Kuna kosa kulinda nikipendacho?

Anti naomba unisaidie, mpenzi wangu ana shepu nzuri sana (sijui wengine wakiiona watasemaje), lakini mimi napagawa kila ninapomuona, sasa sitaki mtu mwingine aione, changamoto mpenzi wangu hataki kuvaa nguo za kuificha, jambo linalonikosesha amani na kutishia mahusiano yetu. Kila nikimwambia ajisitiri sitaki aonekane hataki, anasema hata imani yake haijamuamrisha kufanya hivyo. Nifanyeje, nahisi kumkosa na nikiwa naye asipojisitiri nitapata kichaa, maana huwa akili haitulii, hasa akisema ametoka nje ya nyumbani. Au nakosea maana mpenzi wangu hanielewi kabisa.

Mmh ebu jitulize bwana. Kupenda shepu ya mwenza wako sawa, kuridhika na maumbile yake hasa ndiyo kinachotakiwa, lakini huko unakokwenda sasa siko. Kujisitiri hakuna dini wala kabila kila mwanamke anatakiwa kufanya hivyo, ila sababu zako nahisi ndiyo zinazomfanya akugomee.

Mwanamke hachungwi kama wewe unavyofanya, hata akivaa gunia kama ana tabia mbaya au wanaume wanataka kumuona alivyo ndani ataruhusu tu, lakini akiamua kutulia na wewe hata akivaa bikini atabaki kuwa wako.

Usikubali avae nusu utupu, lakini usije kupata presha kuwa kwa shepu aliyonayo asipoifunika watu watakunyang’anya, hapana.

Hujasikia kuwa shepu ni pembe la ng’ombe halifichiki, basi mpenzi wako pia kama anayo anayo tu hata akivaa guo kubwa itaonekana japo kidogo.

Muamini, mpe uhuru ila usiruhusu avae viguo vifupi au vya kubana sana na hilo ni kwa kila binadamu anapaswa kuishi hivyo, kwani hata mwanamume akivaa suruali ya kubana sana anatisha.

Hakuna kosa kulinda chako, lakini ukimnyima sana uhuru hamtaelewana, sijasema avae ovyo na hujasema kama anavaa hivyo ila unataka aingie kwenye nguo ambayo haitamuonyesha umbo lake, jitahidi kujenga hoja akuelewe, hivi hivi utampoteza, ninahisi anakupenda.


Nachanganyikiwa kila mtu anataka nizae, nifanyeje?

Nakaribia kupata wazimu, kila ninakopita malalamiko ni kuzaa. Wakwe, jamaa, ndugu na marafiki wote nikikutana nao salamu ni kuzaa. Hilo jambo linaniumiza kwa sababu ni mwaka wa tano sasa tangu niolewe na sijapata ujauzito, sijatumia dawa yoyote ninaamini Mungu atanipa.

Lakini kwa hizi kelele naomba nisaidie nianzie wapi kutafuta mimba ili nipate mtoto.

Maana miaka miwili iliyopita nilikwenda na mume wangu hospitali daktari akasema homoni zetu na kila kitu kipo sawa, tujiandae tu kuwa wazazi wakati wowote. Nisaidie nimeelemewa.

Unataka kuzaa kwa sababu upo tayari kufanya hivyo au kuwafurahisha wanaotaka uzae. Mwisho wa siku watoto ni wako wewe na mumeo na hujasema kama na yeye ni miongoni mwa wanaokupigia kelele hizo.

Ingawa hujasema una miaka mingapi, ila sidhani kama kuna haja ya kuhangaika zaidi ya mlichofanya na mumeo kwenda kwa daktari na kupata majibu sahihi kabisa.

Kama utakuwa unahitaji sana, nenda tena kwa daktari wenu ukamueleze kwamba mmesubiri kwa miaka miwili na hamjapata matokeo, najua atakupima au kuwapima na kuwashauri cha kufanya.

Ila siku zote miluzi mingi ilimpoteza mbwa, usiruhusu kuchanganyikiwa na jambo kwa sababu ya kelele za wanadamu, ukianza kuzaa ukawazaa mfululizo napo watakusema, ukiwapishanisha sana watasema, hujapata wanasema, angalia amani ya nafsi yako inakuambia nini.

Kufanya kitu kwa sababu ya watu wengine si busara sana. Unahitaji mtoto sawa, lakini usiende mbio kwa sababu ndugu, jamaa, marafiki na wakwe wanataka hilo litokee.

Usisahau kuolewa ni sheria kuzaa ni majaaliwa ya Mungu, kama hajapanga hata ukichanganyikiwa kazi bure. Muombe atalifanikisha hilo kwa muda autakao.