Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mila potofu, ukatili wa kijinsia; maadui wanaotesa Ngorongoro

Mtoto aliyepigwa risasi katika moja ya migogoro ya ardhi Ngorongoro kama sehemu ya ukatili.
Picha na Mussa Juma

Muktasari:

“Ukatili wa kijinsia upo katika  nyanja nne  ambazo ni ukatili wa kisaikolojia, kimwili, kiuchumi na kisiasa,”

NGORONGORO ni mojawapo ya wilaya sita za Mkoa wa Arusha.Wakazi wake wengi ni wa jamii za Wamasai na Batemi (Wasonjo).

Wilaya hii inapakana  na Kenya na baadhi ya mila na desturi za makabila haya makubwa zinafanana, ikiwamo suala la ukeketaji, ndoa za utotoni na maisha ya wakazi wengi kutegemea ufugaji na kidogo kilimo.

Hata hivyo, wilaya hii  inatajwa ni miongoni mwa wilaya ambazo bado wenyeji wake wapo nyuma kielimu na kushindwa kukabiliana na matatizo na changamoto mbalimbali  zinazowakabili.
Matukio kadhaa ya wazazi kuwahonga mifugo walimu ili watoto wao wasifaulu mitihani ya darasa la saba ni mojawapo ya matukio makubwa wilayani humo.

Kutokana na ukosefu wa elimu ,inaelezwa jamii hiyo imeshindwa kuachana na mila potofu zilizopitwa na wakati na ambazo zinachochea ukatili wa kijinsia.

Hivyo, siyo ajabu kusikia taarifa ya matukio ya  ukatili huo a mara nyingi waathirika wamekuwa ni watoto wadogo hasa wa kike, wanawake au vijana wadogo wa kiume.

Taarifa ya  Polisi wilayani  humo kupitia dawati la jinsia zinaeleza kuwa matukio ya ukatili yamekuwa yakiongezeka na  kati ya  mwaka 2010 hadi 2012, matukio  1,057 yaliripotiwa na baadhi yake kufikishwa mahakamani.

Mkuu wa Dawati la Jinsi wa Polisi Loliondo, Mary Maro anasema  amekuwa akipokea kesi au malalamiko  ya  watoto wadogo kulazimishwa kuozwa ,kukeketwa, wanawake kupigwa na kunyang’anywa mali na kuzuiwa watoto kwenda shule.

“Yote haya ni baadhi ya matukio ya ukatili, lakini tumekuwa tukipambana na hali hii siyo kwa kuwakamata watuhumiwa pekee, bali pia kuwaelimisha madhara ya matendo yao kwa jamii yao,” anasema Maro.

Kutokana na  ongezeko la matukio haya, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwa kushirikiana na mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali Wilaya ya   Ngorongoro(NGONET) na shirika la kimataifa la  Oxfam mwaka jana waliandaa tamasha la jinsia ili kusaidia kutoa elimu ya kupinga ukatili.

Tamasha hili,pia lilifanya tathmini ya maeneo ya kipaumbele ya mikataba na maazimio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia.

Washiriki wa tamasha walitoka vijiji vyote vya wilaya hiyo walipata fursa ya kuipitia mikataba  ya kuondoa aina za ubaguzi,unyanyasaji na ukandamizaji wa haki na uonevu miongoni mwa jamii.
Pia, washiriki walipata fursa ya kuuchambua mkataba wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1984 ambao mataifa kadhaa yaliusaini ikiwepo Tanzania sambamba na maazimio ya milenia, maazimio ya wakuu wa nchi za Afrika kuhusu usawa wa jinsia ya mwaka 2004 sambamba na azimio la nchi zilizopoKusini mwa Afrika(SADC) la mwaka 1997.

Kimsingi, maazimio hayo na mikataba  ile, vyote vililenga masuala ya kupinga ukatili wa kijinsia, kutetea haki za binadamu na uonevu wa aina yoyote katika nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa .

