Shule Iringa zalia uhaba wa walimu wa Tehama

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyang'oro, Wilayani Iringa wakionyesha namna walivyobuni mfumo kwa ajili bili za maji kidigitali.
Muktasari:
- Wakati shule nyingi za sekondari mkoani Iringa zikiwekeza kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa kuandaa miundombinu zikiwamo kompyuta, uhaba wa walimu wenye ujuzi huo umetajwa kuwa kikwazo.
Iringa. Uhaba wa walimu wenye ujuzi wa kufundisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), umetajwa kuwa kikwazo cha wanafunzi wa shule za sekondari mkoani Iringa kujifunza teknolojia hiyo.
Karibu shule nyingi za sekondari za Mkoa wa Iringa zimeanzisha madarasa ya Tehama kutokana na uwepo wa kompyuta.
Hivi karibuni, shirika linalolenga kukuza ujuzi wa Tehama shuleni la Lyra Tanzania liligawa kompyuta 320 kwa shule kumi za sekondari 10 za Mkoa wa Iringa na kufanikiwa kuanzisha Jukwaa la Tehama Mkoa wa Iringa.
Lakini pia, Mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga, taasisi nyingine wamefanikiwa kugawa kompyuta kwenye shule za sekondari jambo lililosababisha uwepo wa madarasa ya Tehama.
Akizungumza katika maonyesho ya bunifu mbalimbali za kidijitali, Meneja wa Mradi wa Mifumo ya Kujifunza Kidijitali kutoka Shirika la Lyra, Nora Mkenda amesema uhaba wa walimu ndio kikwazo
"Changamoto kubwa ni uhaba wa walimu wa Tehama, hili ni tatizo kubwa na linaathiri wanafunzi wenye vipaji vya ubunifu kushindwa kuendeleza bunifu zao," amesema.
Baadhi ya wanafunzi walionyesha ujuzi katika bunifu mbalimbali wakitumia Tehama kufanikisha.
"Wanafunzi wameonyesha ujuzi kwa vitendo, tunategemea watakuwa wabunifu katika kutatua changamoto zao na zile zilizopo katika jamii inayowazunguka. Lengo la kuandaa maonyesho haya ni kukuza elimu kidijitali," amesema.
Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Iringa, Wilbard Yanga amesema tatizo la uhaba wa walimu wa Tehama linaweza kupunguzwa kwa njia mbili.
Amesema moja ni kuwepo kwa mafunzo ya Tehama kwa walimu ambapo kila shule itachagua mwalimu ambaye kwa kutumia wataalamu wa Tehama wa Halmashauri ya Wilaya watanolewa.
Ametaja njia nyingine kuwa ni shule hizo kutafuta walimu wa mafunzo ya vitendo kutoka vyuo vinavyotoa elimu ya Tehama.
Awali wanafunzi wabunifu kutoka Shule ya Sekondari Nyang'oro mkoani Iringa, Octavian Mapile na Naomi Nguswa walisema somo hilo linapaswa kupewa kipaumbele.
Wanafunzi hao ni miongoni mwa wabunifu waliotengeneza mfumo wa kurahisisha utoaji wa huduma ya maji na kudhibiti upotevu wa maji.
Wamesema mfumo huo unatoa huduma ya maji kidijitali ambapo mteja atalazimika kuweka sarafu ya Sh200 na kupata huduma moja kwa moja bila kuwepo kwa mtoa huduma yeyote.