Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zaidi ya miaka 10 ya majanga, sasa vicheko shule za kata

Ziliota kama uyoga kila kona ya nchi; wengi wakaingiwa woga. Swali likawa itawezekana na walimu wa kuzihudumia shule hizo zote watatoka wapi?

Wasiwasi huo hata hivyo haukuirudisha nyuma Serikali ya yawamu ya nne na mpango wake wa kuhanikiza ujenzi wa shule za sekondari kwa kila kata.

 Wananchi wakaitikia, Serikali chini ya Jakaya Kikwete ikakoleza kasi ya uwekezaji; kuanzia miundombinu walimu hadi vifaa. Leo ni punguani pekee anayeweza kupinga mafanikio ya shule hizo.

Miaka 17 Rais mstaafu Kikwete, anakiri kuwa shule hizo zilikuwa kama zigo zito kwake lakini kwa sababu alipenda masuala ya elimu akakubali kulibeba kwa kuwa hata yeye matamanio yake ilikuwa ni kuona nchi inapata maendeleo na hilo lisingewezekana kama watu wengi hawana elimu.

“Kuanzia miaka ya nyuma hadi wakati Mzee Benjamin Mkapa anaondoka madarakani kazi kubwa ilifanyika kwenye elimu ya msingi. Zaidi asilimia 95 ya watoto wenye umri wa kwenda shule walipata fursa hiyo. Kupitia programu ya UPE tulipata mafanikio makubwa kwa elimu ya msingi.

“Kutokana na hilo upande huo haikuwa kazi kuimarisha tuliboresha kwenye upungufu, palipohitajika kujenga shule au kuongeza madarasa ilifanyika ndiyo maana mafanikio yalikuwa makubwa. Changamoto iliyokuwepo ni kwamba tuliweka mkazo kwenye elimu ya msingi hatukutoa msukumo wa kutosha kwa ajili ya elimu ya sekondari,” anasema Kikwete.

Hali hiyo ilichangia wanafunzi wengi waliokuwa wakimaliza elimu ya msingi, kukosa nafasi ya kuendelea na elimu ya sekondari kutokana na uhaba wa shule. Wakati huo ilikadiriwa ni asilimia sita pekee ya wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi, ndiyo waliojiunga na shule za sekondari.

“Ilikuwa matokeo ya darasa la saba yakitoka kila nyumba ni vilio.Wazazi wanalalamika watoto wao kufeli na watoto wanalia wakiamini huo ndiyo mwisho wa maisha.Kukawa na maneno mazuri kwamba mtoto hakufeli bali hakuchaguliwa.

“Katika Ilani ya uchaguzi niliyokabidhiwa na Mzee Mkapa kulikuwa na agizo la CCM kwamba tujenge sekondari moja katika kila kata, wakati huo kata zilikuwa zaidi ya 2,500. Tulikaa kwa pamoja na Makamu wa Rais Dk Mohamed Shein na Waziri Mkuu Edward Lowasa tukasema agizo hili ni kabambe lakini hatuna budi kulitekeleza, tutafute maarifa ya kulifanikisha,”anasema Kikwete katika hotuba yake aliyoitoa hivi karibuni jijini Dar es Salaam katika hafla ya kutambua mchango wa wadau wa elimu nchini.

Viongozi hao wajuu wakakubaliana utengenezwe mfumo wa pamoja kati ya Serikali na wananchi, ambao utawezesha pande zote kushiriki katika kufanikisha lengo hilo kwa kila upande kutimiza wajibu wake.

Makubaliano yalikuwa wananchi wajenge maboma, halafu Serikali iezeke na kutoa vifaa vingine vinavyohitajika ikiwemo walimu ili shule ianze kufanya kazi.

“Kilichotustaajabisha uamuzi huu ulipokelewa kwa nguvu kweli kweli na wananchi, badala ya kujenga shule moja katika kila kata, unaweza kukuta kwenye kata zimejengwa shule nne hadi saba tena sio maboma tu wamejenga na kuezeka kabisa. Nilienda kule Tanga hadi nikauliza hizi shue zote mnajenga watoto wapo, wakaniambia watoto sio tatizo nyie leteni walimu na vitabu,’’ anasimulia Kikwete kuhusu safari ya shule za kata.

Wanafunzi aliowakuta, kuawaacha

Anasema wakati anaingia madarakani wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita walikuwa 524,000, ila awamu yake ya uongozi ilipoisha aliacha jumla ya wanafunzi 1,800,000 katika ngazi ya sekondari, huku waliokuwa wakijiunga kidato cha kwanza wakiwa zaidi ya 500,000 kwa mwaka.

Idadi hiyo kubwa ikamdhihirisha kuwa vijana wengi walikuwa wanafaulu ila fursa ya kwenda sekondari haikuwepo kutokana na upungufu wa shule ambapo kwa sasa idadi yake zimefikia 3,000.

Furaha ya Kikwete iliongezeka maradufu baada ya kubaini mkoa wa Dar es Salaam sasa una shule 179 kati ya hizo, 170 zikiwa zimejengwa kupitia kampeni hiyo ya ujenzi wa shule za kata.

Wakati yeye anaingia madarakani jiji hilo linaloongoza kwa idadi kubwa ya watu nchini, lilikuwa na shule za sekondari tisa ambapo nane kati ya hizo Serikali ilizitafisha kutoka taasisi za dini.

Shule hizo ni Forodhani (ambayo sasa haipo), Kisutu, Azania, Jangwani, Tambaza, Zanaki, Kibasila, Pugu na Benjamin Mkapa iliyoanzishwa kwenye ngwe ya mwisho ya Serikali ya Awamu ya Tatu.