Katika tamasha hilo, mada nyingine  zilizotolewa ilikuwa ni  kuhusu mila na desturi,umiliki wa rasilimali kwa wanawake, umuhimu wa elimu kwa jamii hizo na suala zima la ndoa na ushiriki kwa vijana katika kupanga na kuamua maisha yao.

Matukio ya ukatili
Lilian Mbunito ambaye ni Ofisa Maendeleo ya Jamii wilayani  Ngorongoro akitoa taarifa katika tamasha hilo, lililofanyika Ololosokwan anasema chanzo cha kukithiri kwa matukio ya ukatili ni kushamiri kwa mfumo dume.

“Ukatili wa kijinsia   upo katika  nyanja nne  ambazo ni ukatili wa kisaikolojia, kimwili, kiuchumi na kisiasa,” anasema Mbunito.

Anataja baadhi ya matukio ya kutisha ya ukatili  kuwa ni pamoja watoto wawili wa Kijiji cha Eyasimdito kwa kupondwa vichwa, kukatwa mikono  na kupigwa na kukatwa mikono yote  kwa Theresia Mariki katika Kijiji cha Ololosokwan.

Mbunito anaeleza   Sooi Sadira (12) aliuawa baada ya kugoma kuolewa na mtoto mwingine, Bakuyet Oliokulwo wa miezi sita alivunjwa mikono na miguu na baba yake.

Anaeleza kuwa tukio jingine  ni la Meyasi Kasukia wa Kijiji cha Eyasimdito aliyepigwa na kulazwa kutokana na mgogoro wa ardhi na  mtoto Abia Makoye wa Kijiji cha Wasso aliyeunguzwa mikono kwa kuiba biskuti na juisi. “Haya ni baadhi ya matukio ya ukatili ambayo  yanadhihirisha jinsi ilivyo muhimu kwa jamii ya Ngorongoro kubadilika,” anasema. Mratibu wa NGONET Wilaya ya

Ngorongoro, Samuel Nang’irwa anasema mashirika yasiyo ya kiserikali wilayani humo, yameamua kuungana na Serikali katika vita dhidi ya  ukatili wa kijinsia baada ya kubaini kuna madhara makubwa ambayo yanapatikana. “Wito wetu ni kuwaomba viongozi wa kisiasa, kidini, kimila na wataalamu waendelee kutoa hamasa kwa jamii kushiriki kutoa taarifa na kutokomeza ukatili wa kijinsia,”anasema Nangirwa.

Kauli ya Serikali
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro,  Elias Wawa Lali anatoa wito kwa viongozi wa  mila na kiserikali katika ngazi zote kukemea na kuchukuwa hatua stahiki kwa wote watakaobainika kutenda makosa ya ukatili wa kijinsia.
“Lazima tukubaliane kuwa Ngorongoro bila unyanyasaji na ukatili wa kijinsia inawezekana, ”anasema DC Lali.

Hata  hivyo, DC huyo alitoa agizo kwa Jeshi la Polisi wilayani humo, kuzifanyia kazi taarifa zote za  ukatili wa kijinsia ikiwepo, watoto wadogo kuolewa na kupigwa na kukatazwa kwenda shule .

“Ni lazima sasa Jeshi la Polisi na viongozi wa Serikali katika ngazi zote, tushirikiane kukabiliana na hali hii na pale ambapo tukio litatokea na kufichwa basi hatua zitachukuliwa kwa kumshirikisha pia kiongozi wa eneo husika,”anasema. Hata hivyo, DC huyo anasema matukio mengi ya ukatili yanasababishwa na mila na desturi potofu hivyo ni wakati mwafaka sasa kuachwa kwa manufaa ya jamii nzima. Bado hali halisi ya ukatili  wilayani humo  ni ya kutisha licha ya utajiri mkubwa wa rasilimali ikiwamo mifugo.

Email [email protected] au simu 0754296503.