Gwajima awajia juu wanaodhihaki 'Single mothers'

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalum, Dk Dorothy Gwajima
Muktasari:
- Gwajima amesema kutoa kauli mbaya dhidi yao ni kuwanyanyasa wanawake ambao wameamua kusimama na kulea watoto wao wenyewe kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufiwa au kutengana na mzazi mwenzake.
Dar es Salaam. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalum, Dk Dorothy Gwajima amewasihi wanaozungumza vibaya kuhusu wanawake waolea watoto wao wenyewe maarufu kama 'Single Mothers' kuacha tabia hiyo kwani hao ni wazazi kama wengine hivyo wanahitaji kuheshimiwa.
Gwajima ameyasema hayo jana Alhamisi jijini Dar es Salaam katika hafla iliyoandaliwa na Taasisi ya Her Initiative na kukutanisha wadau mbalimbali kuzungumzia masuala ya wanawake na uongozi.
Gwajima amesema kutoa kauli mbaya dhidi yao ni kuwanyanyasa wanawake ambao wameamua kusimama na kulea watoto wao wenyewe kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufiwa au kutokea migogoro kati yake na mwenza wake.
"Anayehamasisha hayo hana maadili na wala hajui ukuu wa mama katika dunia, cha kushangaza baadhi ya watu katika jamii wanashabikia lazima tujitafakari," amesema.
Hivyo amesema ajenda ya 'single mothers' hawafai haina tija kwani wapo kati yao ambao ni mifano ya kuigwa katika malezi ya watoto.
Wanawake katika uongozi
Gwajima amesema kadri siku zinavyozidi kwenda Tanzania inapiga hatua katika kufikia usawa wa kijinsia haswa katika upande wa uongozi.
Ametolea mfano bungeni ambao umeongezeka kutoka asilimia nane mwaka 1995 hadi asilimia 35 mwaka 2020.
Pia, amesema wapo wanawake wengine ambao ni viongozi katika maeneo mbalimbali ambao bado hawajaibuliwa ili dunia kufahamu wanachokifanya.
Hivyo wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wanakuja na mkakati wa kuwaibua wanawake wanaofanya kazi nzuri kutoka maeneo mbalimbali.
“Tunajenga mazingira yanayowezesha wanawake kustawi kama viongozi, wajasiriamali, na mawakala wa mabadiliko, Uwezeshaji wa kiuchumi ni msingi wa kushiriki kwao katika jamii”
“Tutaendelea kuhakikisha wasichana na wanawake wanapata nafasi ya kuongoza na kuandika mwanzo mpya katika historia yetu, Ni wakati wa kuvunja vikwazo na kuleta mabadiliko makubwa,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Her Initiative, Lydia Charles amesema jamii ina wajibu wa kumshika mkono binti, kumsaidia na kumuongoza ili aweze kufikia ndoto zake.
Anasema wapo baadhi ya mabinti katika jamii wana ndoto na malengo makubwa katika jamii lakini wanashindwa kuzitimiza kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo umasikini.
"Safari yangu hadi kufika hapa imenifundisha kuwa uwezo upo kila mahali lakini si kila mtu anapata fursa ya kuuonesha, kila msichana anastahili nafasi ya kujifunza, kukua, na kufanikisha ndoto zake, tukiwekeza kwa wasichana, tunajenga jamii bora" amesema.
Mwakilishi Mkazi wa UN Women, Hodan Addou amesema miaka 30 baada ya Azimio la Beijing, nchi imeendelea kupiga hatua katika elimu kwa wasichana, wanawake zaidi kwenye uongozi na uwepo wa sheria zinazowalinda
Hata hivyo amesema bado safari ya kuwezesha wanawake bado inaendelea na kuitaka jamii pamoja na wadau mbalimbali kuunga mkono.
"Uwezeshaji wa wanawake siyo tu una umuhimu kwa wanawake wenyewe bali jamii nzima, ukimuwezesha mwanamke umeliwezesha taifa," amesema.
Kwa upande wake Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania Peter Huyghebaert, amesema usawa wa kijinsia ni jambo la msingi kwa maendeleo ya jamii.
"Tanzania na Ubelgiji zitaendelea kushirikiana kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa katika elimu, ajira na uongozi," amesema.