Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mgogoro huu wa Tanzania, Kenya ni hasara kwa uchumi

> Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania na mwenzake wa Kenya ,Rais Uhuru Kenyatta wkionyesha mshikamano baina ya mataifa wanayoyaongoza.

Muktasari:

Wakiwa nchini Namibia kuhudhuria miaka 25 ya uhuru wa nchi hiyo na kuapishwa kwa Rais Hage Geingob, marais hao walikubaliana ‘kutengua’ masharti mapya ambayo kila nchi ilikuwa imemwekea mwenzake.

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete na mwenzake wa Kenya, Uhuru Kenyatta wamefanikiwa kuondoa sintofahamu iliyoibuka kati ya nchi hizo mbili na kutishia kuvuruga sekta ya utalii ambayo inayoingiza fedha nyingi za kigeni.

Wakiwa nchini Namibia kuhudhuria miaka 25 ya uhuru wa nchi hiyo na kuapishwa kwa Rais Hage Geingob, marais hao walikubaliana ‘kutengua’ masharti mapya ambayo kila nchi ilikuwa imemwekea mwenzake.

Masharti hayo ni Kenya kuzuia magari yenye usajili wa Tanzania kubeba au kushusha watalii katika maeneo ya vivutio vya watalii na Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Kwa upande wa Tanzania sharti lililokuwapo ni kupunguza kupunguza safari za Shirika la Ndege la Kenya (KQ) kuingia nchini, kutoka 42 hadi 14 kwa wiki.

Katika kuvunja masharti hayo, marais hao walikubaliana kufuta marufuku hizo kuanzia wiki hii ili hali irejee kama awali.

Rais Kikwete na Kenyatta wamekubaliana kwamba Aprili 29, mwaka huu wawakilishi wa wakuu hao wa nchi watakutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuyapatia ufumbuzi wa kudumu masuala hayo.

Sakata lilivyoanza

Desemba 22, mwaka jana, Kenya ilizuia magari yenye usajili wa Tanzania kupakia au kuteremsha watalii kwenye vivutio vya utalii na viwanja vya ndege nchini humo.

Baadaye mwezi huohuo, Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki, Biashara na Utalii wa Kenya, Phyllis Kandie alikutana na Waziri wa Utalii wa Tanzania, Lazaro Nyalandu na walipeana wiki tatu za kulitafutia ufumbuzi suala hilo.

Baada ya muda huo kwisha bila muafaka, Februari 6, mwaka huu, Kandie alirejesha marufuku ya awali kwa madai kuwa Tanzania imeshindwa kuchukua hatua.

“Wiki tatu zote zimekwisha bila Tanzania kuwa na mkutano wa maridhiano. Kwa hiyo tumeamua kusonga mbele kwa kutekeleza mkataba wa makubaliano wa pande zote mbili,” alisema waziri huyo.

Katika hali iliyoonekana ni kulipiza kisasi, Machi 18, mwaka huu, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TCAA) ikapunguza safari za Shirika la Ndege la Kenya kutoka 42 hadi 14 kwa wiki, ambayo ni karibu na asilimia 60. Mpango huo ulitekelezwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa kati ya shirika na Serikali ya Tanzania ambayo ni safari 14 kwa wiki. Kuongezeka hadi safari 42 ilikuwa ni kinyume na makubaliano.

Kauli ya Watanzania

Baadhi ya wachumi na wadau wa masuala ya utalii wanaonekana kufurahia uamuzi uliochukuliwa na Rais Kikwete pamoja na mwenzake, Kenyatta wa Kenya. Wanaamini busara zao zinagusa sekta nyeti ya utalii nchini.

Sekta ya utalii nchini inaongoza kwa kuingiza fedha za kigeni nchini ikifuatiwa na madini. Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mwaka jana sekta ya utalii iliingiza Dola 2 bilioni za Marekani na kuizidi madini ambayo ilikusanya Dola 1.7 bilioni.

