Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miaka 14, matokeo ya juhudi, nidhamu ya kazi

Mr Blue.PICHA|MAKTABA

Muktasari:

Anasema kwamba kwa sasa amekuwa akitoa wimbo mmoja kila baada ya muda, hatua ambayo imemfanya aonekane kufanya vizuri hadi sasa.

Mawio na machweo hukatika kila inapoitwa leo huku vipaji vingi vikiibuka na kupotea katika familia ya muziki wa Bongo Fleva tangu aina hiyo ya muziki ilipoanzishwa nchini zaidi ya miaka 16 iliyopita.

Hata hivyo, katika safari hiyo kuna baadhi ya wasanii wameendelea kulinda heshima yao na kudumu kama wakongwe kupitia kazi wanazofanya kwenye muziki wa Bongo Fleva kwa zaidi ya muongo mmoja.

Kati ya hao waliodumu yumo Khery Sameer Rajab aliyezaliwa miaka 27 iliyopita katika familia ya watoto wanne ya mzee Sameer Alhaji Alhad Ally mwenye asili ya Sudan, akiwa mtoto wa tatu kuzaliwa.

Huyo siyo mwingine bali ni Mr Blue aliyejizolea umaarufu katika sanaa ya muziki wa R&B na Bongo Fleva akiwa na rekodi ya kuingia kwenye muziki huo na kupata umaarufu akiwa na umri mdogo kuliko wote.

Muziki unatajwa kuwa ndiyo sababu kuu na kikwazo kilichositisha safari yake ya masomo alipokuwa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Dar es Salaam.

Mr Blue ambaye alifanikiwa kupata mashabiki wengi kupitia staili yake ya kurap anasema kuwa siri kubwa ya mafanikio yake hata kuendelea kusikika hewani hadi sasa ni juhudi, nidhamu na kumtumikia Mungu.

“Mafanikio ni lazima kuwa na nidhamu ya kazi, huwezi kufika mbali kama msanii huwezi kuzingatia kanuni hizo tatu. Msanii unapokuwa na mpangilio mzuri wa kazi, ukajipanga na kufanya juhudi, lazima utafika mbali,” anasema Mr Blue.

Anasema kwamba kwa sasa amekuwa akitoa wimbo mmoja kila baada ya muda, hatua ambayo imemfanya aonekane kufanya vizuri hadi sasa.

Kuhusu chipukizi

Akizungumzia wasanii chipukizi Mr Blue anaeleza, wasanii hao wanaohitaji kutoka lazima wafikiri na kuandaa kazi nzuri zitakazokuwa na ushawishi kwa kushirikisha wasanii wakubwa.

Hata hivyo anaeleza kwamba hayupo tayari kushirikishwa na wasanii hao ikiwa nyimbo husika hazitakuwa bora.

“Chipukizi wengi wanaonekana kuwa na juhudi za kutoka mapema, lakini kazi zao nyingi wanazoandaa hazina ubora, hakuna msanii mkubwa aliye tayari kushirikishwa kwenye wimbo mbovu. Wengi ninashirikiana nao,muhimu kuwa na kazi nzuri,” anasema na kuongeza:

“Binafsi nawashauri kuzingatia mambo hayo, vinginevyo hawatafanikiwa kukomaa kimuziki.”

Mipango yake 2014

Mwaka jana, Mr Blue alifanikiwa kung’ara katika muziki kupitia wimbo wake uitwao Pesa, ulio na vionjo vya mzaha kwa vyombo vya habari katika mashairi yake.

Mr Blue anabainisha kuwa katika mwaka huu anatarajia kuandaa video ya wimbo huo wa Pesa siku chache kuanzia sasa.

“Video nikimaliza kutakuwa na kazi nyingine nyingi zinafuata, kwa hivyo mashabiki wajipange kazi nzuri zinafuata,”anaeleza.

Alianza mwaka 1999

Safari ya muziki kwa Mr Blue ilianza miaka 14 iliyopita akiwa miongoni mwa wasanii wakongwe, baada ya kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa ndugu zake waliojulikana kwa majina ya The Boy Stain na Obrey, anaowataja kuwa chachu ya yeye kuwa mwanamuziki.

Hata hivyo, anasema kuwa alitumia miaka minne kujipanga kabla ya kutoka na wimbo wake wa kwanza maarufu uliobeba jina leke la kisanii; Mr Blue, ambao uliomtambulisha katika safari ya muziki katika ulimwengu wa Bongo Fleva nchini.

Baada ya wimbo huo, Mr Blue alizidi kuonyesha uwezo wake ambapo alitoka na wimbo mwingine uitwao Mapozi, hatua hiyo ilichangia kujiongezea idadi ya mashabiki.

Pamoja na kudumu kwa miaka 14 akiwa msanii wa Bongo Fleva, Mr Blue anaweka wazi kwamba ni albamu mbili pekee alizofanikiwa kuzitoa, ambazo ni ‘Mr Blue’ na ‘Yote Kheri’.

“Sifikirii na wala sihitaji tena kusikia habari za kuandaa albamu kwa sababu hazilipi hata kidogo. Tatizo lililopo ni wasambazaji wa kazi zetu, wamekuwa ni kikwazo katika masilahi yanayopatikana,” anasema Mr Blue.

Anahitimisha kuwa mbali na kikwazo hicho, pia soko la muziki limebadilika kutokana na mashabiki kutaka kusikia kazi nzuri, wakiweka kando mpango wa kununua na albamu za muziki akieleza kuwa kwa sasa huduma za mitandao zimerahisisha kazi za wasanii kupatikana.