Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wataalamu wa afya wasisitiza tafiti kupunguza vifo vinavyozuilika

Baadhi ya watafiti wakionyesha machapisho na dawa katika Mkutano wa Kisayansi wa mwaka 2026 ulioandaliwa kwa pamoja na Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU).

Muktasari:

  • Mkutano huo ulihusisha mada sita kuu zinazogusa maboresho ya ubora wa huduma na usalama wa wagonjwa, huduma zinazomlenga mgonjwa, uimarishaji wa mifumo ya afya na rasilimali watu, afya ya kidijitali na ubunifu, mwendelezo wa huduma katika hatua zote za maisha pamoja na ubora wa utafiti na ufundishaji wa taaluma za afya.

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya, watunga sera, watafiti na wadau wa sekta ya afya wamesisitiza umuhimu wa matumizi ya ushahidi wa kisayansi (tafiti) katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa, ili kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.

Mjadala huo umefanyika leo Alhamisi, Juni 4, 2026 katika Mkutano wa Kisayansi wa mwaka 2026 ulioandaliwa kwa pamoja na Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), chini ya kauli mbiu isemayo: “Kuboresha Ubora wa Huduma za Afya Tanzania: Kutoka Ushahidi wa Matokeo hadi Ubora.”

Mkutano huo wa siku mbili utakaofanyika Juni 4 na 5, umejikita katika kutafuta suluhisho za vitendo za kuimarisha usalama wa wagonjwa, kuboresha huduma zinazomlenga mgonjwa, kuendeleza rasilimali watu wa afya na kutumia teknolojia za kidijitali katika utoaji wa huduma.

Akifungua mkutano huo, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea amesema ubora wa huduma za afya haupaswi kupimwa kwa upatikanaji wa huduma pekee bali kwa matokeo yake katika maisha ya wananchi.

“Ubora wa huduma za afya haupimwi tena kwa upatikanaji wa huduma pekee, bali kwa athari zake katika maisha ya wananchi. Ushirikiano kati ya Serikali, vyuo vikuu, taasisi za afya na wabunifu ni muhimu katika kujenga mfumo wa afya imara unaomlenga mgonjwa,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Huduma za Afya Aga Khan Tanzania, Sisawo Konteh amesema mkutano huo umeandaliwa kwa lengo la kuhamasisha utekelezaji wa suluhisho bunifu zitakazosaidia kuboresha mifumo ya afya na matokeo ya huduma kwa wananchi.

“Mjadala huu umevuka mipaka ya nadharia na kuelekea kwenye vitendo. Tunataka kuona mawazo na tafiti zikigeuka kuwa hatua zinazoweza kuboresha huduma za afya kwa Watanzania,” amesema.

Akiwasilisha mada katika mkutano huo, mtaalamu wa masuala ya afya, Dk Meshack Shemwela amesema ubora wa huduma msingi wa huduma za afya na ni mwanzo mzuri wa kufanikisha mapambano ya magonjwa mbalimbali hasa kwa kutumia ushahidi wa kisayansi.

“Ukitaka kufahamu hili, vifo vingi duniani vinatokea si kwa sababu ya magonjwa bali ni ubora wa huduma. Hili limeonekana katika tafiti zetu hapa nchini na duniani kote tafiti zinasema hivyo,” amesema Dk Shemwela.

Mkutano huo ulihusisha mada sita kuu zinazogusa maboresho ya ubora wa huduma na usalama wa wagonjwa, huduma zinazomlenga mgonjwa, uimarishaji wa mifumo ya afya na rasilimali watu, afya ya kidijitali na ubunifu, mwendelezo wa huduma katika hatua zote za maisha pamoja na ubora wa utafiti na ufundishaji wa taaluma za afya.

Pia warsha sita za kitaalamu zilifanyika kabla ya mkutano zikilenga kuimarisha ujuzi katika maeneo mbalimbali ikiwemo huduma ya kwanza, afya ya kidijitali, huduma za watoto wachanga, ufundishaji wa tiba, upimaji wa ubora wa huduma na usalama wa matumizi ya dawa.

Waandaaji wa mkutano huo wamesema pamoja na kusambaza matokeo ya tafiti na ushahidi wa kisayansi, kusanyiko hilo limeweka msingi wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya taasisi za afya, wasomi na watunga sera kwa lengo la kuimarisha mifumo ya huduma za afya nchini.