Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watafiti wabuni mbu wa vinasaba kupambana na malaria

Mkurugenzi wa Mradi wa kutokomeza maambukizi mapya ya malaria katika Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), Dickson Wilson Lwetoijera, akitambulisha teknolojia ya mbu wa kijenetiki katika Kongamano la 33 la Kisayansi jijini Arusha Juni 10, 2026. Picha na Bertha Ismail

Muktasari:

  • Teknolojia hiyo mpya inalenga kubadili vinasaba vya mbu ili wasiweze kusambaza vimelea vya malaria Kwa kuathiri kizazi kilichopo na kuzaliwa kingine kisichoeneza ugonjwa huo.

Arusha. Watafiti wa Tanzania kwa kushirikiana na wenzao kutoka Uingereza, wamefanikiwa kubuni teknolojia mpya ya mbu waliobadilishwa kijenetiki inayolenga kuzuia kusambaa kwa vimelea vya ugonjwa wa malaria.

Imeelezwa kwamba hatua hiyo inaenda kuwa na uwezo mkubwa wa kusaidia juhudi za kutokomeza ugonjwa huo nchini na barani Afrika.

Teknolojia hiyo inalenga kubadili vinasaba vya mbu ili kupunguza au kuondoa kabisa uwezo wao wa kusambaza vimelea vya malaria kwa binadamu, huku ikichochea kuzaliana kwa kizazi cha mbu wasiokuwa na uwezo wa kueneza ugonjwa huo.

Maendeleo hayo yamewasilishwa leo Alhamisi Jubni 11, 2026 jijini Arusha katika Kongamano la 33 la Kisayansi lililoandaliwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), na kuwashirikisha zaidi ya washiriki 450, wakiwemo watafiti, watunga sera, wataalamu wa afya na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi wa Mradi wa Kuzuia Maambukizi Mapya ya Malaria katika Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), Dickson Wilson Lwetoijera amesema majaribio ya awali ya teknolojia hiyo tayari yameanza katika maeneo ya visiwani ili kutathmini ufanisi wake kabla ya kupelekwa katika maeneo mengine ya nchi.

Amesema mbu hao wameundwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya uhariri wa vinasaba (gene editing), inayowezesha sifa maalumu za kijenetiki kuenea kwa haraka ndani ya jamii ya mbu na hivyo kupunguza uwezo wao wa kusambaza malaria kwa binadamu.

“Utafiti huu unafanyika chini ya usimamizi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Kitengo cha Mazingira. Tumeanza majaribio katika maeneo ya visiwani kama Ukerewe, ambako kuna idadi kubwa ya mbu na kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria,” amesema Lwetoijera.

Kwa mujibu wake, majaribio hayo yanalenga kupima uwezo wa teknolojia hiyo katika kupunguza maambukizi ya malaria pamoja na kutathmini athari zake kwa mazingira, kabla ya kuidhinishwa kwa matumizi katika kiwango kikubwa.

Amesema iwapo matokeo yataendelea kuwa chanya, teknolojia hiyo inaweza kusaidia kufikia kiwango cha karibu sifuri cha maambukizi ya malaria katika maeneo husika ndani ya kipindi cha miaka mitano hadi saba.

“Uwezekano wa kufikia sifuri ya maambukizi ya malaria kupitia teknolojia hii ni mkubwa. Kinachohitajika ni ushirikiano wa wananchi na msaada wa serikali ili kuhakikisha utafiti huu unafikia hatua za mwisho na kuleta manufaa kwa jamii,” amesema.

Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Thomas Chali amesema teknolojia hiyo inaweza kuwa nyenzo muhimu katika kufanikisha azma ya Tanzania ya kutokomeza malaria.

“Tunaendelea kukamilisha majaribio na tathmini zote zinazohitajika. Baada ya hapo tutakuwa katika nafasi nzuri ya kuamua hatua zinazofuata kuhusu utoaji wa vibali na utekelezaji wake,” amesema.

Amesema mbali na kupunguza maambukizi ya malaria, teknolojia hiyo inaweza kuongeza ufanisi wa mikakati mingine inayotumika kwa sasa, ikiwemo matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu, upuliziaji wa dawa za kuua mbu na matibabu ya wagonjwa.

Kongamano hilo linafanyika chini ya kaulimbiu isemayo, “Huduma za Afya kwa Wote: Kujenga Mfumo Madhubuti na Endelevu wa Afya kwa Tanzania ya 2050” na limepokea jumla ya mawasilisho 339 ya kisayansi yanayolenga kutoa suluhisho kwa changamoto mbalimbali za afya nchini na duniani.

Naye mtafiti mkuu kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Alphaxard Manjurano, amesema endapo majaribio yataonyesha kuwa teknolojia hiyo ni salama, yenye ufanisi na rafiki kwa mazingira, inaweza kuwa miongoni mwa mbinu muhimu zaidi katika juhudi za Tanzania na Afrika za kutokomeza malaria.