Barabara kwa kiwango cha lami kufungua neema mkoani Ruvuma

Meneja wa Tanroad Mkoani Ruvuma, (wa kwanza kushoto) Lazack Alinanuswe akitoa maelekezo kwa Naibu Waziri Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi, na Mawasiliano, Atashasta Nditiye (mwenye kofia nyekundu) alipokagua matayarisho ya ujenzi wa Barabara ya Mbinga-Mbamba Bay hivi karibuni.Picha na Joyce Joliga
Muktasari:
Hiyo ni kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mdeme ambaye sasa anawatia shime wakazi hao kutumia fursa hiyo kuanza kubadilisha maisha yao.
Kufunguka kwa Barabara nyingi za Mkoa wa Ruvuma zilizotengenezwa kwa kiwango cha lami,kutachochea maendeleo na itasaidia kutokomeza umaskini miongoni mwa wakazi wa mkoa huo.
Hiyo ni kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mdeme ambaye sasa anawatia shime wakazi hao kutumia fursa hiyo kuanza kubadilisha maisha yao.
“Najua nchi hii inao watu wenye uwezo mkubwa kifedha, wanamiliki kampuni na mashirika na taasisi mbambali, waje Ruvuma kuwekeza kusudi wananchi waweze kupata huduma zote muhimu badla ya kuzifuata nje ya mkoa,” anasema Mdeme.
Kihistoria, Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa ile yenye fursa nyingi za kiuchumi, kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara ni wazi kunafungua fursa zaidi kwa wawekezaji hasa wafanyabiashara wadogo na wakubwa kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta mbalimbali zikiwamo za utalii, viwanda, madini na kilimo.
Mdeme anasema ardhi mkoani humo ina rutuba ya kutosha na inaruhusu kulima mazao ya aina mbalimbali. “Nawakaribisha wawekezaji wa ndani na je wasisite kuja huku, ile mikingamo ya ubovu wa barabara sasa haipo tena, tunahitaji na sisi tuwe angalau maduka makubwa ya kisasa yatakayokuwa yanauza bidhaa mbalimbali.”
Anaongeza: “Ujio wa barabara hizi pia utatusaidia hata sisi kusafiri na siyo kusafirisha mazao tu, sasa tutasafiri kirahisi kutoka sehemu moja kwenda nyingine, zitawasaidia wananchi kujifunza mambo mengi yafanywayo na wenzetu wa maeneo mengine.”
Mkoa wa Ruvuma ni sehemu yenye mzunguko mkubwa wa fedha kulingana na mazingira yake, kilichokuwa kikwamisha ni barabara za uhakika.
Lakini Mdeme anasema kujengwa kwa barabara nyingi kwa kiwango cha lami kumesaidia kufungua pande zote tatu za mkoa huo.
Anasema kwa sasa ni kwenda mikoa mingine ikiwamo ya Mtwara, Lindi na Njombe. Anasema barabara hizo zote zinaunganisha Jiji kubwa la Biashara la Dar es Salaam. “Kwa upande wa Nyanda za Juu Kusini, tumerahisishiwa usafiri wa kutoka Ruvuma kwenda Mkoani Njombe kisha Mbeya.”
Mkuu huyo wa mkoa ana wito gani kwa wananchi wa Ruvuma?
Anasema wakazi wa Ruvuma wazitumie barabara hizo kujenga uchumi imara hasa kwa sekta ya kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa mkoa huo.
“Shughuli zetu kubwa ni kilimo, na sasa tumeshautangaza kama mkoa wa kilimo, hadi Desemba 31, mwaka jana Ruvuma ilikuwa na akiba ya chakula tani Laki Tatu. Hii inaonyesha jinsi gani tunajitosheleza kwa chakula. Nahimiza wananchi wazitumie barabara kama kichocheo cha maendeleo. “Nichukue fursa hii kuwapongeza wananchi ni wachapakazi siyo wavivu wanafanya kazi, ziwe za kilimo, uvuvi na mifugo hata shughuli za biashara na ujasiriamali.”
Anasema wananchi wafanye kazi zitakazoinua uchumi kuanzia ngazi ya familia na Taifa zitakazosaidia kuongeza kipato.
Uuzaji wa mazao
Mkuu huyo wa mkoa anasema Serikali inaposisitiza kilimo na uuzaji wa mazao, si kwamba kila mkulima anapaswa kuyauza yote, hapana.
Akizungumzia maeneo ya uwekezaji, Mdeme anasema
Ruvuma inayo maeneo mengi ya uwekezaji, hadi sasa wana zaidi ya heka 5,000 ajili ya EPZ.
Eneo hilo kwa sasa linafika kirahisi na lina miundombinu yote muhimu yakiwamo maji na umeme.
Meneja wa Wakala wa Barabara tanzania (Tanroad) Mkoani Ruvuma, Lazack Alinanuswe anasema ujenzi wa barabara kutoka Wilayani Namtumbo kwenda Tunduru imeshakamlika.
Anasema barabara hiyo iliyokuwa ikijengwa na makandarasi watatu, ina urefu wa Kilimita 193.
