Elimu nyumbani wajibu uliosahaulika na wazazi wengi

Muktasari:
- Hii ni aina ya elimu ambapo watoto hufundishwa nyumbani badala ya kwenda shule za kawaida za umma au binafsi.
- Mara nyingi, wazazi, walezi, au walimu wa binafsi huongoza masomo hayo, na yanaweza kufuata mtalaa rasmi au kuwa huru zaidi kulingana na mahitaji na maslahi ya mtoto.
Dar es Salaam. Jua la asubuhi linaangaza kupitia dirisha la jikoni, huku Anita Msita mwenye umri wa miaka minane akipaka siagi ya karanga kwenye mkate.
Sebuleni, kaka yake Sam Msita ameketi kwenye si
sofa akisoma kitabu kuhusu viumbe wa baharini.
Aghalabu hivi ndivyo ilivyo katika nyumba hii ya familia ya Msita Semu. Huyu akisoma hiki yule anafanya kwa vitendo kile. Kwa watoto hawa, nyumbani hapa ni sawa na shule ya pili kwao.
“Niliwahi kufikiria kwamba shule lazima iwe darasani, kwenye dawati na ubao mweupe,” anasema mkewe, Rachel Thompson, huku akipanga mipango ya masomo mezani na kuongeza: “Lakini sasa najua kwamba kujifunza kunaweza kufanyika popote – hata ukiwa umevaa pajama huku ukiwa unakula keki.”
Inawezekana
Kama ilivyo kwa baadhi ya wazazi, Rachel na mumewe Semu walianza kusomesha watoto nyumbani wakati wa janga la Uviko- 19 lilipoikumba dunia. Mwanzoni ilikuwa kazi ngumu, lakini kadri wiki zilivyopita, waligundua jambo la kushangaza – watoto wao walikuwa wanaendelea vyema kimasomo.
“Tuliona wanakuwa na hamu ya kujifunza, wanajiamini zaidi,” anasema Rachel. Anaongeza' “Hawakusoma kwa kukariri tu – walikuwa wanajifunza kweli kweli”
Baada ya shule kufunguliwa tena, familia ya Semu ilichukua uamuzi wa kishujaa, mbali ya kuwarudisha shule, wazazi waliendelea na utaratibu wao wa kuwasomesha nyumbani.
Wanajifunzaje?
Siku zao zimepangwa lakini zina urahisi. Asubuhi wanajifunza kusoma, kuandika, na hesabu. Alasiri wanajihusisha na masomo ya vitendo – majaribio ya sayansi nyuma ya nyumba pamoja na kupitia mitandao.
Watoto wanahusika kupanga ratiba zao, kuchagua mada wanazopenda na kuweka malengo ya kila wiki.
Mtindo huu wa kujifunza umesaidia Anita, ambaye alikuwa na wasiwasi wa kurejea shuleni akiwa mwenye furaha. Darasani watoto hawa ni moto wa kuotea mbali, wanaonekana kujua hata zaidi ya kile wanachofundisha walimu wao.
Hata hivyo, usomeshaji huu wa nyumbani haukosi changamoto. Rachel anakiri kwamba kuna siku anajihisi asiyejiamini.
“Mimi si mwalimu wa taaluma, ni mzazi tu ninayejitambua. Huwa najihisi, je, nafanya vya kutosha kwa haya ninayowafundisha? Wanakosa nini kwa upande wa kijamii maana muda mwingi sitaki wachangamane na watoto majirani hasa wale watukutu?” anasema.
Familia ya mafunzo
Familia ya Semu ni kielelezo cha uwajibikaji wa wazazi katika kuwaandaa watoto kielimu. Hata hivyo, ni wazazi wangapi wanaotekeleza wajibu huu ili kudhibiti elimu ya watoto wao?
Kwa wazazi waliobahatika, hufanya hivyo kwa sababu za kitaaluma, wengine kwa usalama, maadili, au kutaka kutumia muda mwingi pamoja kama familia.
Wataalamu wa elimu wanasema maana ya “shule” inabadilika. Kujifunza kwa njia mseto, madarasa ya mtandaoni, na mifumo ya nyumbani vinazidi kukubalika.
Inawezekana kile wanachokikosa shule wakakipata nyumbani.
"Chukulia mfano, leo nchini hapa shule nyingi za umma hazifundishi elimu ya kompyuta kivitendo. Mtoto hadi anamaliza kidato cha sita hajui kutumia kompyuta. Hili jukumu shuleni limeshindikana, lakini linaweza kufanyiwa kazi nyumbani. Watoto wafunzwe kompyuta na teknolojia nyingine hasa wale wenye wazazi wanaojua teknolojia hizo, " anasema mdau wa elimu, Bakari Heri.
Kwa Semu na mkewe, kusoma nyumbani si hatua ya mpito tu, ni mtindo wa maisha yao pamoja na kutingwa na harakati nyingine za kutafuta mkate wa siku.
“Tumejifunza kwamba elimu haijafungwa kwenye kuta nne za shule” anasema Semu akiungwa mkono na mkewe Rachel anayesema:
“Elimu iko jikoni, bustanini, maktaba, hata sokoni. Iko kwenye maswali wanayouliza watoto kabla ya kulala."
Swali linabaki wazazi wangapi wanatekeleza wajibu huu kwa watoto wao? Shule ya kwanza huanza nyumbani.
Maana ya elimu nyumbani
Elimu nyumbani ni njia ya elimu ambapo watoto hufundishwa nyumbani badala ya kwenda shule za kawaida za umma au binafsi.
Mara nyingi, wazazi, walezi, au walimu wa binafsi huongoza masomo hayo, na yanaweza kufuata mtaaaa rasmi au kuwa huru zaidi kulingana na mahitaji na maslahi ya mtoto.
Watu huchagua elimu hii kwa sababu mbalimbali, kama vile imani za kidini au falsafa, wasiwasi kuhusu mazingira ya shule au ubora wa elimu na sababu za kiafya au nahitaji ya mtoto.