Isitoshe, Wizara ya Utalii na Maliasili nayo inasema zaidi ya watalii milioni moja waliingia nchini mwaka 2013.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Emmanuel Mallya anasema hakuna nchi inayonufaika na migogoro, badala yake anaishauri Serikali ya Tanzania itakapokaa na wenzao wa Kenya wahakikishe wanafikia suluhisho litakalokuwa na faida kwa pande zote mbili.

Mallya anashauri pia, Tanzania iende mbali zaidi kwa kuhakikisha inaziondoa kero zinazolalamikiwa na watalii.

Anasema baadhi ya watalii wamekuwa wakilalamikia ada za kutua na ndege nchini kuwa ni kubwa mno ikilinganishwa na nchi nyingine. Hivyo, Serikali inapaswa kupitia upya bei hizo ili kuongeza mapato yatokanayo na utalii.

Mhadhiri huyo anasema ili kuimarisha sekta ya utalii na usafiri wa anga nchini, Serikali iliwezesha Shirika la Ndege la Umma kusafirisha abiria bila vikwazo.

“Tanzania tunaathirika kwa sababu hatuna shirika la ndege lenye nguvu,” anasema Mallya. Mratibu wa Sera na Bajeti kutoka Jukwaa la Wadau wa Kilimo wasio wa Serikali (Ansaf), Gilead Teri anasema Tanzania ni ya pili duniani kwa kutoza gharama kubwa za ndege kutua nchini, ikiwa nyuma ya Finland.

Hata hivyo, aliitaka Tanzania isishindane na Finland kwa kuwa yenyewe ina ndege nyingi na uwezo wa kufuata abiria wao katika nchi jirani.

Anasema kupunguzwa kwa safari za shirika la ndege la Kenya kuja nchini kuna athari kwa wakulima wa mboga na matunda wanaosafirisha mazao hayo kwenda nchi za Ulaya. Anasema kupunguza safari za ndege ni sawa na kulazimisha bei za kusafirisha mizigo kwenye ndege kuongezeka na kuwaumiza wakulima nchini. “Uamuzi wa kupunguza safari za ndege ni kama vile umejipiga risasi mguuni,” anabainisha Teri.

Mchumi kutoka Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Abel Maganga anasema mgogoro huu usipopata suluhisho la kudumu haraka, Jumuia itakuwa na changamoto kwenye sekta ya uchumi kwa mataifa yote mawili.

Hata hivyo, anaamini hata kama hawatafikia mwafaka, Tanzania inaweza kujipanga upya katika kuangalia njia mbadala za kuwaleta watalii nchini. “Hakuna mgogoro usiokuwa na athari, lakini sisi (Tanzania) tupo katika upande mzuri zaidi,” anasema Maganga.

Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii (CCK), Constantine Akitanda anaonyesha wasiwasi kwamba mgogoro huo ukiendelea unaweza kuota mizizi hadi kwenye nchi nyingine za Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC).

Anasema Tanzania na Kenya ni miongoni mwa nchi kubwa ambazo zilikuwa na ushawishi mkubwa katika kuunda EAC. Kwa sababu hiyo, migogoro baina ya mataifa haya inaweza kuyumbisha mipango yote ya Jumuia na kuifanya pengine isambaratike. Watu waliochanganua mgogoro huu, wameweka wazi una hasara kwa pande zote za mataifa haya. Ndiyo maana hata marais wa nchi hizi wameliona hilo na kuamua kuwa ipo haja ya kuondoa vikwazo vilivyowekwa na badala yake wajadiliane kama kuna tatizo lisuluhishwe.

Wananchi katika mataifa haya mawili wanasubiri kwa hamu majadiliano ya mwisho ya wawakilishi wa marais hawa watakaokutana mwezi ujao ili kuyaweka mambo sawa. Kwa kuwa suala hili linagusa uchumi wa mataifa haya, ni vyema wawakilishi hao wakawa na busara ya kufikia uamuzi utakaokuwa na manufaa wananchi wa pande zote.