Lakini pia Barabara ya kutoka Tunduru - Mangaka iliyojengwa na makandarasi wawili kimekamlika na kina urefu wa Kiliomita 66.5.
“Tayari Barabara ya Tunduru - Nakapanya na kutoka Nakapanya - Mangaka chenye Kilomita 70.5 kimekamilika kwa kiwango cha lami na barabara zote hivi sasa zinatumika,” anasema Injinia Alinanuswe.
Anasema kukamilika kwa ujenzi huo sasa kumefungua milango ya mawasiliano yenye uhakika kwa mikoa ya kusini.
“Awali haikuwa rahisi kutoka Songea mjini kwenda Tunduru, lakini baada ya kukamilika, kuna mabasi na magari ya kawaida mengi yanatumia barabara hiyo na watu wengi sasa hivi wanapenda kupita njia hiyo kwenda Mtwara, Lindi na Dar es Salaam,” anasema.
Je kuna changamoto gani zilizopo hivi sasa?
Injinia Alinanuswe anasema kila lenye jema halikosi changamoto. Anasema kufunguliwa kwa barabara hizo kumeongeza idadi ya magari, hivyo ajali za barabarani nazo zimeongeza hasa za malori.
Anasema ajali hizo zinaharibu vyuma vilivyowekwa pembezoni mwa barabara. Anasema Tanroad inaendelea kuwafuatilia waharibifu wa kingo hizo. “Tumeanza kuchukua hatua ya udhibiti kwa kuwaandikia chaji kwa ajili ya kurekebisha wengine wanarekebisha na wengine wanasuasua kutoa gharama hizo za marekebisho, lakini tunaendelea kuwafuatilia,”
anasema
Changamoto nyingine ni elimu kwa wakazi wanaoishi jirani na barabara ya Songea - Tunduru hadi Mangaka. “Watu wanaiba alama za barabarani, kwa mfano ‘lifrekta’ wanaiba na kuzifunga kwenye baiskeli zao, wanapaswa kupatiwa elimu ili waache.”
Akizungumzia ujenzi wa barabara Mbinga - Mbambabay ya kilomita 67 kwa kiwango cha lami, Injia Lameck anasema itaanza kujengwa muda siyo mrefu. “Barabara ya Kitai – Litui imejengwa kwa kiwango cha changarawe kwa sababu inapita kwenye makaa ya mawe, ila tunaendelea kuilinda ili kuhakikisha magari hayakwami,” anasema Alinanuswe.
Wito kwa Wananchi
Injinia Alinanuswe anasema wananchi waendelee kufurahia matunda ya Serikali lakini watambue miundombinu inayotengenezwa ni kwa faida yao na vizazi vijavyo wanapaswa kuitunza. Wasisite kutoa taarifa sehemu husika wanapombaini mtu yeyote anaiharibu hasa kwa kung’oa kingo za barabara na alama zake.
Naye Zachalia Mlimila mkazi wa Namtumbo ameishukuru serikali kwa kujenga barabara kwa kiwango cha lami kwani zimerahisisha shughuli za biashara. Anasema hivi sasa wafanyabiashara wa Namtumbo wanafanya minada yao Wilayani Tunduru na kurejea, kwani awali walilazimika kwenda siku moja kabla kutokana na ubovu wa barabara.
“Hali ilikuwa mbaya, kipindi cha nyuma tulilazimika kutumia siku nne hadi tano kusafirisha bidhaa zetu na kipindi cha masika tulikuwa tukipoteza muda mwingi, fedha na hata ndoa zetu ziliyumba, lakini sasa hali nzuri, tunafurahia kuwa raia wa Tanzania.” anasema Zachalia.
Mkazi mwingine, Matrida Mapunda anasema, wananachi watumie fursa hiyo kwenda kuwekeza mikoa ya kusini hasa biashara ya matunda, viazi, mahindi na maharage ambayo ni rahisi kusafirisha. Anasema kutokana na kukamilika kwa barabara hizo, hata biashara ya nyumba za kulala wageni mahitaji yake yameongezeka.
“Watu wanazidi kuja huku hata nyumba za kupangisha na ofisi, halafu huku tunapori la Akiba la Selous na Ziwa Nyasa, barabara hizi zitawaleta watalii wengi na wengine watahitahiji kutembelea makumbusho ya MajiMaji, watu waje kuwekeza huku,” anasemaMapunda.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Namtumbo, Christopher Kilungu anasema kufunguka kwa barabara ya Namtumbo – Tunduru kutahamasisha ujengaki wa hoteli na nyumba za kisasa za wageni kwani ardhi bado ipo ya kutosha.
Anasema,hadi sasa wilaya hiyo ina viwanja kwa ajili ya matumizi mbalimbali vipatavyo 6,742 vilivyopimwa. Anasema vilivyomilikishwa kwa watu ni 3,242 bado wanaviwanja 3,500.
“Eneo inapojengwa stendi mpya ya Namtumbo kuna viwanja 333 vinauzwa na vinahitaji waendelezaji, halmashauri inatarajia kupata Sh 2.5 bilioni kutokana na mauzo ya viwanja hivyo,” anasema.