Prime
Ufaulu unavyokwamisha wanawake ukufunzi vyuoni
Muktasari:
- Takwimu za TCU zinaonesha kuwapo kwa ongezeko la wakufunzi katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu kutoka 8,565 mwaka 2023/2024 hadi kufikia 8,709 mwaka 2024/2025.
Dar es Salaam. Ufaulu, kusoma kila wakati na majukumu mengi, zimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazofanya wanawake wengi kutopenda kuwa wakufunzi wa vyuo.
Hayo yanasemwa na wadau mbalimbali wakati ambao takwimu za Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) zinaonyesha kuwa asilimia 69 ya wakufunzi wa ngazi mbalimbali vyuoni ni wanaume, huku asilimia 31 inayobakia ndiyo ikichukuliwa na wanawake.
Hiyo ikiwa na maana kuwa kati ya wakufunzi 8,709 waliokuwapo katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini mwaka 2024/2025, wanawake walikuwa 2,700 na 6,009 walikuwa ni wanaume.
Idadi ya wanawake waliokuwapo kwa mwaka husika ilikuwa ni ongezeko kutoka 2,693 waliokuwapo 2023/2024, huku wanaume wakiwa wameongezeka kutoka 5,963 mwaka uliotangulia.
Kwa ujumla, takwimu za TCU zinaonesha kuwapo kwa ongezeko la wakufunzi katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu kutoka 8,565 mwaka 2023/2024 hadi kufikia 8,709 mwaka 2024/2025.
Akizungumzia suala hili, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Mary Kafyome, amesema hali hiyo huweza kuwa na sababu nyingi lakini baadhi ni kukosa sifa za kufundisha chuo kikuu.
“Kwa mfano, kwa mujibu wa TCU, ili kufundisha chuo kikuu inabidi kuwa na GPA ya 3.8 kwa shahada ya kwanza ambapo unakuta wengi hawana,” amesema.
Mbali na ufaulu huo, pia kukosa utayari kwa wanawake ni sababu nyingine, huku akieleza kuwa baadhi ya anaowafahamu wameacha kazi hiyo kwa sababu ina majukumu mengi na inahitaji kusoma mara kwa mara.
“Pia sababu nyingine zinaweza kuchangiwa na masuala ya kijamii. Wanawake kama ujuavyo tuna mambo mengi ya kijamii yanayotubana kama vile familia, malezi ya watoto na hata shughuli za kijamii nyingine nyingi.
Wakati mwingine inakuwa ngumu kujigawa na kuyatimiza yote na kufanikiwa hasa pale mwanamke asipokuwa na mwenza na wanafamilia wanaompa ushirikiano,” amesema.
Mtafiti wa Elimu, Muhanyi Nkoronko, amesema hali hii huweza kuchangiwa na idadi ya wasichana wanaofaulu kutoka kidato cha sita kwenda vyuoni kuwa ndogo.
Hali hii inafanya hata walioingia vyuoni kuwa wachache, hali ambayo tayari imeweka pengo, na huko vyuoni wavulana wanaonekana kufanya vizuri zaidi kuliko wasichana.
“Kutokufanya vizuri vyuoni kumefanya kuwapo kwa idadi ndogo ya wanawake wanaoweza kupata nafasi ya kufundisha vyuoni kutokana na kushindwa kufikia kiwango cha ufaulu kinachotakiwa,” amesema.
Pia amesema kumekuwa na dhana potofu ya kuwa mwanamke hawezi kufundisha vyuoni na wanaume ndiyo wanaweza, hali inayofanya kukosekana kwa msisimko wa wanawake kuomba kazi hizo zinapotokea.
Amesema baadhi ya wanawake wamekuwa wakiona kuwa kufundisha sekondari na ngazi nyingine ndiyo hadhi zao na hudhani kuwa kufundisha vyuo inahitaji mtu mwenye ujuzi mkubwa ambao hawana.
“Hata kama ana nafasi, anaona kama hawezi kushindana. Zinahitajika jitihada za makusudi kufanya uchechemuzi kujenga fikra kuwa mtoto wa kike anaweza kufanya kazi za kufundisha vyuoni kama wanaume,” amesema.
Pia amesema juhudi zinapaswa kuwekwa kwa watoto wa kike kuhakikisha wanajifunza na wanaelewa masomo yao vyema katika hatua za awali ili wafikie fursa hizo.
“Pia kuweka mazingira sawa katika upatikanaji wa hizi kazi, hili limefanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa kwani sasa mazingira haya yameboreshwa kisheria, kisera na kimuundo na inawapa watu wote nafasi sawa na wanawake wanahamasishwa zaidi kuomba,” amesema Nkoronko.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Jimson Sanga, amesema kwa sababu wanazuoni wanashughulika na akili ya mtu, ni vyema kumjenga mwanamke tangu shule ya awali, msingi, sekondari hadi vyuo vikuu ili wawe na uwezo wa kuchagua wanachotaka kufanya.
“Tuanze kuhakikisha kuwa wanaokwenda kufundisha kuanzia darasa la awali hadi vyuo wawe waliofaulu zaidi katika ngazi zote ili inapofika wakati wa kupanga nani anakwenda wapi iwe rahisi na walimu wawe wanaolipwa vizuri zaidi,” amesema Sanga.
Pamoja na hayo, Sanga amesema kwa wakufunzi waliopo, pamoja na uchache wao, wanafanya vizuri, wanaobanana na ushindani, wanasoma ili wawe sawa.
Hata hivyo, hili linaloonekana halitofautiani na kile kilichopo katika nchi nyingine kwani kwa asili mwanamke ana kazi nyingi, hivyo kupewa uhuru wa kuchagua kazi ni kipaumbele duniani kote.
“Kwa ulimwengu mzima labda Finland ndiyo nchi pekee ambayo wanawake wamewezeshwa kufanya kila kitu, lakini kwingine duniani kote viwango vinatofautiana kwa kiasi kikubwa hivyo,” amesema.
Alitumia nafasi hiyo kupongeza uelekeo uliopo nchini kwa sababu sehemu mbalimbali sasa ukandamizaji wa wanawake umetokomezwa na hata kauli za kukatisha tamaa hazipo.
Hali hiyo imefanya sasa kama nchi kuondoka kwenye ajenda ya kumtetea mwanamke na kwenda katika kumthamini mwanamke na kumuona kuwa sawa na mwanaume, hali inayofanya na wao waonyeshe kuwa wanaridhika na hali iliyopo na hawanyanyaswi.
“Ni wajibu wa nchi kutafakari upya katika ajira, wajengewe uwezo wanawake kujitambua kuwa wanauwezo sawa na wanaume. Ni wajibu wa kila mmoja kupiga kelele kusema kuwa mwanadamu ni mwanadamu na anaweza kila kitu,” amesema.