Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tuwafundishe watoto kuelewa hisia za wenzao

Muktasari:

  • Kosa letu wazazi wengi tukishakasirika hatuchagui tunasema nini kwa watoto.

Mama Hadija ana wanawe watatu wanaofuatana.  Wa kwanza, Hadija, ana miaka nane kaingia darasa la tatu. Luqman, miaka sita ndio kwanza kaanza la kwanza na Mah’mood ndio kwanza ana miaka mitatu.

Siku moja akiwa jokoni anaendelea na shughuli zake nyumbani, Hadija alimfuata na mashtaka.

“Mama! Mama! Luqman amevunja mdoli wangu.’

Luqman ni wale watoto wazungumzaji wenye utundu fulani hivi.

Kila mara Luqman hujiweka kwenye mazingira ya kujiona ana haki ya kumchokoza mwenzake, ambaye kwa hulka yake hajui kujitetea sana.

‘Luqman wewe ni mpumbavu sana,’ mama analipuka. ‘Hii tabia nimekuambia mara kwa mara uache hunisikii. Hebu muone ndio maana una kichwa kama kikapu cha kubebea mihogo. Utapata akili lini mjinga wewe?

Mama Hadija kakasirika kweli. Kinachomchukiza zaidi ni tabia ya Luqman kurudia rudia makosa yale yale na habadiliki.

‘Hebu niondokee hapa shenzi kabisa wewe. Ondoka kabla sijakupasua hilo bichwa!’

Niko sebuleni nasikia ugomvi huu wa jioni. Nawaza haya maneno makali anayoambiwa Luqman. Je, maneno haya makali yanaweza kumbadilisha tabia mlengwa?


Kosa letu wazazi

Wazazi wengi tunafanya hiki anachokifanya mama Hadija. Tukishakasirika hatuchagui tunasema nini kwa watoto. Tena kuna wakati tunasema maneno yanayoacha alama mbaya kwa mtoto.

Ukifikiria maneno haya anayoambiwa Luqman, unaweza kuona yanavyoweza kubadili namna anavyojitazama.

Naona umuhimu wa kuzungumza na mama Hadija, ambaye kimsingi ni mdogo wangu.

‘Watoto wana mambo mengi kweli. Pole mama Hadija. Umekasirika sana,’ naanzisha mazungumzo.

‘Kweli kabisa. Haya matoto yanaudhi sana,’ anajitetea mama Hadija.

Naona pengine nimsaidie afikiri upya maneno yake.

‘Hivi umemwambiaje Luqman? Sijasikia vizuri,’ namwambia huku tukicheka.

‘Jinga sana lile. Unaenda kuvunja kitu cha mwenzako na wala hufikiri anavyojisikia.’

‘Nimeona unavyojitahidi kumrekebisha. Umekasirika kweli.’

‘Nimekasirika sana,’ anaunga mkono.

‘Umemwambiaje wakati unamrekebisha?’ Kidogo ananitazama kwa jicho la kiuchunguzi.

‘Nimemwambia alivyo mpumbavu. Humjui Luqman ni mshenzi sana.’

‘Umelenga kufikisha ujumbe gani kwa Luqman?’

‘Acha kuuliza kitu cha wazi na wewe. Huoni ni mpumbavu ?’ Kanipiga kijembe huku akicheka kicheko cha aibu fulani. Nahisi hata hivyo anatafakari athari ya maneno hayo kwa Luqman.

‘Luqman kwa sasa anaamini yeye ni mpumbavu. Unalitambua hilo?’

‘…na hilo ndio lengo. Nilitaka ajue alichofanya ni upumbavu.’

‘Umewaza athari ya Luqman kujiona mpumbavu? Kweli kamkosea dada yake na wewe usingependa kuona anaendelea kukosea. Sina hakika kama maneno yale yatamsaidia kujua makosa yake.’


Mama Hadija anacheka kicheko cha aibu. Nami nacheka kicheko cha kumrudisha kwenye mazungumzo.

Kisha tunazungumza kwa kirefu namna maneno tunayowaambia watoto yanavyoweza kuathiri hisia zao. Badala ya kuwarekebisha waelewe makosa yao, tunawaambia maneno yanayoongeza tatizo.


Tunazungumza pia namna ya kutatua migogoro ya watoto na wakati huo huo tukiwasaidia kujifunza kuelewa hisia za wenzao. Hatimaye naona Mama Hadija yuko tayari kurekebisha makosa yake. Kawaita Hadija na Luqman.


‘Luqman umefanya nini kwa Hadija? Manake kaja kwangu analia.’

‘Nimetupa mdoli wake mama,’ Luqman anajitetea na kuendelea.

‘Dija alichukua penseli yangu bila kuniomba.’

‘Hadija umemfanya nini mwenzako mpaka avunje mdoli wako?’

Hadija kaona anaingizwa kwenye matatizo. Kajibu mapigo, ‘Luqman muongo mama sijachukua penseli yake.’

Mama Hadija anaona kesi imekuwa ngumu. Kaamua kuwasemea kwangu. ‘Mjomba unawasikia wajomba zako hawa?’

Naitikia. Nikaona nianze na Luqman.

‘Anko umesikia alichokisema Hadija?’ hapo nataka afikirie hisia za mwenzake.

‘Nimemsikia.’

‘Kasemaje?’

‘Nimevunja mdoli wake.’

‘Hebu niambie ulivyovunja mdole wake Hadija kajisikiaje?’

‘Mwenyewe kachukua kalamu yangu!’ Luqman kakomaa na kuhalalisha kosa lake. Kuendelea kumpa hiyo nafasi ni kumfundisha kutokuwajibika.

‘Utaniambia hiyo penseli baadaye. Umewaza Hadija kajisikiaje ulivyovunja mdoli wake? Hebu niambie alivyojisikia.’

Luqman kagundua hana pa kutokea. Kaona bora yaishe ‘Kajisikia vibaya.’

Tunazungumza na Luqman kwa muda aone athari za alichokifanya kwa dada yake. Luqman anaelewa.

‘Haya omba msamaha,’ mama anadakia. Kweli Luqman anaomba msamaha.


Tunageukia kesi yake ya penseli

‘Luqman ulisema Hadija alichukua penseli yako? Hebu tuambie ilikuwaje?’ Luqman anaona hiyo ndio nafasi ya kuanika mabaya ya mwenzake. Kaeleza. Hadija anamkatisha katisha kuweka sawa kumbukumbu. Tukaona ni muhimu na yeye ajifunze kuelewa hisia za mwenzake.

‘Hadija hebu rudia anachokilalamikia Luqman.’

Hadija anarudia kwa kurekebisha. Tunasisitiza arudie kwa maneno ya Luqman. Hadija anarudia.

‘Hadija umewaza kwa nini Luqman anakushtaki? Hata kama kuna maneno anatia chumvi umeelewa kwa nini amekushtaki?’ Tunazungumza kwa kirefu na kugundua kumbe ni kweli Luqman alikasirika na alichokifanya ni kulipiza kisasi. Hadija pia anaomba msamaha. Kesi imeisha. Unaridhika na namna tulivyoishughulikia?