Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mapito ya wenye mahitaji maalumu kutafuta elimu-1

Muktasari:

  • Licha ya uwepo wa sera, utekelezaji wa elimu jumuishi umekuwa wa kusuasua kutokana na ukosefu wa rasilimali muhimu, zikiwamo vifaa saidizi, walimu wa kutosha na mazingira wezeshi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu

Dar es Salaam. Ni mazoea ya kila asubuhi watoto wengi huamka kuelekea shuleni pasipo kufikiria changamoto zinazoweza kuwazuia kufika darasani.

Lakini kwa Ashinilat na Siwajibu, safari yao ya kupata elimu ni mapambano ya kila uchao yakihusisha usafiri, mazingira yasiyo rafiki na ukosefu wa vifaa muhimu vya kuwasaidia kuishi na kujifunza kwa uhuru.

Wawili hao, wanafunzi wa Shule ya Msingi Nianjema, iliyopo wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani wanaishi na ulemavu wa viungo uliosababisha miguu yao kujikunja hivyo kushindwa kutembea au kujisogeza pasipo msaada.

Wakiwa darasani hukaa kwenye viti maalumu muda wote wa masomo wakitegemea msaada wa watu wengine katika shughuli nyingi za kila siku.

Mary Gervas, mwalimu wao wa darasa huwatazama wakipambana na changamoto hiyo, huku akijitahidi kuhakikisha hawakosi haki yao ya kupata elimu bora.

Gervas anasema safari ya Ashinilat shuleni huanza kwa kupanda pikipiki maarufu bodaboda.

“Anapofika shuleni dereva humbeba na kumuingiza darasani. Bila msaada huo angekuwa anapata ugumu wa kuhudhuria masomo,” anasimulia Gervas.

Kwa Siwajibu hali ni ngumu zaidi kwani hutegemea baiskeli ya baba yake kufika shuleni. Chombo hicho cha usafiri pia ndicho tegemeo la familia kwa shughuli nyingine za kila siku.

Siku ambazo baiskeli hutumika kwa mambo mengine ya kifamilia, Siwajibu hubaki nyumbani hivyo hukosa masomo. Pia, kuna wakati hushindwa kufanya mitihani licha ya kuwa anaishi umbali wa kilometa moja kutoka shule ilipo.

Umaskini na ukosefu wa vifaa saidizi vya kumwezesha kujisogeza vinafanya umbali huo mfupi kuonekana mrefu.

Ndani ya shule changamoto haziishii darasani. Hata kwenda chooni ni safari nyingine inayohitaji msaada wa watu wengine.

Kutokana na kutokuwa na vitimwendo, Ashinilat na Siwajibu hubebwa mgongoni na wanafunzi wenzao wa kike wanapokwenda na kurudi kutoka chooni.

Hali hii huwaondolea uhuru wa kufanya mambo yao binafsi na wakati huohuo kuwaongezea mzigo wanafunzi wenzao wanaojitolea kuwasaidia.

“Laiti wangekuwa na vifaa saidizi wangeweza kujihudumia kwa kiwango kikubwa zaidi na kupunguza utegemezi kwa wengine,” anasema Gervas.

Licha ya changamoto zilizopo, mwalimu Gervas hajakata tamaa. Mara nyingi hubaki shuleni hadi saa 10:00 au 10:30 jioni akisubiri watu wanaokuja kuwachukua wanafunzi hao baada ya masomo kumalizika.

Hofu yake kubwa kwa sasa ni maendeleo ya kitaaluma ya Siwajibu ambaye changamoto za usafiri zimeanza kuathiri uwezo wake wa kujifunza.

Mbali ya wawili hao, Jafari Mwinyi, licha ya kuwa na umri wa miaka 11 na shauku ya kusoma, hajawahi kukanyaga darasani kutokana na ulemavu wa akili na viungo.

