Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Haja ya kuendeleza uwezo na vipaji vya watoto shuleni

Muktasari:

  • Wanaolia ajira ni watu wa makundi yote; waliopata elimu na wale ambao hawakufanikiwa kuipata kutokana na sababu mbalimbali. Kwa wenye elimu kuna kitu wanachokimudu nje ya taaluma zao ila hawakukitambua mapema.

Japo suala la ukosefu wa ajira ni jambo linalosumbua dunia nzima, tatizo ni kubwa zaidi katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania.

Wanaolia ajira ni watu wa makundi yote; waliopata elimu na wale ambao hawakufanikiwa kuipata kutokana na sababu mbalimbali. Kwa wenye elimu kuna kitu wanachokimudu nje ya taaluma zao ila hawakukitambua mapema.

Kimbilio la wengi hivi sasa ni katika shughuli za kujiajiri, hata hivyo kwa Tanzania wanafunzi bado wanaendelea kusoma masomo yaliyo kwenye mitalaa ambayo kwa kiwango kikubwa hayawapi fursa ya kupata stadi za kujiajiri.

Mkazi wa Yombo Buza jijini Dar es Salaam, Manase Jason anaamini kuwa uwezo binafsi ni zaidi ya taaluma ya darasani, kwani mtoto akiendelezwa katika uwezo wake atapata mafanikio zaidi.

“Tunaona kuna wanaosoma lakini hawana msaada kwa jamii yao na wengine hawasomi, lakini vipawa vyao vinawasaidia kuendesha maisha yao na wakati mwingine kuhudumia jamii. Ndiyo maana wenzetu wanaendelea kuliko sisi kwani wanamlea mtoto kwa kukuza kipaji chake,” anasema.

Mkurugenzi mkazi wa kampuni ya Trademark East Afrika, John Ulanga anasema ni muhimu kwa wanafunzi kuwezeshwa kushikamana na vitu wanavyopenda kwa kuwa ndiyo njia ya kupata mafanikio.

“Kusoma ni muhimu lakini lazima tuendeleze uwezo na kipaji ulichonacho nje ya masomo, kuna mambo yanayofanywa na wanafunzi yanayochukuliwa kimzaha, lakini yana maana kubwa na yanaweza kubadilisha maisha ya mtu na jamii kwa jumla,” anaeleza.

Tuzo kwa wanafunzi

Kutokana na umuhimu wa kutambua uwezo wa watoto nje ya masomo ya darasani, Taasisi ya Great Hope Foundation (GHF) imeanzisha tuzo zijulikanazo kwa jina la Uwezo Award kwa ajili ya kuhamasisha utambuzi wa vipaji na uwezo wa wanafunzi shuleni.

Mratibu wa tuzo hizo, Noelle Mahuvi anasema lengo lao ni kuwafikirisha vijana wadogo waliopo shuleni watambue uwezo wa ziada, ili wajue namna wanavyoweza kuishi na kufikia malengo na ndoto zao.

“Waanzilishi wa GHF tuliona umuhimu wa kuiinua elimu katika nchi yetu kama inavyotakiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF), ambalo husisitiza elimu bora kwa watu wote sambamba na kumwendeleza mtu katika uwezo binafsi, anasema.

Anasema, “Katika utafiti tulioufanya tulibaini shule nyingi zina klabu mbalimbali lakini hazitumiki kuendeleza uwezo wa wanafunzi nje ya masomo. Tumegundua kuna wanafunzi wengi wanaoweza kufanya kazi za sanaa za mikono kama kuchora; wengine wanaweza kungiza, kuimba na hata kucheza michezo mbali mbali.”

Mahuvi anasema Tanzania kuna shule chache zenye miundombinu na mfumo mzuri wa kuendeleza wanafunzi wenye vipaji na uwezo binafsi, ndiyo maana ni wajibu wa kila mwanajamii kusaidiana na wadau wa elimu na maendeleo ya vijana.

Kutambua vipaji vya watoto

Februari mwaka 2016, GHF ilianzisha shindano lililoshirikisha shule 20 za Mkoa wa Dar es Salaam na kutaka washiriki kubuni jambo lolote la kuhudumia jamii.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Zanaki waliibuka na ushindi wa kwanza baada ya kuandaa maonyesho ya mavazi na kisha fedha zilizopatikana kutumika kupaka rangi katika zahanati ya shule yao. Wengine walilima bustani za mboga na kuuza kisha kunua mashuka ya shule na madawati. Mahuvi anasema mafanikio hayo yanaonesha kuwa endapo wanafunzi wote wakisaidia katika kuonyesha uwezo walionao, wataweza kusaidia jamii na wao wenyewe kwa kiasi kikubwa.

Teckla Tchulte ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Zanaki anayesema kupitia majaribio waliyopewa, aligundua kuwa wanafunzi wana uwezo mkubwa wa kufanya mambo ya kijamii ikiwa watapewa nafasi ya kufanya hivyo.

“Kama wanafunzi tuna mchango katika jamii, ile nafasi ndogo tuliyoipata tulijitoa na kuweza kuonyesha uwezo tulionao, hivyo kuna haja ya kulifanya suala hili la kutambua uwezo kuwa la kitaifa ili nchi nzima inufaike,’’ anasema.

“Kama Serikali, walimu na wazazi watakuwa na nia ya dhati katika kuibua, kusimamia na kuendeleza uwezo wa wanafunzi shuleni, itakuwa ni chachu ya maendeleo ya jamii na uchumi wa taifa hili,’’ anasema.

Mwalimu Zuhura Rashid ambaye ni mdau mkubwa wa kuendeleza uwezo wa watoto, anakumbana na changamoto ya ukosefu wa rasilimali fedha, wataalamu na muda wa kufanya kazi hiyo.

“Suala la kuwafundisha watoto ujasiriamali, kutambua uwezo wao binafsi na kuuendeleza ni masuala ambayo yanahitaji fedha kwa ajili ya kuandaa mazingira, wataalamu na hata kuyaingiza kwenye mitalaa na ratiba za shule. Tofauti na hivyo mambo haya yatakuwa yanafanyika katika matamasha na sherehe,” anasema.

Anashauri Serikali na wadau kuwekeza katika utambuzi wa vipaji vya wanafunzi kwa kutenga fedha na hata kuingiza kwenye mitalaa ya masomo.