Uanaume ni zaidi ya kugharimikia sikukuu

Muktasari:
- Hivi yule ambaye kwa sababu moja au nyingine, hana uwezo wa kununua nguo mpya kwa watoto wake au kupika chakula kizuri cha sikukuu; je, inamaanisha amepoteza uanaume wake? Huu ndio mjadala wa leo.
Sikukuu ndio hizo zimefika; Eid na Pasaka. Ni nyakati za furaha, kusherehekea na kuonyesha upendo kwa familia.
Watoto watavaa nguo mpya, familia zitakaa pamoja kwenye meza moja kufurahia chakula kizuri na sherehe zitapigwa kisawasawa.
Kwa muda mrefu, imekuwa desturi kwamba wanaume, kama walezi wa familia, ndio wanaobeba jukumu la kuhakikisha haya yote yanawezekana.
Lakini vipi kwa yule ambaye mwaka huu mambo hayajakaa sawa? Kwa yule ambaye, kwa sababu moja au nyingine, hana uwezo wa kununua nguo mpya kwa watoto wake au kupika chakula kizuri cha sikukuu? Je, inamaanisha amepoteza uanaume wake?
Uanaume ni zaidi ya sikukuu
Wanaume tunapaswa kukumbuka kwamba uanaume haupimwi kwa uwezo wa kuwezesha sherehe za siku moja, bali kwa jitihada zetu za kila siku kuhakikisha familia inaendelea kuishi. Ni kwa juhudi zetu watoto wameenda shule, familia imekuwa na mahali pa kuishi na tumehakikisha kuwa chakula kinapatikana hata kama siyo kile cha sherehe.
Jiulize, ni mara ngapi umewahi kujinyima ili watoto wako wale? Ni mara ngapi umeamka alfajiri kwenda kazini au kutafuta riziki kwa ajili ya familia yako?
Ni mara ngapi umepambana kuhakikisha mkeo na watoto wako wanapata matibabu wanapougua? Hayo yote ni uanaume! Huo ni upendo wa dhati ambao hauwezi kupimwa kwa mavazi ya sikukuu au sahani iliyojaa pilau kuku.
Ni rahisi kujihisi vibaya ukiona wenzako wakifanya sherehe kubwa wakati wewe huwezi. Lakini kumbuka, sikukuu moja haiwezi kufuta kazi kubwa uliyofanya mwaka mzima.
Hata kama mwaka huu hauwezi kusherehekea kama ulivyopanga, usikate tamaa. Maisha ni safari yenye milima na mabonde.
Wakati mwingine mambo huwa magumu, lakini kumbuka kuwa hali yako ya sasa siyo mwisho wa safari yako.
Kuna sikukuu nyingi mbele na kwa bidii yako, mambo yatakuwa mazuri. Kilicho muhimu ni kwamba familia yako inakuthamini na inajua kuwa unafanya kila uwezalo kwa ajili yao.
Uanaume huko kwenye vitu
Kwa wanaume wote wanaohisi huzuni kwa sababu hawawezi kutimiza matarajio ya sikukuu hii, nataka mkumbuke kuwa uanaume wenu hauko kwenye mavazi ya watoto wenu au chakula cha sikukuu.
Uanaume wenu uko kwenye kujituma kwenu kila siku, kwenye mapenzi yenu kwa familia yenu, na kwenye juhudi zenu za kuhakikisha wanapata maisha bora.
Msijione duni. Msijilaumu. Mmeshafanya kazi kubwa. Kukosa sikukuu moja haifutilii mbali uanaume wenu.
Tuendelee kupambana, tuendelee kujitahidi, na muhimu zaidi, tuendelee kujipenda na kujiheshimu. Kesho ni siku nyingine, na sikukuu nyingine itakuja. Mambo yatakaa sawa.
Heri ya sikukuu za Eid na Pasaka. Nawatakia sikuu njema.