Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jinsi wanawake wa vijijini watakavyoinuliwa kiuchumi

Muktasari:

  • Serikali imezindua mwongozo wa uratibu na majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi ulioenda sambamba na uzinduzi wa kamati ya elimu na uhamasishaji kwa jamii

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imekuja na mkakati wa kuhakikisha uwezeshaji wanawake kiuchumi unaanzia ngazi ya vijiji na mitaa ili asiwepo anayeachwa nyuma katika ujenzi wa uchumi jumuishi.

Hilo litafanyika kupitia uzinduzi wa mwongozo wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi uliokwenda sambamba na uzinduzi wa kamati ya elimu na uhamasishaji kwa jamii itakayofanya kazi kwa miaka mitano kuanzia sasa.

Akizungumza katika uzinduzi huo leo Jumanne, Aprili 8, 2025, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amesema kujenga uchumi imara kwa jamii itasaidia pia kupunguza ukatili wa kijinsia.

Ili kukuza ujumuishi huo, Serikali iliamua kufanya mapitio ya mwongozo wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi wa mwaka 2002 kwa ajili ya kuendelea kujenga msingi wa kuimarisha majukwaa ili yaweze kuendana na haki halisi ya sasa.

Mapitio ya mwongozo huo yalianza mwaka 2023 na yalikamilishwa mwaka 2024 na sasa toleo la mwaka 2024 limeakisi mahitaji ya sasa.

Maboresho hayo sasa yanatoa mwongozo wa uundaji, uratibu na uwezeshaji wa majukwaa ya wanawake na sasa nakala za mwongozo huo zitagawiwa katika maeneo mbalimbali.

“Usambazaji huu utafanyika ili kusaidia utekelezaji wake hapa nchini siyo tu kitaifa, mikoa, wilaya bali kata, mitaa, vijiji na huko vijijini ndiyo tunapataka kwa sababu mwongozo huo unahitaji kuwa na vikundi vya wanawake vya kijamii vya kujiendeleza kiuchumi ambavyo vikisajiliwa ndiyo vinaunda majukwaa haya,” amesema.

Kupitia kusajiliwa kwa vikundi hivyo baadhi ya viongozi watakuwa wanawakilisha vikundi vyao katika ngazi zinazofuata, mfano kutoka kijiji kwenda kata hadi mkoa na baadaye hadi Taifa.

“Lengo letu ni kuhakikisha dhana ya uchumi inagusa watu huko chini ikiwamo kwenye kaya ambazo ziko katika mitaa na vijiji,” amesema.

Amesema kupitia vikundi hivyo wanawake watajua mambo mengi yatakayowawezesha kuimarika kiuchumi ambayo huenda kwa sasa yanafahamika kwa watu wachache ambao ndiyo wanafanikiwa kuzijua fursa na vitu wanavyotakiwa kuwa navyo.

“Sasa tunataka kila mtu ajue na itakuwa rahisi kujua kwa sababu kutakuwa na kamati ya kitaifa inayoratibu suala la elimu na hamasa jambo ambalo linafanya wadau wote wenye ajenda za kuendeleza wanawake kuratibiwa na kujulikana wako wapi ili nguvu iweze kufika hadi ngazi ya chini,” amesema Dk Gwajima.

Amesema jambo hilo sasa ndiyo litafanikisha kwa urahisi dhana ya uchumi jumuishi kwani itawezesha watu kujua hatua mbalimbali za kufanya ili kuweza kufikia masoko na namna wanavyoweza kutumia taasisi za kifedha.

“Hivyo, majukwaa haya yatakuwa ni ulingo wa kumfanya kila anayetamani kukamata uchumi aweze kuelewa vitu vinavyoweza kumtoa hatua moja kwenda hatua nyingine,” amesema.

Hili linafanyika wakati ambao Serikali imerudisha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri kwa vikundi mbalimbali kupitia mfumo wa benki, hivyo uanzishwaji na usajili wa majukwaa haya utasaidia kurahisisha vikundi hivyo kufikia fursa mbalimbali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Mihayo amesema watatoa nakala 1,000 za mwongozo wa uundaji na uratibu wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi ili kufanikisha utekelezaji wake.

“Tunaamini nakala hizi zitakuwa ni chachu ya ufanikishaji wa kazi hii, tunaamini mwongozo huu utasaidia katika utekelezaji na uratibu wa utoaji elimu kuhusu uundaji wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi na sisi kama benki tutakuwa karibu kuwapatia wanawake huduma bora,” amesema Mihayo.