Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KONA YA WASTAAFU: Mstaafu anapotamani kuwa mbunge!

Hatimaye Bunge, lililo moja ya mihimili minne ya Taifa likiwa na wabunge wanaopaswa kuwawakilisha wananchi, akiwemo huyu mstaafu, limemaliza awamu yake ya miaka mitano, na kama kanuni zilivyo, kuchapa lapa na kurudi majimboni kuomba tena 'kula' nyingine!

Tumeona wabunge karibu 390 waliokuwa wakipata Sh14 milioni kwa kila mmoja wao kama mshahara wa mwezi, marupurupu na marapurapu mengine, wakipata kiinua mgongo takriban cha Sh300 milioni kila mmoja kwa wabunge hao wapatao 390! Ni hela nyingi ambazo hata ukiziita kwa dola bado ni nyingi vilevile!

Mstaafu amejaribu kupiga hesabu kwa kichwa chake cha kizee, na si kwa ‘kalikiuleta’, jumla ya hela zetu za madafu zilizotumika hapo na ameishia kutaka kupandisha shinikizo la damu, kwa sababu yeye, baada ya miaka 40 ya kujenga Taifa lake kwa jasho na damu, aliishia kupata kiinua mgongo wake uliopinda kwa kazi ngumu ya kujenga nchi, Sh30 milioni. Rudia hapo, milioni 30 tu kwa miaka 40!

Yaani, kwa kazi ngumu ya kukaa kwenye kiti cha kuzunguka na kuunga mkono hoja kwa miaka mitano tu, mwakilishi wa mstaafu bungeni anapata kiinua mgongo cha Sh300 milioni, wakati mstaafu mwenyewe, baada ya miaka 40 ya kujenga nchi kwa jasho na damu na kuwawezesha watu kulipana Sh14 milioni kwa mwezi anapata kiinua mgongo cha Sh30 milioni 30! Kweli, shilingi yetu ya madafu hata ukiitaja kwa dola ni nyingi hivyo hivyo!

Mstaafu wetu alitaka kujitafutia kifo cha kujitakia alipojaribu kupiga hesabu ya mshahara wa Sh14 milioni 14 kwa mwezi mara wabunge 390 kwa mwezi. Jumla yake ikamtia kizunguzungu. Na alipopiga hesabu nyingine ya viinua mgongo vya wabunge, Sh300 milioni mara wabunge 390 na kisha kujumlisha na ile jumla ya mishahara ya wabunge, hakuishia kuona kizunguzungu tu, bali Kinondoni ikamkonyeza aende akawe mkazi wa kudumu huko!

Pamoja na Kinondoni kumkonyeza aende fasta akawe mkazi wa kudumu huko, anafahamu kwamba hesabu aliyopiga kwa wabunge 390 huenda ikaongezeka Januari kwenye Bunge jipya, maana katika miaka mitano iliyopita kuna majimbo mapya yameanzishwa yatakayohitaji 'wapokea milioni 14 kwa mwezi' wapya.

Hivyo, hesabu aliyopiga kuongezeka maradufu huku yeye akiishia kupokea pensheni ya Shilingi laki moja elfu hamsini tu kwa mwezi! Hakika mabadiliko yanamhusu mstaafu!

Mstaafu wetu analitazama rundo hili la warudisha fomu ili kuwania kupata ubunge, na anajikuta akitamani naye kugombea kupata ubunge, ili kufikisha bungeni kilio cha kudumu cha wastaafu wenzake wa kima cha chini wa nchi hii, ambayo inaweza kupanga mwakilishi wa wananchi apokee Sh14 milioni kwa mwezi (ambazo huenda zikapanda mwaka kesho!), lakini mstaafu wa kima cha chini aliyeijenga nchi kwa jasho na damu aishie kupokea pensheni ya Shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi!

Hii ni hela aliyojichangia mstaafu mwenyewe kwa mshahara wake. Siri-kali haijaweka mkono wake unaoeleweka kwenye pensheni ya mstaafu wa kima cha chini kwa karibu miaka 21 ya kupokea pensheni ya laki si pesa, lakini imetia mkono kwenye pensheni ya wawakilishi wa wananchi, japo huwa hawachangi chochote kwenye Sh14 milioni zao wanazopata kwa mwezi, lakini kiinua mgongo chao kinakuwa Sh300 milioni!

Hili la yeye kuwa miongoni mwa ‘waliowasha jiko na kupuliza moto’ ili kuipika keki ya Taifa, ndilo linamfanya mstaafu atamani sana kugombea ubunge ili kufikisha kunakohusika kilio cha wastaafu wenzake cha kulikoni wao wanaishia kusikia harufu tu ya keki ya Taifa ikiliwa na ‘watu’ kwa mapande ya keki bila hata kunawa mikono, wala kumkumbuka mstaafu wa kima cha chini anayeshia kupiga miayo tu!

Ni haya yanayomfanya mstaafu wetu atamani kuingia bungeni, maana wawakilishi wake walioko – na bila shaka wapya watakaoingia Bunge jipya – wanajiumauma tu badala ya kuuliza swali simple kabisa lakini gumu la: "Kwa nini wastaafu wa kima cha chini wanapokea pensheni ya Shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi kwa miaka 21, hawa wanaopaswa kuwawakilisha walalahoi wanapokea Shilingi milioni 14 (na pengine mwaka kesho kauongezwa!) mwezi huo huo?"

Ndiyo, mstaafu wetu anatamani kugombea ubunge, ateme cheche, lakini anapoona vijana wanaorudisha fomu ili kupitishwa kugombea ubunge, anakata tamaa. Kama kweli kuna mpiga kura atakayesikiliza hoja zake za kutetea wastaafu wenzake, wakati wapiga kura wanaamini kuwa wazee wa Taifa, wakiwemo wastaafu, wapo Burundi!

Mstaafu wetu amebaki kusali na kumuomba Mungu kuwa mheshimiwa kiongozi wa nchi atamchukua kuwa mmoja wa wabunge wa zile nafasi zake kumi, ili aanze mazoezi fasta ya kunyoosha mdomo wake ambao umepinda kutokana na stroke, ili akapige kelele sawasawa bungeni kwa ajili ya wastaafu wa nchi hii ambao hayuko anayewapigania. Kimawazo wako Burundi, lakini kimwili tupo hapa hapa tukibanana kupata keki ya Taifa tuliyopika wenyewe!