Haya yakifanyika shule za kata zitatamba kitaaluma

Wengi walizibeza, kwao taswira haikuwa mahala pa kutoa wahitimu bora bali majengo yaliyojengwa kisiasa kwa ajili ya kufifisha ndoto za watoto wa Kitanzania.
Wakazipa majina lukuki ya kebehi na istihzai, hata wazazi nao hawakuwa tayari kuona watoto wao wakisoma katika shule hizo.
Hizi ni shule za kata zilizopo karibu kila kona ya nchi. Kwa takwimu za Serikali shule hizo sasa zinafikia 3,000.
Awali madai ya wale waliokuwa wakizibeza yalikuwa na nguvu. Ni kweli kuwa shule nyingi za kata hazikuwa na sifa ya kuitwa shule ndio maana ziliongoza kwa kutoa wahitimu wengi waliofeli mitihani ya taifa.
Hata hivyo, leo hadithi ya shule hizi imeanza kuchukua mkondo tofauti. Pamoja na kukabiliwa na changamoto kama vile uhaba wa walimu na miundombinu hasa maabara, shule hizi sasa zinaonekana kuwa mkombozi wa wengi.
Katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2019, shule mbili za kata Kisimiri na Mwandet, zote za mkoani Arusha zilifanikiwa kupenya na kuingia katika orodha ya shule 10 bora.
“Mwaka huu katika matokeo ya kidato cha sita shule, kati ya shule bora 100, 54 zilikuwa za kata. Sasa watoto wametokea kuzipenda shule hizi za kata na wanaohitimu na kwenda vikuu wameonekana ni miongoni wanaofanya vizuri,” anasema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo.
Jitihada za Serikali
Mafanikio haya kama anavyosema Jafo hayaja kwa urahisi. Jitihada mbalimbali zinafanyika ikiwamo kuboresha miundombinu ya shule hizo.
Anasema jambo la kwanza Serikali inaendelea kupeleka walimu katika shule hizo kwa kuhakikisha asilimia 90 ya walimu wanaoajiriwa asilimia 90 wanakwenda huko katika shule zilizojengwa kwa nguvu ya wananchi.
“Ndiyo maana utaona maeneo ya miji na manispaa hatuwapeleki walimu hawa,” anasema.
Suala jingine Serikali imenunua vifaa vya maabara ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwenye masomo ya sayansi. Tayari shule 1,960 zimeshanufaika tangu mwaka 2017.
“Mwaka huu tutapeleka vifaa kwenye shule 1,250. Kingine tunachokifanya ni kuimarisha miundombinu ya vyumba vya maabara, ili kuwapa fursa wanafunzi kusoma kwa nadharia na vitendo,” anasema na kuongeza:
“Pia tulipeleka vitabu vya sayansi na sasa hivi uwiano umekuwa kitabu kimoja kwa wanafunzi watatu.Uwiano huu siyo mbaya na msaaada wa vitabu tulipata kwa wenzetu wa Marekani.’’
Jafo anasema hivi sasa Serikali inaendelea kuandika vitabu vya sanaaa, kuimarisha na kuboresha miundombinu ya shule hizo ikiwemo kujenga matundu ya vyoo.
Hadithi ya shule ya sekondari Kisimiri
Baadhi ya watu wamekuwa na mawazo tofauti kuhusiana na shule ya sekondari Kisimiri ambayo kwa miaka ya karibuni imekuwa ikitamba katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha sita. Hoja iliyopo je, shule hiyo ni ya kata ama la
Waziri Jaffo anasema kuwa Kisimiri ni shule ya kata iliyojengwa na wananchi lakini ina sura mbili “Kuanzia kidato cha kwanza hadi nne inachukua wanafunzi wanaotoka katika mazingira ya kawaida wenye sifa za kusoma shule za kata.
