Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi wanawake walioshinda uchaguzi serikali za mitaa 2024

Baadhi ya wanawake walioshinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024

Safari ya mwanamke katika uongozi hapa nchini imekuwa na changamoto kubwa kutokana na mfumo dume kukita mizizi katika jamii ya Watanzania, hivyo kuwaacha nyuma katika kushiriki kwenye vyombo vya uamuzi.

Mkutano wa Beijing uliofanyika mwaka 1995 ulikuwa chachu ya kuongeza kasi ya kupigania usawa wa kijinsia na sasa ni takribani miaka 30 imepita, huku harakati hizo zikianza kuzaa matunda baada ya wanawake kushiriki kwenye vyombo vya uamuzi.

Novemba 27, mwaka jana, ulifanyika uchaguzi wa serikali za mitaa ulioandaliwa na kusimamiwa na Ofisi ya Rais (Tamisemi). Uchaguzi huo ulihusisha nafasi za wenyeviji wa mitaa, vijiji na vitongoji pamoja na wajumbe wa maeneo hayo.

Katika uchaguzi huo, baadhi ya wanawake waliibuka kidedea baada ya kupata ushindi na kufanikiwa kuandika historia kwenye maeneo yao, kwa kuwa wanawake walioshinda nafasi hizo za uongozi tangu taifa hili lilipopata uhuru wake mwaka 1961.

Nafasi hizo ambazo zimekuwa zikishikiliwa kwa wingi na wanaume, wanawake wamebadilisha utaratibu huo na sasa wana deni kubwa la kuionyesha jamii kwamba wanawake nao wana uwezo wa kuwa viongozi.

Mwananchi limefanya mahojiano na baadhi ya wanawake walioshinda kwenye nafasi zao ambao wanasimulia changamoto walizokabiliana nazo wakati wa harakati zao za kutafuta uongozi na mikakati yao ya kuwatumikia wananchi katika maeneo yao.




Simulizi za wanawake

Mwenyekiti wa kitongoji cha Bondeni kilichopo katika Kijiji cha Nyalutanga, Wilaya ya Morogoro Vijijini mkoani Morogoro, Asma Kilonga anasema alipata kura 155 akiweka rekodi ya kushinda uchaguzi huo dhidi ya mwanaume aliyemfuati, Omary Mkanga aliyepata kura 10.

Asma anasema katika mchakato wa kuomba kura, alikutana na changamoto mbalimbali, ikiwemo kuombwa rushwa ya ngono.

“Nilikuwa nikifika kuwaomba kura wanaume, wananiambia nifanye nao kwanza mapenzi ndiyo wanipe kura na kwa haraka nakumbuka walioniomba hilo hawapungui sita,” anasema mwanamke huyo.

Hata hivyo, Asma anasema hali hiyo haikumkatisha tamaa kwa kuwa alikuwa akijiamini na pia mume wake na ndugu zake walikuwa bega kwa bega na yeye katika kumfanyia kampeni, hali iliyompa nguvu ya kusonga mbele.

Akieleza sababu iliyomsukuma kugombea, anasema ni kutokana na kijiji chao kutokuwa na umeme kwa muda mrefu, licha ya kuwa umeme umepita hapo kuelekea vitongoji vingine.

“Hivyo nimeona nichukue fomu ili kusimamia suala hilo kwa karibu, kwani hata walimu katika shule yetu wamekuwa wakienda kuchapisha mitihani kitongoji cha jirani kutokana na shule kutokuwa na umeme,” anasema Asma.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Miwindi kilichopo katika Kijiji cha Miwindi mkoani Mtwara, Josephine Vicent anasema katika uchaguzi huo, alipata kura 195 dhidi ya mshindani wake, mwanamume, aliyepata kura tano.

Anasema katika kampeni zake, alipata changamoto ya kuambiwa wanawake hawawezi kuongoza na hiyo yote imechangiwa na ukweli kwamba kwa miaka mingi eneo lao limekuwa na viongozi wanaume pekee.

Hata hivyo, anasema alikuwa akiwapa elimu ya umuhimu wa kumchagua mwanamke kuwaongoza katika kila mahali alipopita kuomba kura na anashukuru amefanikiwa.

“Moja ya mambo nitakayopigania katika uongozi wangu ni kupiga vita kuchezwa watoto wakiwa na umri mdogo, kwani wapo wanaochezwa hadi miaka minne na kufundishwa mambo ambayo ni makubwa kuliko umri wao,” anasema. Kwa upande wake, Leokadia Ntalaswa, Mwenyekiti wa Mtaa wa Tabirigu uliopo Kanazi, Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, anasema katika uchaguzi huo, alipata kura 24 na aliyemfutia ambaye ni mwanamume, alipata kura 21.

