China ya sasa, Tanzania ijipange kunufaika zaidi

Muktasari:
- Tanzania na China zina uhusiano tangu mwanzoni mwa miaka ya 1960 zilipokuwa sawa kiuchumi. Sasa hivi, China ni taifa la pili kwa uchumi mkubwa duniani lenye marafiki wengi. Ili kuendelea kunufaika, viongozi wanapaswa kuweka mikakati kwa kubainisha vipaumbele na kuvifanyia kazi.
China imesherehekea miaka 69 tangu kuanzishwa kwake Jumatatu ya wiki hii. China huadhimisha siku hiyo kila Oktoba Mosi. Mwandishi wetu, Julius Mnganga amepata nafasi ya kuzungumza na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mbelwa Kairuki juu ya mustakabali wa diplomasia baina ya mataifa haya mawili yaliyoshibana kisiasa kwa muda mrefu.
Swali: Ni mambo gani Tanzania inajivunia kutokana na uhusiano wake na China kwa zaidi ya miongo minne sasa?
Jibu: Miongoni mwa mambo yaliyoshamirisha uhusiano ni China kuiunga mkono Tanzania katika harakati za ukombozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika na Tanzania kuongoza harakati za kuiwezesha Jamhuri ya Watu wa China kutambulika Umoja wa Mataifa na kuwa mwanachama wa kudumu wa baraza la usalama.
Yapo mengi ya kujivunia kutokana na uhusiano uliopo kati ya Tanzania na China. China ni mshirika wa kutumainiwa wa Tanzania katika nyanja za kimataifa. Mara zote Tanzania inapokuwa na ajenda Umoja wa Mataifa, China huunga mkono bila kusita.
Tanzania ni miongoni mwa mataifa yaliyonufaika na misaada ya China tangu miaka ya 1960 hadi leo. Reli ya uhuru (Tazara) ilijengwa kwa mkopo usio na riba kutoka China, mradi mkubwa wa kwanza kufanywa na China nje ya mipaka yake.
Tanzania pia inanufaika na misaada ya China katika sekta ya elimu na afya. Kwa miaka 50 China hutuma madaktari wake kufanya kazi nchini huku maelfu ya Watanzania wakipata fursa ya mafunzo nchini China.
Swali: Kama kuna sehemu ya kuboresha kwenye diplomasia iliyopo baina ya mataifa haya, ungeshauri wapi pafanyiwe marekebisho?
Jibu: Diplomasia iliyopo baina ya China na Tanzania ni nzuri na imezidi kushamiri. Jambo la msingi kutambua ni ukweli kwamba mtazamo wa diplomasia umebadilika. Zamani mkazo ulikuwa kwenye uhusiano wa kisiasa lakini hivi sasa ni uchumi. Kila nchi inaangalia itapata nini.
China ya leo si ya zamani, miaka ya 1960 ikiwa masikini na isiyo na marafiki wengi wanaoitegemea, ndio maana wachache iliokuwa nao ikiwemo Tanzania, walifaidika sana kwa misaada na mikopo isiyo na riba.
Zama zile tulijengewa reli ya Tazara na karakana zake, kiwanda cha Urafiki, cha zana za zilimo (ZZK), cha matrekta Mahonda na shamba la mpunga Mbarali kwa uchache. China ya sasa, ni taifa lenye nguvu kubwa kiuchumi, kiteknolojia na kijeshi. Inatumainiwa na ulimwengu mzima.
Hivi sasa, China ipo katika kundi la G20, Brics, Shanghai Corporation ambako imejenga uhusiano wa kiuchumi na wengi.
Mataifa tajiri na masikini yote yana urafiki na China siku hizi yakitaka kunufaika na fursa za biashara hasa masoko, uwekezaji, utalii, na mikopo. Hivi sasa, China ipo katika kundi la G20, Brics, Shanghai Corporation ambako imejenga uhusiano wa kiuchumi.
