Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Neema kuzishukia shule 17 kongwe nchini

Muktasari:

  • Baadhi ya shule hizo zimekuwa zikiwekewa mikakati ya kupandisha kiwango cha ufaulu, huku wakuu wa shule wakiwajibishwa kwa kuhamishwa au kushushwa vyeo.
  • Maamuzi hayo yanaweza yasiwe mwarobani kwa kuwa ufaulu wa mwanafunzi yeyote unachangiwa na mambo mengi ikiwamo miundombinu rafiki ya kujifunzia.

Aghalabu, matokeo ya mitihani ya kidato cha nne na tano yanapotangazwa, Serikali, wadau wa elimu na wazazi wamekuwa wakielekeza lawama kwa walimu wa shule zilizofanya vibaya.

Baadhi ya shule hizo zimekuwa zikiwekewa mikakati ya kupandisha kiwango cha ufaulu, huku wakuu wa shule wakiwajibishwa kwa kuhamishwa au kushushwa vyeo.

Maamuzi hayo yanaweza yasiwe mwarobani kwa kuwa ufaulu wa mwanafunzi yeyote unachangiwa na mambo mengi ikiwamo miundombinu rafiki ya kujifunzia.

Hali ya shule za Serikali

Miaka ya nyuma shule nyingi za sekondari za Serikali zilipata umaarufu kutokana na kufaulisha wanafunzi wengi huku zikiwa na miundombinu ya kuvutia kwa utoaji wa taaluma.

Hata hivyo, sasa hali imekuwa tofauti. Shule hizo zimepoteza umaarufu na nyingine zimeshuka kitaaluma kwa kiwango kikubwa.

Miongoni mwa shule hizo zilizojizolea umaarufu ni pamoja na shule ya sekondari ya wavulana Mzumbe na ya wasichana Kilakala zilizopo mkoani Morogoro ambazo miaka nyuma zilikuwa zikitamba kila mwaka.

Pamoja na shule hizo kuwa za vipaji maalumu, lakini mazingira yake hasa majengo na miundombinu mingine hayafanani na vipaji vya wanafunzi wanaosoma katika shule hizo.

Mwanafunzi Wiliam Kihanza wa kidato cha tatu shule ya sekondari Mzumbe, anasema kuwa majengo ya shule hiyo hayana sifa ya kuitwa shule ya vipaji maalumu na kwamba hilo linaweza kuchangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu.

“Nilipochaguliwa kuja hapa Mzumbe nilifurahi kwa sababu niliwahi kusikia baadhi ya viongozi walisoma shule hii, hivyo nilidhani miundombinu na vifaa vipo katika ubora. Hata hivyo, nilipofika hapa sikuamini kama ndio Mzumbe iliyokuwa na umaarufu miaka ya nyuma,” anasema.

Anafafanua kuwa pamoja na uchakavu wa majengo pia miundombinu ya maji na umeme nayo imechakaa, hivyo kusababisha tatizo la upatikanaji wa maji safi na umeme wa uhakika

Wakati wa kiangazi wanalazimika kutumia muda wa masomo kwenda kutafuta maji nje ya shule kwa ajili ya matumizi ya chakula na usafi binafsi.

Kihanza anasema mabweni na madarasa nayo yamechakaa; dari, madirisha na milango imeoza na kuning’inia hali inayohatarisha usalama wao na kuongeza kuwa vyoo vilivyopo havina ubora na havikidhi wingi wa wanafunzi waliopo shuleni hapo.

Changamoto hizi zipo pia kwenye shule ya Sekondari ya wasichana Kilakala. Wanafunzi hao wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa uzio na hivyo kuwafanya waishi kwa mashaka na wengine kutoroka kirahisi.

Diana Mwikila ni mwanafunzi wa kidato cha tano shuleni hapo, anaeleza changamoto nyingine kuwa ni maabara ya shule hiyo kutokuwa na vifaa vya kutosha vya kufanyia majaribio ya kisayansi, hali inayowafanya washindwe kufaulu vizuri masomo ya sayansi.

Mwalimu Alfred Mdende anasema ili mwanafunzi aweze kuelewa vizuri lazima majengo anayoyatumia yakiwamo madarasa, mabweni, maabara na maktaba yawe bora na yenye kuvutia ili apende kubaki shule kipindi chote cha masomo.

“Kutokana na shule hii kuwa ya vipaji wanafunzi wengi wanapochaguliwa kuja hapa wanategemea wakute maisha ya tofauti na shule zingine za kawaida lakini badala yake wanakutana na changamoto kama hizi,’’ anasema na kuongeza:

‘’Yapo mabweni ambayo madirisha yake, vioo vimevunjika hivyo baridi na mbu wanapenya na mara kwa mara wanaugua malaria kutokana na hali hiyo baadhi ya wanafunzi muda mwingi wanawaza maisha ya nyumbani kwao kuliko masomo.”

Kwa upande wa walimu, kilio chao cha pamoja kwa shule zote mbili ni uchakavu wa nyumba zao ambazo zilijengwa miaka mingi iliyopita na kwamba hazijawahi kufanyiwa marekebisho tangu zilipojengwa.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mzumbe, Wenceslaus Kihongosi anasema ubora wa nyumba za walimu, mazingira na miundombinu ya shule, unachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wake

Mwokozi apatikana

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imeanzisha mradi wa kukarabati shule kongwe za sekondari hapa nchini, lengo likiwa ni kuboresha miundombinu na mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ambayo inachangia kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.

Kaimu mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Graceana Shirima anasema shule nyingi kongwe zimepoteza umaarufu wake kutokana na kushuka kwa kiwango cha elimu na kuchakaa kwa majengo.

Shirima anasema mradi huo utatekelezwa kwenye shule kongwe 17 zikiwamo Mzumbe na Kilakala ambapo awali shule 88 zilizofanyiwa upembuzi yakinifu wa kubaini hali ya uchakavu wa shule hizo ambazo miaka ya nyuma zilijizolea umaarufu.

Anasema mradi huo utagharimu Sh17 bilioni huku kila shule ikitarajiwa kugharimu Sh1 bilioni. Katika awamu ya kwanza, shule 10 zitaanza kufanyiwa ukarabati. Kwa Mzumbe na Kilakala anasema tayari Shirika la Nyumba NHC imeshapewa tenda ya kufanya ukarabati ulioanza kutekelezwa kuanza Juni mwaka huu.

Wasemavyo wadau wa elimu

Baadhi ya wadau wa elimu mkoani Morogoro, wanasema shule hizo zimesaidia kuimarisha uzalendo, umoja na upendo kutokana na kuwa na mchanganyiko wa wanafunzi wanaotoka mikoa mbalimbali.

Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Mvomero Othman Sanga, anashauri pamoja na TEA kufanya ukarabati wa shule kongwe, uwekwe mpango wa kuziwezesha shule hizo mitaji itakayowasaidia kujitegemea na kufanya ukarabati mdogo badala ya kuziacha na kusubiri Serikali kuzifanyia ukarakati.

“Kama shule hizi zingekuwa na vitega uchumi vingesaidia kupata fedha za kufanya ukarabati mdogo hata wa kupaka rangi mabweni, kununua samani na kuboresha miundombinu. Kitega uchumi hicho kinaweza kuwa ufugaji na kilimo,” anasema.

Sanga anasema lazima shule hizi kongwe zithaminiwe na zienziwe ili ziweze kuwa na mazingira bora ya utoaji elimu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma zilipopata umaarufu kutokana na kufanya vizuri kitaaluma.