Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viazi lishe hupunguza kasi ya uzee

Mbegu ya viazi lishe vilivyofanyiwa utafiti na kuongezewa virutubisho kwa lengo la kuboresha afya kwa mlaji. Picha na Elias Msuya

Muktasari:

  • Wengine huvisindika viazi hivyo kwa lengo la kupata unga kwa ajili ya uji, kuoka vitafunwa vya aina tofauti zikiwamo keki, donati, mkate ambao huongezewa unga wa ngano kidogo.

Zao la viazi limeendelea kulimwa nchini kwa muda mrefu sasa. Na viazi hivyo vinatumika kama mlo kwa jamii nyingi. Hili ni zao linalopendwa duniani kote na hutayarishwa katika aina mbalimbali za mapishi ikiwa ni pamoja na kuchomwa, kuchemshwa, kukaangwa kama chipsi, futari au kusindikwa na kuwa vinywaji vya aina mbalimbali.

Wengine huvisindika viazi hivyo kwa lengo la kupata unga kwa ajili ya uji, kuoka vitafunwa vya aina tofauti zikiwamo keki, donati, mkate ambao huongezewa unga wa ngano kidogo.

Viazi hivyo pia hutengenezwa kaukau (clips) na majani yake ni hutumika kama mboga.

Lakini hivi karibuni, Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kwa kushirikiana na Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ukiriguru Mkoani Mwanza, wamefanya utafiti wa mbegu ya viazi wanayoiongezea virutubisho, ili kuboresha afya kwa mlaji wake.

Nzega ni miongoni mwa wilaya zilizonufaika na mradi wa viazi lishe ambao kwa sasa wakulima na wananchi huvilima na kuvitumia kwenye familia zao na vingine huviingiza sokoni kwa ajili ya biashara.

Kiazi lishe ni kipi?

Akifafanua manufaa ya viazi hivyo hivi karibuni wakati wa kukagua shamba la mfano la Kijiji cha Lububu, Ofisa Lishe wa Wilaya ya Nzega, Eufrasia Kihwelu alisema kiazi lishe ni kile ambacho ukikikata kina rangi ya chungwa inayotokana na kirutubishi cha beta-Carotene ambayo ni mojawapo ya vitamin A na kadiri rangi ya chungwa inavyokolea au kuiva, ndivyo kiwango cha kirutubishi hicho kinavyoongezeka.

Mbali na viazi hivyo, anasema kuna viazi vya rangi ya zambarau na vipo vyenye rangi nyeupe.

“Viazi vya rangi ya chungwa hutupatia kiasi kikubwa cha vitamin A ukilinganisha na viazi vingine.

“Kiazi cha gramu 200 kina vitamin A mara tatu zaidi ya kiasi kinachopendekezwa mtu ale kwa siku,” anasema Kihwelu.

Akieleza umuhimu wake, anasema husaidia afya ya macho, ngozi na kukua kwa mifupa, mfumo wa uzazi, tumbo, upumuaji na ukuaji bora wa mtoto.

“Hurekebisha pia kiwango cha sukari kwenye damu, huongeza kinga ya mwili, husaidia watu wasizeeke mapema na vina kiasi kikubwa cha vitamin E, B na C, ambazo ni muhimu kwa mwili wa binadamu,” anasema na kuongeza:

“Viazi hivi vina wanga kwa wingi pamoja na vitamin A, C,B1,B2, B3, B5, BC na vitamin K. Vina madini ya chuma, potashiamu, manganese kalisiamu, sodiam, folate na protini ambavyo vyote ni muhimu kwa afya zetu.

“Utafiti unaonyesha gramu 125 za kiazi lishe kilichochomwa au kuokwa hutoa vitamin A inayotakiwa na watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wenye umri wa kwenda shule, wajawazito na wanaonyonyesha. Makundi haya yako kwenye hatari ya kuwa na upungufu wa vitamin A.”

Akizungumzia umuhimu wake kwa ujumla, anasema husaidia kukinga na maradhi ya moyo, kiharusi na saratani kwa sababu madini yaliyomo husaidia moyo kufanya kazi vizuri na kurekebisha mzunguko wa damu mwilini.

“Viazi hivi vina virutubisho kama carotene ambayo hurekebisha sukari mwilini. Havina lehemu na vina nyuzinyuzi ambayo huzuia uyabisi wa tumbo (constipation) inayosaidia mlaji kupata choo laini,” anasema na kuongeza:

“Wanga wake hupandisha kiasi cha sukari polepole ukilinganisha na wanga wa vyakula vingine, kwa hiyo ni vizuri pia kwa wagonjwa wa kisukari. Hii ni kwa sababu sukari nyingi hutumika wakati wa usagaji wa chakula tumboni ukilinganisha na sukari inayopatikana kwenye viazi.”