Licha ya kupimwa na kufanyiwa tathimini ya ulemavu wake kisha kusajiliwa katika Shule ya Msingi Kapolo, iliyopo Ifakara mkoani Morogoro, Mwinyi hajawahi kwenda shule kutokana na hali aliyonayo, ukosefu wa vifaa saidizi na umbali wa ilipo shule.

Mwinyi anayeishi na bibi yake, Janeth Kajiri katika Kijiji cha Kapolo hutazama watoto wenzake wakipita jirani na nyumbani kwao wakiwa wamevaa sare za shule na mabegi mgongoni wakielekea darasani.

Akizungumza na Mwananchi, bibi Kajiri anasema mara nyingi mjukuu wake huuliza ni lini atakwenda shule kama ilivyo kwa watoto wengine.

“Kama unavyomuona hali yake, hawezi kwenda shuleni mwenyewe na shule aliyosajiliwa kwenda ipo umbali wa kilometa nne. Kusema utambeba umpeleke na kumrudisha kila siku haiwezekani,” anasema.

Kwa Mwinyi haki ya elimu ambayo watoto wengi huipata kwake imegeuka kuwa ndoto inayosubiri kutimia siku atakayopata kitimwendo.


Utekelezaji elimu jumuishi

Simulizi za Ashinilat, Siwajibu na Mwinyi ni taswira ya changamoto zinazokabili utekelezaji wa elimu jumuishi nchini Tanzania.

Licha ya jitihada za Serikali kuendeleza elimu jumuishi, shule nyingi za msingi bado zinakabiliwa na changamoto zinazozuia watoto wenye mahitaji maalumu kujifunza kwa heshima na usawa kama wengine.

Tanzania ilianza rasmi utekelezaji wa elimu jumuishi mwaka 1998 kupitia mradi wa majaribio uliotekelezwa na Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Shirika la Kimatafa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) katika baadhi ya shule za Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanasoma pamoja na wenzao katika madarasa ya kawaida.

Hatua hiyo iliimarishwa kupitia Sera ya Taifa ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004. Hata hivyo, utekelezaji wake umekuwa ukisuasua kutokana na ukosefu wa rasilimali muhimu, zikiwamo vifaa saidizi, walimu wa kutosha na mazingira wezeshi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Hali hiyo ya upungufu wa vifaa saidizi haipo tu kwenye madarasa ya kawaida bali pia kwenye madarasa yaliyo chini ya vitengo maalumu kwa ajili ya kuwahudumia watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali.

Suzan Nkya, mkuu wa kitengo cha elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Nianjema, iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani anasema changamoto kubwa ni upungufu wa vifaatiba vinavyohitajika kwa wanafunzi hao, hususani wenye ulemavu wa viungo wanaohitaji mazoezi tiba ambayo kwa sasa hayapatikani shuleni hapo.

“Ingawa kuna baadhi ya vifaa kwa ajili ya ulemavu wa akili, vifaa vya kusaidia mazoezi tiba ni changamoto kubwa,” anasema.

Anaeleza changamoto hiyo inaathiri moja kwa moja utekelezaji wa elimu jumuishi, kwani baadhi ya wanafunzi hulazimika kukaa chini kwa muda mrefu kutokana na ukosefu wa viti maalumu vya kukalia.

Anasema idadi ya viti ni ndogo na walimu hawawezi kuwashikilia watoto hao kwa muda wote wa masomo hali inayowalazimu kutumia zulia kama mbadala.

“Hii ni kwa sababu viti ni vichache na mwalimu hawezi kumshikilia mtoto kwa saa zote. Tunatumia zulia zaidi kwa sababu viti vya kawaida si salama kwa wanafunzi hawa, wanaweza kudondoka au kusukumwa na wenzao,” anasema.

Mwalimu Nkya anasema changamoto hizo zimewakatisha tamaa baadhi ya wazazi na kusababisha wengine kuacha kuwapeleka watoto wao shuleni wakidai hawaoni mabadiliko yao.

