Prime
Zijue faida za katuni kwa watoto

Muktasari:
- Wataalamu wa saikolojia wamethibitisha kuwa kutazama katuni kuna mchango wa asilimia 50 kwenye maendeleo ya akili ya mtoto, hususan mzazi anaposhiriki naye, husaidia akili ya mtoto kukua kwa asilimia 100.
Dodoma. Ni nadra nyumba yenye televisheni hasa katika maeneo ya mijini, kukuta watoto wadogo wakiangalia vipindi vingine tofauti na katuni.
Katuni ni picha jongefu ambazo zimetiwa sauti na matendo, ambapo zamani zilikuwa zikitumiwa kama burudani lakini kadiri muda unavyoenda, ubunifu wa watengenezaji wengi wamejikita katika kutoa elimu na burudani.
Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii na Elimu (FAHE), kutoka Chuo Kikuu cha St John cha jijini Dodoma, Dk Shadidu Ndossa anasema watoto wanaweza kupata burudani na kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo uhifadhi mazingira, ujenzi, kutambua herufi, namba, kusoma, kuandika na elimu ya anga.
Hata hivyo, anasema utengenezaji wa katuni hizo unategemea na umri wa watoto, huku akitaja umri wa kwanza ni miaka miwili hadi mitatu ambapo watoto wanaanza kujifunza kuongea.
Anasema ngazi hii katuni zake ni fupifupi, wahusika wanazungumza taratibu na kurudia ujumbe zaidi ya mara moja.
“Kuna katuni za watoto hadi wa umri wa miaka 16, ambazo sasa zinakuwa ni ndefu, zinachanganya visa vingi kwa wakati mmoja. Lakini za watoto zinakuwa ni kati ya dakika sita hadi 10 kwa sababu umakini katika ufuatiliaji kwa watoto sio wa muda mrefu na ukiweka katuni ndefu unampoteza anachotaka,”anasema.
Anasema kwa mataifa yaliyoendelea, wameweka uwekezaji mkubwa katika utengezaji wa katuni za kuburudisha na kufundishia watoto.
“Wenzetu wanajua kuwa uwekezaji mkubwa kwa watoto unahitajika katika maeneo yote si kuwekeza tu shuleni kama tunavyojua sasa hivi, watu wetu wengi wanatumia simu au televisheni," anaeleza.
Anasema wanachofanya ni kuwekeza kuhakikisha kuwa wanaweza kutoa maarifa kupitia teknolojia hiyo kwa kulingana na umri wa watoto.
Fursa muhimu
Anasema watoto wengi hivi sasa wanapenda digitali, kwa hivyo badala ya kuangalia ujinga, katuni zenye maudhui mazuri na zilizotengenezwa vizuri, zinaweza kuwavutia kama zana za kujifunzia.
"Ukiachana na ubongo kids, nadhani tunahitaji katuni nyingi ambazo zinaburudisha na kuelimisha watoto. Vyombo vya habari vinapaswa kuelewa hili ni eneo zuri na kuwekeza rasilimali kwa ajili ya kununua ama kutengeneza. Naamini vijana wa Kitanzania wako wengi katika vyombo vyetu vya habari wakiungana na kutengeneza, fursa hiyo ipo, anasema.
Anasema sasa hivi vyombo vya habari vimekuwa vikinunua maudhui ya filamu, mpira lakini vipaswa kufikiria kununua katuni ili kuleta burudani kwa watoto na jamii.
Dk Ndossa anasema kutokana na watoto kupenda katuni, chochote utakachokipeleka katika, kina uwezo mkubwa wa kutumika kufundisha watoto.
Anasema bado katika shule nyingi hakuna walimu wa kutosha, kuna baadhi ya maarifa ambayo yangeweza kufundishwa kupitia katuni.
Anasema hivi sasa duniani elimu inayotakiwa ni ile ya kumwezesha mwanafunzi kuwa na uwezo wa kufikiri kwa kina, hivyo katuni anasema zinaweza kuwa sehemu ya kumsaidia sio tu kufikiria lakini hata kuwa na uwezo wa kujifunza kwa kujisimamia.
Hata hivyo, Dk Ndossa anasema kuwa katuni haziwezi kuwa mbadala wa mwalimu japo mtoto anaweza kuangalia na kuzitumia kujifunza.
"Ni njia ya kuwajengea watoto utamaduni wa kujifundisha wenyewe. Kwa mfano, anaweza kujua Kingereza kwa njia hiyo," anasema na kuongeza:
“Kitu muhimu katika dunia tunayokwenda nayo si kila kitu ni lazima ufundishwe shuleni, tukiwajengea uwezo wa watoto kujifunza vitu mbalimbali, wakija sekondari watajikuta wanaweza kujifunza baadhi ya mambo wao wenyewe,”anasema.
Mitazamo tofauti
Dk Ndossa anasema katika utafiti wake wa jinsi katuni inavyoweza kuwasaidia watoto katika fasihi ya Kiswahili, amebaini kuwa wazazi wamegawanyika kwenye mitazamo ambapo wapo wanaosema katuni inaweza kumsaidia mtoto kujifunza na wapo ambao hawaamini katika hilo.
“Wapo wanaosema katuni ni mbaya, zinapoteza muda na watoto wanajifunza mambo ambayo si utamaduni wao, lakini wapo ambao hawajui na hawana taarifa za kutosha. Katuni ninazozungumza ambazo zinafaa kufundishia hata shuleni. ni zile ambazo zimetengenezwa na taasisi na mashirika yanayotambulika duniani,”anasema.
Anasema ukiingia katika mtandao wa yotube kuna katuni ambazo hata aliyetengeneza hajulikani na kuwa hizo unaweza kukutana na maudhui ambayo hayafai kuangaliwa na mtoto.
