Muktasari:
Kwa matiki hii, utendaji wao utapimwa kwa namna wanavyotekeleza dhana hii katika vituo vyao vya kazi. Ipo mitizamo mbalimbali kuhusu dhana ya diplomasia ya uchumi. Baadhi ya mambo haya yanajadiliwa katika makala haya japo kwa ufupi.
Kati ya mambo yanayotiliwa mkazo na serikali katika uhusiano wa kimataifa ni pamoja na diplomasia ya uchumi. Wawakilishi wa Tanzania nje ya nchi wanategemewa kufanya kazi ya diplomasia ya uchumi pamoja na mambo mengine.
Kwa matiki hii, utendaji wao utapimwa kwa namna wanavyotekeleza dhana hii katika vituo vyao vya kazi. Ipo mitizamo mbalimbali kuhusu dhana ya diplomasia ya uchumi. Baadhi ya mambo haya yanajadiliwa katika makala haya japo kwa ufupi.
Diplomasia ya uchumi
Wawakilishi wa Tanzania nchi za nje wakiwamo mabalozi kama ilivyo kwa nchi nyingine, hufanya shughuli nyingi za kuiwakilisha nchi. Haya ni pamoja na yale ya kisiasa, kijamii, kijeshi, kibiashara na kiuchumi pamoja na mengineyo.
Diplomasia ya uchumi ni dhana pana. Kwa lugha rahisi inaweza kumaanisha uwakilishi wa nchi nje ya nchi unaojikita katika mambo ya kiuchumi. Mambo haya ni pamoja na yale yahusuyo uwekezaji na biashara.
Kila moja kati ya haya ni jambo muhimu kwa nchi yoyote inayojihusisha kiuchumi na mataifa mengine yaani nchi yenye uchumi uliofunguka kimataifa.
Kuvutia Uwekezaji
Kati ya mambo ya msingi katika diplomasia ya uchumi ni kuvutia uwekezaji kutoka katika nchi mbalimbali.
Ili kuweza kuvutia uwekezaji inavyotakiwa yapo mambo kadhaa ya msingi ya kuzingatia.
Haya ni pamoja na kujua namna ya kuvutia uwekezaji na wawekezaji. Kuvutia uwekezaji na wawekezaji kunahitaji ujuzi maalumu.
Pamoja na mambo mengine ni lazima kujua fursa na miradi ya uwekezaji iliyopo katika nchi kwa upana wake.
Hizi ni fursa na miradi katika sekta mbalimbali za uchumi kama vile kilimo, viwanda, madini, utalii, huduma mbalimbali na kadhalika.
Fursa na miradi inaweza kuwa katika maeneo kadhaa kijiografia kama mikoa na wilaya.
Pamoja na kujua fursa na miradi ya uwekezaji katika muktadha wa diplomasia ya uchumi, ni lazima pia kujua malengo makuu, sera na mipango ya nchi kwa ujumla katika muktadha wa uwekezaji.
Vilevile ni lazima kujua utaratibu unaotakiwa kufuatwa na mwekezaji katika sekta na mradi kimahususi.
Pia, ni muhimu kujua vivutio vya uwekezaji vinavyotolewa na nchi na namna ya kuvipata.
Katika muktadha huu ni muhimu pia kujua wawekezaji wanataka nini wanapotaka kuwekeza katika nchi.
Juhudi kubwa huwekwa katika kuvutia uwekezaji. Ni vizuri pia kutia nguvu za kutosha katika kubakiza wawekezaji baada ya kuwavutia.
Ni lazima wanaotekeleza diplomasia ya uchumi kujua yote haya na zaidi sana namna ya kuyatekeleza inavyotakiwa.
Biashara
Pamoja na kuiwakilisha nchi katika shughuli za uchumi, diplomasia ya uchumi inahusu shughuli za biashara pia.
Yapo mambo mbalimbali yahusuyo diplomasia ya uchumi katika tasnia ya biashara.
Kati ya mambo haya ni pamoja na kuwezesha wafanyabiashara wa Tanzania kufanya biashara na nchi za nje kwa urahisi.
Mambo haya ni pamoja na kununua na kuuza bidhaa na huduma kati ya nchi husika.
Diplomasia ya uchumi katika eneo hili pamoja na mambo mengine, inapaswa kuwezesha wafanyabiashara kupata masoko ya huduma na bidhaa wanazozalisha nje.
Katika jambo hili wanapaswa kuonyesha ukubwa wa soko la bidhaa na huduma husika na utaratibu wa kuingia katika masoko hayo.
Pamoja na kuwezesha uuzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi, diplomasia ya uchumi inapaswa kuwezesha ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka nchi za nje kuja Tanzania.
Hii ni pamoja na kubaidi bidhaa na huduma hizo, bei zake na utaratibu wa kuzinunua ili kuziuza au kutumika Tanzania.
Pamoja na hili, diplomasia ya uchumi inapaswa kulenga katika kuwezesha wafanyabiashara wa Tanzania kushiriki katika mikutano, makongamano na maonyesho ya biashara ndani ya nchi walizopo.
Vilevile, wanapaswa kusababisha wafanyabiashara kutoka nchi walizopo kuhudhuria katika mikutano, makongamano na maonyesho ya biashara ndani ya Tanzania. Haya ni pamoja na maonyesho kama ya Saba Saba na Nane Nane.
Utalii
Katika tasnia ya diplomasia ya uchumi, shughuli za kuvutia watalii kutoka nje ya nchi kuingia nchini zinapaswa kuwamo.
Kama ilivyo kwa uwekezaji na biashara, wanadiplomasia wetu walio nje ya nchi wanapaswa kuwa wawezeshaji katika kuleta watalii nchini.
Kwa mantiki iliyotumika katika uwekezaji na biashara, lazima wajue mambo yote muhimu kuhusu utalii nchini.
Haya ni pamoja na vivutio vya aina zote vya utalii vilivyopo nchini.
Ni lazima pia waweze kutangaza na kujibu maswali ya wanaotaka kutalii Tanzania kuhusu namna ya kufika nchini katika kila kivutio cha utalii kimahususi.
Ujuzi wa wanadiplomasia
Kusudi diplomasia ya uchumi ifanyike vizuri na kwa ufasaha, ufanisi na jinsi inavyotakiwa, ujuzi wa wanadiplomasia ni muhimu.
Hii ni kweli kwa mwanadiplomasia mkuu kama balozi na timu yake yote. Kimsingi, diplomasia ya uchumi ni juu ya uchumi kuliko diplomasia tuu.
Kwa mantiki hii ni lazima wanadilomasia wafahamu vizuri na wawe na weledi kuhusu siyo tuu diplomasia, bali zaidi kuhusu uchumi.
Hata kama uchumi sio kitu ambacho baadhi ya wanadiplomasia wanakifahamu vizuri, ni ujuzi wa lazima katika kazi ya diplomasia ya uchumi.
Uzuri ni kuwa kila mara kuna nafasi ya kujifunza kile tusichofahamu kama nchi na zaidi sana kama mtu mmojammoja wakiwemo wanadiplomasia.