Tanzania mwenyeji mkutano wa kimataifa wa elimu mtandao

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu kongamano la 18 la kimataifa la e-learning Afrika litakalofanyika Mei 7 hadi 9, 2025 Jijini Dar es salaam, leo Machi 29, 2025. Picha na Rachel Chibwete
Muktasari:
- Kongamano la kimataifa la 18 la e-learning Afrika kufanyika nchini Mei 7 hadi 9, 2025 ikiwa ni mara ya pili kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa kongamano hilo.
Dodoma. Tanzania imetaja fursa itakazonufaika nazo kwa kuwa mwenyeji wa kongamano la 18 la kimataifa la e-learning Afrika ikiwemo mbinu mpya za kuongeza matumizi ya teknolojia za kidigitali katika elimu na sekta nyingine.
Fursa nyingine ni kuvutia programu za pamoja za biashara za wabunifu na teknolojia zinazoibuliwa nchini na kuvutia kampuni ya kiteknolojia ya kikanda na kimataifa kuja kuwekeza hapa nchini.
Pia, kuimarisha ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi katika maendeleo na matumizi ya teknolojia za kidigitali pamoja na kuchagiza uchumi wa ndani kupitia bidhaa na huduma zitakazotolewa kwa washiriki wa kongamano hilo na kuhamasisha washiriki kutembelea vivutio vilivyopo nchini.
Hayo yamebainishwa leo Jumamosi Machi 29, 2025 jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano la 18 la kimataifa la e-learning Afrika litakalofanyika Mei 7 hadi 9, 2025 jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo lenye kaulimbiu isemayo “Kufikiria upya elimu na maendeleo ya rasilimali watu kwa ustawi wa Afrika”, linafanyika kwa mara ya pili nchini ambapo kwa mara ya kwanza lilifanyika mwaka 2011, likiwakutanisha washiriki zaidi ya 1,500 kutoka nchi 65 za Afrika.
Ametoa rai kwa wizara, taasisi, mashirika, asasi, kampuni za teknolojia, wanataaluma, watafiti, wabunifu, waandishi wa habari, wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla kujiandaa kutumia fursa za kongamano hilo vilivyo.
“Elimu duniani inabadilika kwa kasi sana kwa sababu ya teknolojia na kuna mambo mengi ya kujifunza kuhusu teknolojia kwa mfano kama mmefuatilia kwenye mitandao kumekuwa na msukumo mkubwa sana wa kutumia teknolojia kwa ajili ya kufundisha kuanzia elimu ya awali kwenda juu,” amesema Profesa Mkenda.
Ameongeza kuwa: “Halafu kuna nchi zinaanza kufanya tathmini ya faida za kutumia teknolojia kwenye elimu ya msingi na elimu ya awali kwa hiyo kuna sehemu za kubadilishana mawazo vizuri.”
Amesema nchini Sweden wanaangalia kama mtoto anapoanza darasa la kwanza mpaka kumaliza elimu ya msingi kama kuna sababu ya kutumia teknolojia kwa wingi au aendelee kutumia kalamu na karatasi na ubao na chaki.
“Kwa hiyo, tutabalishana mawazo. Lakini kwa ujumla wake tunataka kuangalia suala la teknolojia katika ngazi zote hasa katika kufundisha na inasaidia sana kutumia rasilimali zilizopo za ufundishaji kwa ufanisi Zaidi,” amesema.
Amesema kongamano hilo kwa sehemu kubwa linalenga kuyaleta pamoja makundi ya wadau kutoka katika nchi 65 kujadili, kubadilishana uzoefu kuhamasisha uwekezaji na kuazimia mipango ya pamoja ya kuchagiza matumizi ya teknolojia ya kidigitali hususani katika sekta ya elimu barani Afrika.
Makundi hayo ya wadau yatahusisha watunga sera, watoa maamuzi, watalaamu wa elimu, watalaamu wa teknolojia watafiti, wabunifu wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wa maendeleo.
Amesema pamoja na matukio mengine kongamano hilo litajumuisha mkutano wa mawaziri zaidi ya 50 kutoka nchi 49 barani Afrika mkutano huo utatoa fursa ya kujadili na kuazimia mikakati ya pamoja ya kuandaa nguvu kazi mahiri katika kubuni, kuzalisha na kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidigitali.
“Teknolojia inakwenda kwa kasi haitusubiri hivyo na sisi twende nayo kwa haraka na kujifunza na kuitumia kwa manufaa, ama tusubiri halafu tukisubiri madhara yake ni kuwa tutakuwa tunapelekeshwa, tunapenda kuwa mstari wa mbele kwenye matumizi ya teknolojia,” amesema Profesa Mkenda.
Tangu kuasisiwa kwake mwaka 2005, kongamano hili limeshafanyika katika nchi 17 ikiwemo Tanzania ambapo ilifanyika mwaka 2011, hivyo mwaka 2025 litakuwa linafanyika kwa mara ya pili hapa nchini.