“Kutokana na mazingira haya kutokuwa rafiki, wazazi wasio wavumilivu wanakata tamaa na kuacha kuwaleta watoto wao shuleni kwa kuona kuwa hakuna mabadiliko ya mtoto anapokuwa shuleni. Ukweli ni kwamba, watoto hawa wanahitaji muda kujifunza siyo kitu cha matokeo ya haraka,” anasema.

Hali kama hiyo imedhihirika katika Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro ambako Mwananchi imetembelea shule za msingi za Lipangalala na Ifakara na kubaini watoto wenye mahitaji maalumu wanakabiliwa na changamoto lukuki zinazosababisha baadhi yao kuwa nje ya mfumo wa elimu.

Ofisa Elimu Ifakara, Ester Kilima anakiri licha ya jitihada mbalimbali kufanyika kuhakikisha utekelezaji wa elimu jumuishi kwenye halmashauri hiyo, bado kuna changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi ili watoto wenye mahitaji maalumu wapate elimu.

Kwake changamoto ni upungufu wa walimu, vifaa saidizi na uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto hao, mambo yanayosababisha baadhi ya watoto wenye mahitaji maalumu kuwa nje ya mfumo wa elimu licha ya ubainishaji kufanyika.


Utafiti ulichobaini

Tafiti zinaonesha mafanikio ya elimu jumuishi yanategemea upatikanaji wa vifaa saidizi, lakini hali halisi shuleni inaonyesha uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinavyokidhi mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu.

Upungufu wa vifaa pia ulionekana mkoani Dodoma katika utafiti uliofanywa na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU) kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro uliolenga kuangalia upatikanaji wa miundombinu na vifaa vya kujifunzia katika utekelezaji wa elimu jumuishi kwenye shule za msingi za umma Mkoa wa Dodoma.

Utafiti huu uliochapishwa mwaka 2023 kwenye Jarida la Kimataifa la Utafiti na Ubunifu katika Sayansi za Jamii (IJRISS) unaonesha asilimia 95 ya walimu waliohojiwa wameripoti kuwa vitabu vya nuktanundu (braille) havitoshi jambo linalofanya wanafunzi wasioona kupata tabu kubwa katika kujifunza.

Vilevile, vifaa vya kusaidia kusikia na vyumba maalumu vya kupima usikivu vimepungua kwa asilimia 96 hali inayozuia walimu kufanya tathimini sahihi ya mahitaji ya wanafunzi wenye uziwi.


Kauli ya Serikali

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Elimu Maalumu Wizara ya Elimu, Dk Magreth Matonya anasema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa kwa watoto wenye mahitaji maalumu kuhakikisha hawaachwi nyuma kwenye mfumo wa elimu.

Mbali ya hayo, anakiri bado kuna changamoto ambazo zinakwamisha jitihada hizo mojawapo ikiwa ni uwepo wa maofisa elimu maalumu wasiotekeleza majukumu yao ipasavyo.

Anasema tathmini iliyofanywa imebaini kuwa baadhi ya maofisa elimu maalumu hawajatekeleza wajibu wao kwa kiwango kinachotarajiwa, jambo ambalo Serikali imeanza kulifanyia kazi na Julai, 2026 watakutana nao ili kuwapatia miongozo na maelekezo yatokanayo na matokeo ya uchambuzi wa hali ya utekelezaji wa elimu jumuishi katika elimu ya msingi.

Kuhusu watoto kukosa vifaa saidizi, Dk Matonya anasema hilo kwa kiasi kikubwa linachangiwa na walimu wakuu na maofisa elimu maalumu kushindwa kutimiza wajibu wao akieleza Serikali imegawa vifaa vya Sh10 bilioni nchi nzima na vipo vingine vya akiba.

Itaendelea kesho kwa kuangalia hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa mkakati wa elimu jumuishi.

Sehemu ya pili kesho, itaangazia viongozi walivyo vikwazo kwa utekelekezaji wa elimu jumuishi.