Anasisitiza kuwa hata kwa zile zinazofaa, lazima zitazamwe kwa kiasi, huku akisisitiza udhibiti wa wazazi katika kuzitazama katuni hizo.
“Haiwezekani mtoto anaamka asubuhi mpaka usiku anapolala yuko tu katika TV, itamletea changamoto ya macho, unene... atashindwa kuchanganyika na wenzake katika michezo kwa kuwa muda mwingi atakuwa anazitazama,” anasema.
Anasema ingawa familia nyingi zina televisheni bado watoto wengi hawapewi nafasi ya kuangalia katuni kwa sababu wazazi wanakuwa na utaratibu wa kuangalia mambo mengine yaliyo kwenye televisheni.
“Unakuta baba anashika rimoti anapeleka kwenye mpira, mama naye anataka kuangalia sinema, dada anaangalia bongo flavour. Tunawanyima watoto haki yao, lazima tuseme tuache na ikiwezekana uangalie kwa pamoja katuni ikiwa ni sehemu ya kuhakiki wanachoangalia na kisha tuwatupie maswali kuona wameelewa nini,”anasema.
Katuni shuleni
Dk Ndossa anasema kwa shuleni, katuni zinaweza kutumika kama zana za ufundishaji hasa zikiwezeshwa kwa mifumo ya kitehama.
Anashauri shule ziwezeshwe kwa kuwa na miundombinu na pia walimu wawezeshwe kwa kupatiwa mafunzo, ili wachanganye maarifa ya kawaida wanayofundisha na katuni hizo.
Wasemavyo wadau wengine
Mwenyekiti wa vituo vya kulelea watoto wadogo mkoani Dodoma, Rehema Mdengede, anasema katuni zina umuhimu ikiwa zitawekwa maudhui yanayomwezesha mtoto kujifunza.
"Sisi walimu kuna muda lazima tutumie sauti za wanyama, vitu na mavazi Ili kuvuta hisia za watoto,”anasema.
Rehema ambaye pia ni mwalimu wa Shule ya Kulelea Watoto wa Wadogo na Elimu ya Awali ya Tehillah, anasema wanachofanya ni kuweka namba na herufi kwenye katuni ambazo wanazitumia katika kufundishia watoto wadogo.
“Katuni zinawasaidia katika kusoma yaani wanaelewa kwa haraka, yeye atakuwa anaipenda katuni na hapo hapo anajifunza. Lakini katuni zinazofaa kufundishia isiwe ni zile za kuchekesha pekee au wanyama kurukaruka.Muhimu mtoto anajifunza nini?" anaeleza.
Naye mzazi, Emma Mshumbuzi anasema wazazi wanatakiwa kuwa na usimamizi wa karibu, kwa kuwa zinaweza kumharibu mtoto.
“Changamoto ipo katika maudhui ya katuni, kuna maudhui mengine yanaweza kumjenga ama kumpotosha mtoto. Hapo mzazi awe makini na maudhui wanayoangalia. Sasa hivi watoto wanajua kucheza na teknolojia kuliko hata watu wazima na hili tunaliona kupitia simu zetu,” anasema.
Anasema kitu cha kwanza mtoto akipata simu ni kwenda kupakua katuni katika mitandao na huko anakutana na maudhui ya kila namna.
Anashauri Watanzania wengi kujitokeza katika kutengeneza maudhui ambayo yanaendana na mila na desturi zao.
Kuhusu katuni
Wataalamu wa saikolojia wamethibitisha kuwa kutazama katuni kuna mchango mkubwa kwa asilimia 50 kwenye maendeleo ya akili ya mtoto, hususan pale ambapo mzazi atashiriki naye husaidia akili ya mtoto kukua kwa asilimia 100.
Mzazi anapaswa kufanya yafuatayo; Kuchunguza wahusika anaowapenda zaidi. Hii itakupa ishara ya mapema kuwa mtoto wako anavutiwa zaidi kuwa nani au mtu wa aina gani atakapokuwa mkubwa.
Chunguza kama kuna sauti za wahusika wa katuni anazozipenda kuziiga. Ukiona anaiga na anaziwezea basi tambua kuwa mtoto wako anaweza kuja kuwa muigiza sauti mkubwa.
Fahamu kuwa sauti unazozisikia kwenye ckatuni ni za binadamu wa kawaida na wanalipwa fedha nyingi sana kwa kazi hiyo.
Kisha baada ya kumaliza kutazama, kaa naye na mjadili kuhusu katuni mliyoangalia. Unaweza kumuuliza maswali kupima kumbukumbu na jinsi alivyoielewa hiyo katuni. Hapa utakuwa unamjengea mtoto wako vitu viwili; Kwanza, uwezo wa kujieleza na pili utamjengea tabia ya kuzingatia mambo kwavile anajua kuna maswali utamuuliza akimaliza kuangalia.
Hiyo tabia atakuwa nayo mpaka shuleni atakuwa ni mtu wa kuzingatia mambo kwakuwa kuna maswali anajua ataulizwa.
Pia msaidie mtoto wako kuchimbua kuhusu mambo mapya aliyoyaona kwenye katuni. Soma naye vitabu au maelezo mtandaoni yanayohusu kitu alichokiona. Hii itamjenga, kila siku akitazama katuni atatoka na kitu kimoja ambacho atakwenda kukidadisi zaidi ili akielewe, hivyo utajikuta mtoto wako anajua mambo mengi sana kwa muda mchache.
Ukiyafanya haya, akili ya mtoto wako itakuwa vizuri na kiwango chake cha ubunifu kitakuwa juu kuliko watoto wengine.