Katika mazingira hayo, sio rahisi kwa nchi moja kupata ‘full attention’ ya China kama ilivyokuwa miaka ya 1960. Ni lazima kujipanga kimkakati na kubaini maeneo ya kimkakati kunufaika. Tukishayabaini hatuna budi kujipanga.
Endapo tutaamua kunufaika na soko la bidhaa basi tuzalishe kwa wingi na ubora unaokubalika ili kulikamata soko na kufaidika nalo. Kama ni utalii, kujidhatiti kuanzia matangazo hadi miondombinu ya kuwahudumia maelfu ya wageni kutoka China.
Kama tunataka kujenga uwezo wa kitaalam na teknolojia, lazima tubainishe maeneo ya kipaumbele kama ni uhandisi na kilimo, tuwaambie Wachina fursa wanazotupa zijielekeze huko.
Swali: Rais Magufuli anasisitiza diplomasia ya uchumi…unalitekelezaje jukumu hili kuhakikisha Tanzania inanufaika zaidi na uhusiano uliopo baina yake na China?
Jibu: Ni kweli mabalozi wote tumepewa mwongozo na maelekezo ya kutafuta fursa za biashara, uwekezaji, utalii na misaada kwa manufaa ya Watanzania ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya mambo ya nje.
Kwenye uwekezaji, ubalozi umeandaa makongamano 10 kuvutia uwekezaji, umefanya mikutano na kampuni zaidi ya 100 ili kuzishawishi kuwekeza nchini. Kwa miaka miwili iliyopita miradi mipya 196 yenye thamani ya Dola 1.25 za Marekani imesajiliwa nchini katika sekta za viwanda, makazi, kilimo na uvuvi.
Ubalozi umetafuta masoko kwa kushiriki maonyesho mbalimbali kutangaza bidhaa za Tanzania. Kwa mwaka mmoja uliopita ubalozi umeshiriki maonesho makubwa saba katika miji ya Guangzhou, Haikou, Hangzhou, Yiwu, Qingdao, Nanning.
Katika maonyesho hayo bidhaa za Tanzania kama vile kahawa, chai, asali, mvinyo, ufuta, mbaazi na choroko zilioneshwa. Hivi sasa kuna shauku kubwa ya China kununua bidhaa kutoka Tanzania. Ujazo wa biashara kati ya China na Tanzania umefika Dola 4.3 bilioni kwa mwaka.
Katika mkutano wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika, China ilitangaza kutenga Dola 5 bilioni kununua bidhaa kutoka Afrika. Hiyo ni fursa muhimu inayopaswa kuchangamkiwa.
Rai yangu kwa taasisi zenye dhamana ya kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali nchini kama vile Tnatrade, bodi za kahawa, chai, korosho, nafaka na mazao mchanganyiko, mkonge na pamba zichangamkie soko la China kwa kushiriki maonyesho ili kutafuta masoko mapya.
Utalii
Kuhusu utalii, ubalozi unashirikiana na wadau nchini kuwavutia Wachina kutembelea Tanzania. Katika mwaka mmoja uliopita, ubalozi umeshiriki maonesho katika miji ya Beijing, Zhoushan, Guangzhou na Changsha.
Aidha, ubalozi unatumia vyombo vya habari hususan televisheni na mitandao ya kijamii ya China kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini. Binafsi nimefanya mahojiano mara tatu na televisheni za China kutangaza vivutio vya utalii.
Vilevile, tuliandaa timu ya waandishi wa habari kutangaza vivutio vya utalii vilivyorushwa kwenye runinga kama Travel Channel ya vipindi vya utalii vinavyoangaliwa na watu milioni 750 hapa China. Waandishi hao watashiriki maonesho ya Swahili Expo yatakayofanyika mwezi huu jijini Dar es Salaam na kwenda kutembea mbuga za Serengeti, Ngorongoro, Tarangire na Zanzibar.
Aidha, ubalozi kwa kushirikiana na mwakilishi wa heshima wa Tanzania jijini Hong Kong, Dk Annie Wu umewezesha maonesho ya kimataifa ya wanamitindo vijana kutoka China na nchi nyingine kufanyikia jijini Dar es Salaam (Septemba 28) yakivishirikisha vyombo vya habari kutoka Hong Kong hivyo kuitangaza Tanzania nchini China.