Leokadia anasema katika kipindi cha kampeni, wanaume walikuwa wakimkatisha tamaa kwa kumwambia lini mwanamke akaweza uongozi.

“Pamoja na maneno haya, nilikuwa nikiwajibu kuwa mbunge wetu ni mwanamke, Spika wetu ni mwanamke na Rais wetu, pia, ni mwanamke, hivyo hata mimi nitaweza kuongoza,” anasema Leokadia.

Mwanamke huyo anaeleza siri yake ya kupata ushindi kuwa ni mafunzo waliyoyapata kutoka TGNP ambayo yaliwawezesha kuzunguka maeneo mbalimbali kuangalia changamoto zinazowakabili wakazi wa kijiji hicho, ikiwemo ukatili wa ndani ya ndoa, ukatili wa kiuchumi na kupigwa.

Kutokana na matunda yaliyoonekana katika kazi hiyo, anasema anaona imekuwa moja ya sababu za ushindi huo.

Akiwa na simulizi ya tofauti na wenzake, Tatu Ambukegwe, ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mshewe kilichopo Wilaya ya Mbeya Vijijini, anasema katika uchaguzi huo hakuwa na mpinzani na badala yake alipita kwa kura za “Ndiyo”.

Katika mchakato ndani ya chama, anasema alikuwa mwanamke peke yake na alipita kwa kupata kura 150, huku akieleza kuwa bado kuna woga kwa wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali. Changamoto aliyopitia anasema ni ukosefu wa fedha, kwa kuwa katika kampeni lazima uwe na fedha angalau ya kukodi viti, lakini anashukuru kukubalika kwake kulifanya kazi hiyo ikawa rahisi kwake.


Wadau watia neno

Josephine Damas kutoka kata ya Mngazi, Morogoro Vijijini, ambaye ni mhamasishaji wa wanawake kugombea, ameshauri katika uchaguzi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufika ngazi za chini kwa kuwa huko ndiko rushwa imetawala zaidi.

Kutokana na hali hiyo, anasema wanawake wamejikuta wakiwa wanyonge kwa kuwa wanaoshindana nao, ukiacha kuwa ni wanaume, pia wanatumia nguvu zao kifedha kuwatisha na kuwashawishi wananchi kuwachagua.

Anasema pamoja na changamoto hizo, anashukuru katika kata ya Mngazi, vitongoji vitano wameshinda wanawake, huku akiahidi kuendelea kusimama nao katika uchaguzi mkuu utakaoshirikisha madiwani na wabunge.

Kwa Morogoro Vijijini, anasema wamejitokeza wanawake 72 kutaka kugombea, yote hiyo ni kutokana na elimu waliyowajengea ya kusimama kuomba kura mbele za watu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi anasema tangu kufanyika kwa mkutano huo wa wanawake, yapo baadhi ya mafanikio, ikiwamo Tanzania kushika nafasi ya pili kwa nchi za Afrika Mashariki Januari 2019 kwa kuwa na wabunge wengi kwa kupata alama ya asilimia 36.9

“Lakini pia tumeweza kupata mwanamke wa kwanza Rais na wanawake wawili wamekuwa maspika wa Bunge, matokeo yanayoonyesha wanawake wanaweza kupasua miamba kama wakijengewa uwezo,” anasema.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo anasema pamoja na mikakati iliyowekwa, bado hakujaweza kufikiwa asilimia 50 kwa 50 inayotakiwa katika uongozi.

Anasema kwa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 ulionyesha asilimia 6.5 ya wanawake ndio waliochaguliwa kuwa madiwani, asilimia 2.1 nafasi ya wenyeviti wa vijiji, asilimia 6.7 vitongoji na asili17.6 mitaa.

Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Mkutano wa Beijing, Getrude Mongela anasema katika harakati za masuala ya Beijing, TGNP walikuwa na mchango mkubwa, ikiwemo kusambaza elimu kwa wananchi kuhusu yale wanayoenda kuyapambania katika mkutano huo.

Getrude anatoa wito kwa jamii kuendelea kupambania haki za wanawake na kuacha kuona kazi hiyo ni ya wanawake pekee. Anasema bila mchango wa wanaume, huenda asingefika hapo alipofika sasa.

“Nikianzia na mume wangu kunipa ruhusa kuingia katika kazi za uanaharakati, ilinipa nguvu.,” anasema.