“Lakini kidato cha tano na sita ni shule maalumu ambayo inachukua wanafunzi wa kitaifa wa maeneo yote kama zilivyo shule za Kibaha au Msalato,” anasema .
Anafafanua kuwa “Kwa kidato cha kwanza hadi cha nne siyo siyo shule maalumu. Ndio maana unaona inawika katika matokeo ya kidato cha sita,” anasema.
Wadau wanavyozizungumzia shule za kata
Mhadhiri Mwandimizi wa Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Duce), Dk Joviter Katabalo anasema ni bahati mbaya zinaitwa shule za kata na kwamba baadhi ya Watanzania walilibeza neno ‘kata’.
“Shule hizi hazina tofauti na shule nyingine, tumeshuhudia zikifanya vizuri kwenye mitihani mbalimbali tofauti zile zisizo
INAENDELEA UK 20
INATOKA UK 13
za kata zikiwemo za binafsi. Kuendelea kulitumia neno ‘kata’ kwangu naona ni bahati mbaya.
Dk Katabalo anasema shule hizo zimesaidia Taifa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopata elimu ya sekondari, kwa sababu hazina masharti ya malazi na kwamba huduma imefika hadi kwenye makazi ya wanafunzi.
Kwa mujibu wa Dk Katabalo, changamoto katika shule za kata ni pamoja uhaba wa walimu katika masomo yote, vifaa ya kujifunzia na kufundishia
‘’Changamoto nyingine ni shule hizo kutokuwa na miundombinu inayojitosheleza na rafiki ikiwamo nyumba za walimu, umeme, maji, lakini zikitatuliwa hizi ni shule kama shule nyingine,” anasema Dk Katabalo.
Kwa upande wake, Catherine Sekwao anasema kuwa shule hizo zimekuwa mkombozi kwa idadi lakini siyo kwa ubora, huku akitaka wanafunzi wanaoingia sekondari wanolewe vilivyo upande wa lugha.
‘’ Bado napigania kuwapo kwa utaratibu mzuri wa kuhama kwa lugha ya kufundishia. Lugha ya kufundishia kutoka Kiswahili shule za msingi kwenda Kiingeza kwa sekondari inawafanya wanafunzi kutoka shule za Serikali kutofanya vizuri kutokana na kuchelewa kumudu lugha. Hawawezi kushindana kwa usawa na wale wanaotoka shule za msingi za kimataifa na inajenga matabaka katika jami,”anasema
Sekwao anapendekeza lugha ya lugha ya Kiingereza iimarishwe kwa walimu ili kuanzia darasa la tano iwe ya kufundishia kwa shule zote za Serikali na binafsi.
Mbinu za kusaidia shule za kata kufanya vizuri
Mdau wa elimu, Alistidia Kamugisha anasema ili shule hizo zizidi kufanya vizuri kitaalamu ni vyema miundombinu mbalimbali ya shule ikiwamo mabweni ikaboreshwa kwa kuwa na mkakati wa makusudi kama inayofanyika kwenye maabara na madawati.
“Pia zile shule zinazofanya vizuri zitambuliwe na kupongezwa ili kuwapa morali na nyingine ziweze kujifunza kwao,” anasema.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Watoaji Elimu Wasiotegemea Serikali Kusini mwa Jangwa la Sahara (Ciepssa), Benjamin Nkonya ana mawazo tofauti kwa kusema li shule hizo zifanye vizuri kitaaluma lazima zifuate sheria na mfumo wa Serikali ikiwamo walimu kuhudhuria vipindi kwa wakati kama inavyofanyika katika shule nyingine zikiwamo za Serikali.
“Jambo jingine wazazi wasikariri elimu ya madarasa na vidato pekee yake, bali hata kwenye vyuo vya ufundi kuna elimu pia na watoto wanafanya vizuri. Tukiona kwenye elimu ya darasani hawafanyi vizuri tuwapeleka kwenye vyuo vya ufundi,” anasema Nkonya.