Kutokana na juhudi hizo, idadi ya watalii imeongezeka. Mwaka jana Tanzania ilipokea watalii 34,000 wakilinganishwa na 20,000 wa mwaka 2015. Matarajio yetu ni idadi hiyo kuongezeka zaidi zitakapoanzishwa safari za moja kwa moja za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kutoka China hadi Tanzania.
Hivi sasa ubalozi unashirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kuandaa makogamano maalum ya kutangaza utalii katika miji ya Shanghai, Guangzhou, Chengdu na Beijing. Makongamano hayo yatafanyika kuanzia tarehe 12 mpaka 20 Novemba.
Misaada
Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazonufaika zaidi na misaada ya China kupitia Focac kwani jumla ya miradi 11 imeidhinishwa na ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Miradi hiyo ni ujenzi wa jengo la Wizara ya Mambo ya Nje, maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Ufundi Kagera, ukarabati wa Uwanja wa Taifa na Chuo cha Polisi Moshi (CCP).
Vilevile, kuna ujenzi wa miradi miwili ya maji Unguja na Pemba, ukarabati wa Hospitali ya Abdula Mzee huko Pemba, ukarabati wa Uwanja wa Mao Tsetung Unguja na ujenzi wa nyumba za madaktari Pemba. Aidha, China imeipa Tanzania msaada wa dawa za malaria.
Hata kwenye miradi, China imesaidia kufanya upembuzi yakinifu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere kilichopo Butiama, mradi wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa (standard gauge) na mradi wa mipango miji mitano ya Tanzania. China ipo mbioni kutuma wataalam kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa chuo kikuu cha usafirishaji.
Kwa miaka miwili iliyopita, Watanzania 450 wamepata mafunzo ya muda mrefu China na 1,029 ya muda mfupi. Ubalozi unaendelea kutembelea vyuo mbalimbali kutafuta fursa zaidi za masomo na ufadhili.
Swali: Kwenye mkutano wa Focac, China iliahidi kutoa Dola bilioni za Marekani ikiwa ni mikopo nafuu na misaada kwa nchi za Afrika. Tanzania ina nafasi gani ya kunufaioka na fedha hizo?
Jibu: Fedha hizo zitaelekezwa kwenye maeneo manane ukiwamo ujenzi wa maeneo maalum ya viwanda ambayo Tanzania inayo fursa kuvutia wawekezaji kutoka China kuyajenga katika mikoa ya Pwani, Tanga, Mtwara, Lindi na Kigoma.
Kuna miundombinu ya nishati, usafirishaji, habari na mawasiliano vielvile. Kwa sasa Tanzania inajenga reli ya kisasa (SGR) na mradi wa umeme wa Stigler’s inaweza kunufaika pia.
Fedha hizo pia zitatumika kukuza biashara kati ya China na Afrika, Tanzania ina nafasi ya kuchangamkia soko la bidhaa mbalimbali.
Kipaumbele kingine ni kutunza mazingira kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Vilevile kuna mpango wa kuimarisha mafunzo ya ufundi ili kufanikisha uwekezaji endelevu wa viwanda. Kati ya nafasi 50,000 zilizotangazwa, tunakusudia kupata walau 3,000 katika miaka mitatu ijayo.
Fedha hizo pia zitatumika kuboresha sekta ya afya. Tanzania itachangamkia mafunzo ya wataalam hasa fani ya tiba za miondozi, figo, moyo, mishipa na ubongo.
Hata katika masuala ya habari, utamaduni, sanaa na michezo, tutatangaza vivutio vyetu vya utalii na utamaduni wa Tanzania kwenye matamasha na maonyesho makubwa.
Eneo la nane ni ulinzi na usalama ambalo ni miongoni mwa kiini vya uhusiano wa Tanzania na China uliodumu kwa muda mrefu.