaji wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu

Tofauti na zamani, mfumo wa elimu nchini hivi sasa unakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwapo kwa wahitimu wa elimu ya msingi wasio na maarifa ya kutosha ya stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu, maarufu kwa kifupi cha KKK.

Kwa kutambua kiini cha tatizo shuleni, Dk Mafumiko anasema taasisi yake imelivalia njuga suala hilo kwa kuanzisha mpango maalumu unaolenga kuwawezesha walimu kufundisha stadi hizo kwa ufanisi.

“Mpango tuliouanzisha kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi chini ya Matokeo Makubwa Sasa, ni kuwaandaa walimu watakaokwenda kupambana na KKK na matokeo ya mpango huu yataanza kujitokeza miaka mitatu ijayo,” anaeleza.

Matarajio ya TEWW

Ukiondoa changamoto kubwa ya kukosa bajeti ya kutosha kufanikisha shughuli za taasisi, ambayo hata hivyo anasema Serikali inaifanyia kazi, Dk Mafumiko anabainisha kuwa wanajipanga kuboresha shughuli za taasisi ili iendelee kuwa chachu katika maendeleo ya jamii hasa katika nyanja za kijamii, teknolojia, uchumi na siasa.

“Kuanzisha kituo maalumu cha taifa cha machapisho ya elimu ya watu wazima, maendeleo ya jamii na mambo mtambuka chenye kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano ili kurahisisha mawasiliano na pia kwenda na mabadiliko ya sayansi na teknolojia,” anaeleza mkakati mwingine.

Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ilianzishwa mwaka 1960 kama sehemu ya kitengo cha mafunzo ya ziada cha chuo kikuu kishiriki cha Makerere Kampala, Uganda ambacho kilikuwa chini ya chuo kikuu cha London, Uingereza.

Ilipofika mwaka 1963 taasisi hiyo ikawa chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama idara ya elimu ya watu wazima. Taasisi hiyo iliendelea kukua na kupata hadhi ya kuwa shirika la umma linalojitegemea na kutoa huduma nchini chini ya Sheria ya Bunge Na 12 ya mwaka 1975.

Mwaka 2005, TEWW ilisajiliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) na kupata ithibati kamili mwaka 2009 ya kutoa mafunzo ya elimu ya watu wazima na na maendeleo ya jamii katika ngazi za astashahada, stashahada na shahada.