Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tuzingatie mambo haya mabadiliko ya mfumo wa elimu

Kama kuna jambo linaloweza kuleta matumaini kwa siku za baadaye ni kuanzishwa kwa mfumo wa elimu nchini, ambao unakonga nyoyo za walio wengi.

Mfumo huo unatokana na mabadiliko ya kielimu yanayolenga kumkomboa mtoto wa Kitanzania anayeitazama elimu kama nyenzo ya kumuwezesha kupambana na fursa za soko la ajira duniani.

Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, Serikali imeanzisha mtalaa wa amali kwa shule za sekondari na ufundishaji wa lugha ya Kiingereza kuanzia darasa la kwanza. Alisema hayo yote ni katika kuboresha mfumo wa elimu ili uendane na mahitaji ya sasa.

Mabadiliko haya yamezua mjadala mkubwa, huku wengi wakiona kama ni hatua muhimu ya kuwaandaa wanafunzi kuwa na ujuzi wa kushindana katika mazingira ya kiuchumi duniani.

Abdul Mutashobya, mchambuzi kutoka Chuo Kikuu cha Jimbo la Michigan, anaandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa Linkeldin, kwamba mageuzi haya yanaweza kuwa daraja muhimu kati ya elimu na ajira.

Anasema kwa kuingiza mafunzo ya ufundi, ambayo huku nyuma hayakuwa yakipewa uzito mkubwa katika mfumo wa elimu nchini, sasa wanafunzi wanaweza kupata ujuzi wa moja kwa moja unaoendana na mahitaji ya viwanda vya ndani.

Hata hivyo, licha ya kuwa wazo la mafunzo ya ufundi si jipya, utekelezaji wake mara nyingi umekuwa ukikwama kutokana na uhaba wa rasilimali na ukosefu wa uratibu.


Elimu ya mtalaa, kifanyike hiki

Mhadhiri wa masuala ya mitalaa na ufundishaji Dk Joviter Katabaro anasisitiza kuwa ili mafunzo ya ufundi yawe na matokeo chanya, lazima yaendane na mahitaji maalum ya kijiografia.

Kwa mfano, maeneo kama Shinyanga yanayojikita kwenye kilimo yanaweza kunufaika na programu za kufundisha mbinu za kisasa za kilimo; wakati maeneo kama Dar es Salaam yenye sekta ya viwanda inayokua, yanaweza kuzingatia ujuzi wa viwanda vidogo.

Godson Makoye, mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Pamba mkoani Mwanza, anaunga mkono mawazo haya akibainisha kuwa mkakati huo unaweza kuwasaidia wanafunzi kupata ajira katika sekta kama vile usindikaji wa mazao ya kilimo.

Mbinu hii ya kijamii inalenga kuhakikisha mafunzo ya ufundi yanahusiana moja kwa moja na mahitaji ya kiuchumi ya maeneo husika, na hivyo kuwa na athari endelevu kwa jamii.

Aidha, wanazuoni kama Ishumi Abel G.M. na William A.L. Anangisye, katika kitabu chao Elimu Nchini Tanzania: Muktadha wa Kihistoria, Muundo na Changamoto, wanaeleza kuwa mafanikio ya mageuzi haya, yatategemea ushirikiano wake na mahitaji ya jamii.

Bila uhusiano wa moja kwa moja kati ya mafunzo yanayotolewa na sekta zinazoendesha uchumi wa eneo husika, juhudi hizi zinaweza kukosa matokeo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Profesa Justinian Galabawa anaonya kuwa mageuzi yanayokosa uwekezaji mkubwa, mara nyingi hubaki kuwa ishara badala ya kuwa kichocheo cha mabadiliko halisi.

Anasema ni muhimu viongozi katika ngazi zote za mfumo wa elimu kushirikishwa katika kuendesha na kudumisha mabadiliko hayo

‘’Uongozi unaoweza kubadilika ni muhimu kuhakikisha kwamba mageuzi yanajibu changamoto zinazoibuka,’’ anaeleza.

Anasema maofisa elimu wa wilaya wanapaswa kuzingatia uwajibikaji na ushirikiano, kwa kuunda mifumo inayosaidia maendeleo endelevu. ‘’Maofisa elimu wa wilaya wanapaswa kutilia mkazo uwajibikaji na ushirikiano, wakitengeneza mifumo inayosaidia maboresho ya kudumu,’’ anasema.

Anasema kwa kukuza utamaduni wa uongozi unaoweza kubadilika, Tanzania inaweza kujenga uimara ndani ya mfumo wake wa elimu, ukihakikisha kwamba mageuzi haya sio tu yanatekelezwa bali pia yanadumu kwa muda mrefu.




Ufundishaji Kiingereza



Sehemu nyingine muhimu ya mageuzi haya ni kuanza kufundisha kwa Kiingereza kuanzia darasa la kwanza.

Kwa historia, ukosefu wa ujuzi wa lugha ya Kiingereza umekuwa kikwazo kikubwa kwa wanafunzi, hasa wa maeneo ya vijijini.

Kwa kuwa Kiingereza ni lugha ya kufundishia katika ngazi za sekondari na vyuo vikuu, ni muhimu ikaanzwa kujengewaa msingi imara

Mutashobya, akichota maarifa kutoka mifumo ya elimu ya Asia, anasema kuwa kufundisha Kiingereza mapema ni hatua muhimu ya kujenga ufasaha na kujiamini miongoni mwa wanafunzi.

Mutashobya anasema hatua ya ufundishaji wa Kiingereza katika ngazi za chini, ni mpango unaoweza kuanza kwa maeneo machache ili kupima uwezo wa walimu na upatikanaji wa rasilimali kabla ya kusambaa nchi nzima.

Anatoa mfano wa Korea Kusini ambapo ushirikiano na taasisi za kimataifa katika mafunzo ya walimu kwa kutumia mbinu za kisasa, umeonekana kuwa na mafanikio.

Hata hivyo, mwalimu Nuru Japhet wa Shule ya Sekondari Chamaguha mkoani Shinyanga anaonya kuwa mafanikio ya umahiri wa lugha hiyo, yatategemea sana mafunzo ya kutosha kwa walimu na mbinu za kisasa za ufundishaji.

Mafunzo ya walimu yameonekana kuwa nguzo muhimu ya mageuzi endelevu. Stedius Kazinduki kutoka Chuo cha Ualimu Katoke anapendekeza programu za ushauri zinazowaunganisha walimu wenye uzoefu na wenzao katika maeneo yasiyo na rasilimali za kutosha.

Mitandao ya aina hii inaweza kuongeza athari za mageuzi kwa kukuza ushirikiano wa maarifa na maendeleo endelevu ya kitaaluma.

Vifaa vya teknolojia, kama majukwaa ya kidijitali yanayofanya kazi nje ya mtandao na masomo ya redio, vinaweza pia kuziba pengo la rasilimali katika shule za vijijini.