Majanga na mabonde

Awali haikuwa rahisi kwa shule za kata kukubalika kwa baadhi ya watu wakiwamo watendaji serikalini. Kulikuwa na wasiwasi wa kujenga shule hizo na kisha kushindwa kuzihudumia ipasavyo.

Kikwete anakumbushia namna aliyekuwa waziri wake wa elimu, Margareth Sitta alivyokuwa na wasiwas kama Serikali ingeweza kwenda na kasi ya ujenzi wa shule hizo.

‘’ Magreth Sitta, kuna siku alinifuata akaniambia tuwaambie wananchi waache kujenga shule nyingine maana hatuna walimu. Nikamwambia wananchi wamehamasika kujenga shule, tukisema wasiendee kujenga mpaka sisi tutakapokuwa tayari kuwapatia elimu, wanaweza kubadili mawazo,”anasema.

Kama haitoshi hata zilipoanza kazi zikabezwa hasa kutokana na uendeshaji wake kwani haikuwa ajabu kuona shule nzima ikiwa na mwalimu mmoja au wawili.

Pamoja na hilo Serikali ikaweka mipango kadhaa ya kutengeneza walimu, ndipo ilipokuja programu ya kuwatumia wahitimu wa vyuo vikuu bila kujali fani walizosomea. Hawa wakapewa mafunzo maalum ya ualimu wakiwa tayari wanafundisha shuleni.

“Tulianza kwa tabu na tulikutana na ukosoaji mwingi lakini nikasema mwanzo mgumu lakini hatuwezi kusubiri tuwe na walimu wa kutosha, ndiyo tujenge shule acha tuanze na kujenga shule. Zipo shule zilizoanza na walimu wawili tena tulichukua vijana waliomaliza vyuo vikuu bila kujali walichosomea tukawapa crush program (program ya mafunzo ya muda mfupi).

“Nikasema sasa tushughulikie tatizo la kupata walimu hapo ndipo nilipoamua mojawapo ya kozi kubwa itakayotolewa Chuo Kikuu cha Dodoma ni ualimu. Nikafanya mkutano na watu wenye vyuo binafsi nikawaomba kuhakikisha vyuo vyote viwe na vitivyo wa ualimu na ahadi ya Serikali ilikuwa ni kuwaajiri na hilo lilifanyika,”anaeleza.

Kikwete anasema jitihada zilizofanywa katika kutengeneza walimu zimefanya wengi wanaohitimu ualimu vyuo vikuu, wanaamini wanastahili kufundisha sekondari na si vinginevyo.

Aidha, kilio zaidi kikawa kwenye matokeo.

Miaka ya mwanzo shule hizo ndizo zilizokuwa zikiburuza mkia katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne.

Katika shule hizo watahiniwa kupata daraja la kwanza na la pili, ilikuwa sawa na bahati ya mtende.

Hata hivyo, miaka michache baadaye baadhi ya shule hizo zikawa mfano wa kupigiwa mfano, ikiwamo Shule ya Sekondari ya Kisimiri ya mkoani Arusha, ambayo kwa miaka kadhaa ilikuwa katika orodha ya shule kumi bora kwenye mtihani wa kidato cha sita.

 Lakini pia leo si ajabu kukuta watahiniwa katika shule za kata wakipata daraja la kwanza kwa wingi.

Wanufaika wanasemaje?

Asma Mbwana ni mmoja wa wanufaika wa shule hizi anayeeleza: “Mimi ni miongoni mwa wanufaika wa shule za kata, hatua hii niliyofikia leo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na elimu niliyopata kupitia shule ya sekondari ya kata, maana familia yangu haikuwa na uwezo wa kunisomesha shule binafsi.’’

Anaongeza: ‘’Pamoja na mazuri hayo nikiri wazi kwamba changamoto zilikuwepo katika kuipata hiyo elimu, kubwa zaidi ikiwa tatizo la ukosefu wa maabara wakati ilikuwa ni sharti la lazima kwa mwanafunzi kufanya majaribio ya kisayansi. Ilikuwa inanilazimu kulipia maabara za nje ya shule kwa ajili ya kufanya majaribio hayo..’’

Wakati Asma akieleza hayo, Jaffari Kulyunga ambaye ni mnufaika mwingine wa shule za kata, anasema kwake suala la upungufu wa walimu ndiyo ilikuwa tatizo kubwa hali iliyosababisha kutumia muda mwingi kwenye madarasa ya masomo ya ziada kuliko shuleni.

Anasema; “Sijui sasa hivi hali ikoje ila ile miaka ya mwanzoni kulikuwa na shida kubwa ya walimu. Mnaweza kujikuta kuna masomo hamna mwalimu au yupo mmoja anayefundishe madarasa mengi, hivyo hata ufundishaji unakuwa sio mzuri. Nilikuwa nalazimika kushinda mchikichini (eneo maarufu kwa utoaji wa twisheni jijini Dar es Salaam). Kule nilikuwa nakutana na wenzangu wa shule nyingine angalau tunasaidiana.’’

Wadau nao…

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet) Ochola Wayoga anasema bado kazi kubwa inatakiwa kufanyika ili shule hizo ziweze kutoa elimu bora ikizingatiwa kuwa ni tegemo kwa Watanzania walio wengi.

Wayoga anasema: “Ni kweli shule hizi zimesaidia vijana wengi wa Kitanzania kupata elimu, lakini bado inahitajika ufanyike uwekezaji mkubwa katika kuhakikisha inayotolewa ni elimu bora na sio bora elimu. Uwekezaji huu ufanyike kwenye miundombinu, zana za kufundishia na kujifunzia na walimu. Haya yakifanyika kwa pamoja, tutapata matunda tunayoyatarajia.”