‘Darasa janja’ kuwasaidia wanafunzi, wahitimu wa sekondari Rungwe

Mwalimu wa Tehama katika Shule ya Sekondari Mpuguso, Philimon Mwakyusa akiwafundisha wanafunzi somo la Tehama.
Muktasari:
- Shule za Sekondari wilayani Rungwe zimeshauriwa kusajili somo la Tehama ili kurahisishia wanafunzi wanaohitimu elimu yao kujiajiri badala ya kutegemea ajira za Serikali na watu binafsi.
Mbeya. Shule ya sekondari Mpuguso iliyopo Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya inatarajia kufungua darasa janja “smart classroom” ambalo litamwezesha mwalimu wa somo la teknolojia kulifundisha kwa shule zote zilizopo ndani na nje ya wilaya hiyo bila kutembea.
Hatua hiyo imetajwa kuboresha elimu kwa wanafunzi kujiandaa kukabiliana na changamoto ya ajira kupitia teknolojia na kutengeneza fursa za ajira baada ya kumaliza masomo yao.
Akizungumza wakati wa kugawa kompyuta mpakato 80 katika shule nne za sekondari wilayani humo, Mratibu wa Shirika la Reneal International Education Outreach, David Nyangaka amesema uwekezaji huo unalenga kuboresha sekta ya elimu na kuunga mkono kazi ya Serikali katika sekta hiyo.
Amesema kompyuta hizo zimefungwa programu zenye vitabu vya kiada na ziada ambapo mwanafunzi atapata mafunzo bora kwenye Tehama pamoja na walimu kujifunza, akiomba vifaa hivyo kutunzwa na kutumika inavyopaswa.
“Nishauri shule zitakazopata huduma hii zisajili somo la teknolojia kama ilivyo kwa baadhi ya mikoa ikiwamo Arusha, ambapo wanafunzi wataweza kusoma tahasusi ya fizikia, kemia na Tehama, kuna wanafunzi waliohitimu kwa tahasusi za PMC (Fizikia, Hisabati na Kompyuta).

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mpuguso wakiwa darasani wakijisomea somo la kompyuta baada ya shule hiyo kukabidhiwa vifaa hivyo 20 kwa ajili ya somo Tehama.
“Lengo ni kusaidia wanafunzi kujiajiri baada ya kuhitimu elimu yao bila kutegemea kuajiriwa, pia, kuunga mkono Serikali kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza Tehama kufundishwa,” amesema Nyangaka ambaye ni Ofisa Tehama Mkuu, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Hata hivyo, ameongeza kuwa Rungwe si sehemu ya kwanza kupatiwa kompyuta hizo, bali zaidi ya halmashauri 35 katika mikoa tisa nchini, zimefikiwa na huduma hiyo ambayo inatolewa bure baada ya kukidhi vigezo.
“Vigezo ni vinne; uhakika wa umeme, chumba maalumu kwa ajili ya vifaa, shule iwe na wanafunzi wanaozidi 300 na mpango mkakati wa halmashauri yenyewe, hivyo Rungwe imekidhi,” amesema ofisa huyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jafari Haniu, Katibu Tawala Wilaya hiyo, Amimu Mwandelile amesema shule zote zinapaswa kupata vifaa hivyo ili kuweka usawa kwa wanafunzi wote, vinginevyo ni kuweka matabaka ya wanaojua na wasiojua.
Amesema Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake, akiomba wadau wengine wa elimu kushirikiana na kuunga mkono juhudi za awamu ya sita katika kuboresha sekta hiyo kwa ustawi wa nchi.
“Bado hatujachelewa, tunapaswa kila mmoja anayejua ni mdau wa elimu kuunga mkono juhudi hizi, kilichofanyika katika shule hizi kifanyike shule zote ili kusambaza maarifa na kuweka usawa kwa wanafunzi wote hapa Rungwe,” amesema Mwandelile.
Naye Mkurugenzi wa Mwaiteleke Foundation, Aliko Anyambilile ambaye ndiye alifanikisha programu hiyo, amesema ndoto yake ilikuwa ni kufikisha huduma ya teknolojia wilayani humo ili kuchagiza maarifa kwa wanafunzi.
Amesema pamoja na kufanikisha mpango huo kwa shule nne, mkakati wa taasisi hiyo ni kuzifikia shule 10 au zaidi katika wilaya hiyo kwa lengo la kuboresha elimu katika mfumo wa Tehama, akiomba wadau wengine kujitokeza kuchangia.
“Shule zilizopata kompyuta kwa sasa ni Mpuguso, Lupoto, Kinyala na Ikuti, tunaendelea kupambana kuhakikisha tunazifikia nyingine zaidi hapa wilayani na kwa kuanzia haraka tutazifikia 10 ambapo kila moja itapata kompyuta 20.
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Magreth Mkoveke amesema somo hilo linaenda kuwabadilisha kifikra na kuwaandaa kidigitali.
“Tuko tayari kujifunza na kufuata maelekezo lakini zaidi tukiiwaza kesho yetu kuhakikisha tunatengeneza fursa za kujiajiri badala ya kusubiri ajira,” amesema Magreth.
Naye mmoja wa walimu wanaofundisha somo hilo, Philimon Mwakyusa amesema wapo tayari kujifunza na kufundisha teknolojia hiyo kwa kuwa wamepatiwa mafunzo, hivyo matarajio yao ni kubadili maarifa ya wanafunzi.
“Tumekuwa wa kwanza kufikiwa na huduma hii, kwetu ni fursa ya kuwaelimisha wanafunzi kuhakikisha wanaweza kutengeneza kesho yao hata kuandaa kadi za harusi na teknolojia nyingine,” amesema Mwakyusa.