Akifafanua kuhusu ukinzani wake kwa ugonjwa wa saratani, Kihwelu anasema Beta carotene, vitamin C na E ambazo ni anti oxidant husaidia kukinga mwili na ugonjwa huo.

“Vitamin C husaidia kuponya vidonda na kufyonzwa kwa madini ya chuma yanayotengeneza chembe za damu mwilini. Vitamin K husaidia kuganda kwa damu na muhimu kwa kutengenezwa kwa mifupa. Vitamin B husaidia kuwa na kumbukumbu na kujenga mishipa ya fahamu na madini ya folate hufanya meno kuwa imara,” anasema.

Madhara

Mtaalamu huyo wa lishe anasema kuna madhara makubwa ya kutokula viazi lishe ikiwa ni pamoja na upofu kwa watoto na kuongeza uwezekano wa maambukizi na pengine kufariki dunia mapema.

“Watoto wanapokosa vitamin A, hupata ugonjwa wa surua, kuharisha, upofu, vichomi na kupata malaria kirahisi kiasi cha kusababisha kifo. Watoto hao pia hudumaa na watu wazima wakiikosa kinga yao, uwezo wa kupona haraka hupungua pia.

“Wajawazito huwa na upungufu wa damu na mtoto aliyeko tumboni hawakui vizuri na anauwezekano mkubwa wa kuwa na upungufu wa damu,” anasema.

Kuhusu matumizi, anasema watu wote wanapaswa kula viazi kwani virutubisho vinavyohitajika mwilini vinapatikana ukilinganisha na vyakula vingine.

“Hata hivyo, kuna vyakula vingine vyenye vitamin A kama vile karoti, mapapai, maboga, maparachini na pilipili nyekundu, lakini vyakula hivyo havipatikani kirahisi na kwa wingi kama viazi,” anasema.

Mkurugenzi wa Sayansi ya Jamii wa Costech inayofadhili utafiti wa viazi hivyo, Dk Joyce Nyoni anasema lengo la mradi huo ni kuwawezesha wananchi kuwa na uhakika wa chakula na kupata virutubisho vinavyokosekana katika vyakula vingine.

“Lengo la Costech ni kusambaza mbegu za viazi lishe ili wananchi wenyewe waone namna zinavyofanya kazi. Pili tumewapa ujuzi wa namna ya kupanda mbegu,” anasema na kuongeza:

“Matarajio yetu ni kuona mbegu hizo zikisambaa kutoka kijiji hiki na kwenda vingine, kwa sababu hilo shamba darasa linatumiwa tu na maofisa ugani kufundishia.”

Miongoni mwa vikundi vilivyobahatika kubeba mradi huo wilayani Nzega ni cha Osama ambacho pia kinajishughulisha na kilimo cha mazao mengine kama pamba na mpunga.

Katibu wa kikundi hicho, Cotrida Mabula anasema wanakabiliwa na changamoto lukuki ikiwamo ya upungufu wa mtaji.

“Kwanza tuna changamoto ya ukosefu wa mbolea na dawa za kupuliza mazao yetu pindi wanaposhambulia mazao. Vilevile tunahitaji trekta ili kukuza kilimo,” anasema.

Akizungumzia mikakati ya kuvisaidia vikundi vya uzalishaji mali, Katibu Tawala msaidizi wa Mkoa wa Tabora, Lucas Kusare anasema kuna vikundi 500 mkoa mzima vya kilimo na uzalishaji mali ambavyo wanapanga kuvisaidia kifedha na kimkakati.

Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngupula ametoa wito kwa wananchi wilayani humo kuwa na mashamba ya viazi lishe kwa ajili ya kuepuka utapiamlo na kukuza viwanda.

Akizungumza katika shamba hilo la mfano, Ngupula ametoa mfano wa nchi ya China, ambayo imejikita kwenye teknolojia ikiwamo ya kilimo na viwanda.

“Hii inadhihirisha umuhimu wa sayansi ya teknolojia, ukweli inaonyesha jinsi tulivyoipuuza. Kama mnavyofahamu China na Tanzania zilipata uhuru pamoja, lakini sisi tukaendeleza mambo ya kuzaana mpaka sasa unaona tumefika milioni 53, wenzetu wakawekeza kwenye sayansi na teknolojia,” anasema Ngupula.

“Mimi nimefurahi sana baada ya kuona teknolojia hii ya viazi lishe, nilikuwa silimi viazi lishe, lakini kama hali ni hii na mimi nitalima.”

Kutokana na matokeo ya kilimo hichom DC Ngupula amesema watawahamasisha wananchi wilayani humo kulima viazi kwa ajili ya lishe na biashara.

“Mahindi yanaonyesha kutukataa, tukawahimiza walime mihogo, lakini kule wanachokipata ni wanga tu, lakini tukipigia debe viazi lishe kila familia wakalima angalau ekari moja, itasaidia sana kwenye suala zima la lishe bora,” anasema.