Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

uzazi tanzania unakabiliwa na changamoto chekwa kila uchao

Muktasari:

 Usemi wa nani kama mama una maana kubwa zaidi nchini kutokana na hatari ya kifo wanayokumbana nayo wazazi wakati wa kujifungua

Unaingia katika wodi ya wazazi katika hospitali ya wilaya, unaziona sura za wanawake walio katika uchungu wa kujifungua zikiwa  shakani.Kwanza ni  uchungu wenyewe na pili wasiwasi  mkubwa iwapo watakiepuka kifo wakati wa tendo hilo la kuleta uhai duniani.

 Aghalabu, wanawake wanaopata ujauzito katika Tanzania huambiwa: “Sali sana, kuzaa mguu mmoja jehanamu mmoja duniani.”

 Wauguzi, wakunga na madaktari nao wanajua kuwa kujifungua  katika wodi hizi ni kufa au kupona lakini wanaendelea  kuwajibika.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaweka wazi kuwa asilimia 99 ya vifo vya uzazi vinatokea katika nchi za Afrika na nusu ya vifo  hutokea katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Katika ufafanuzi huo wa takwimu za  WHO inaeleza zaidi kuwa Tanzania ni miongoni mwa  nchi 10 duniani zinazoongoza kwa kukumbwa na vifo vya uzazi.

Hapa nchini, wanawake 21 hadi 24 hufariki kila siku kwa sababu za uzazi.

Hivyo katika kila saa moja, watoto 144  hufariki dunia.

 Mratibu wa Taifa wa Muungano wa Utepe Mweupe wa Uzazi Salama Tanzania, Rose Mlay anasema tatizo la vifo vya uzazi halijapewa kipaumbele kama ambavyo mambo mengine yanapewa uzito hapa nchini na kutatuliwa.

Anafafanua zaidi na kusema kuwa kama changamoto za uzazi katika hospitali zetu zingetatuliwa, basi tungekuwa na Taifa imara na lenye watoto wenye afya.

“Natafakari ingekuwa vipi iwapo suala la vifo vya uzazi lingepewa umuhimu kama yanavyopewa matukio mengine kama saratani, Ukimwi na majanga mengine,” anasema

 Anaelezea ukubwa wa tatizo la uzazi na kusema  linatazamwa kama tukio la kawaida wakati ni janga kwani linamaliza maisha ya wanawake ambao ndiyo wazalishaji wenyewe na  kizazi ambacho kingekuwa taifa la kesho.

“Nadhani tunalichukulia kimazoea kwa sababu vifo vya uzazi vilianza kuongezeka na kuonyesha hali ya hatari tangu mwaka 1999, wanawake wengi mno wanapoteza maisha,” anasema Mlay.

 Pamoja na kuonyesha umuhimu wa kulifanyia kazi suala la vifo vya uzazi lakini pia Mlay anasema chanzo cha vifo hivi kinafahamika.

 Kwa mfano anasema changamoto kubwa iliyopo ni uhaba wa maabara zenye vifaa ambavyo vitamsaidia mama wakati wa kujifungua na ukosefu wa huduma za dharura za upasuaji.

“Lakini pia kuna changamoto ya wahudumu wa afya. Wapo wakunga wachache na wauguzi w ambao wana ufanisi wa kutoa huduma hii,” anasema

Mazingira yanayosababisha vifo vya uzazi yapo lukuki  na baadhi yameangaziwa na Utepe Mweupe ambao wanaeleza kuwa  umeme na maji nazo ni changamoto.

Katika utafiti wao, White Ribbon waliona kuwa vituo vingi vya afya havina benki ya damu salama, maji salama, hakuna mawasiliano ya simu za mezani wala kiganjani.

Mfanyakazi mmoja wa afya eneo la Wampembe Rukwa anasema: “Tufanye nini kumwokoa mwanamke anayekaribia kupoteza maisha? Hatuna chumba cha upasuaji, maabara, benki ya damu salama na maji ya bomba, pia hatuna mawasiliano kwani masaa 24 redio hazifanyi kazi kwa siku za jumamosi na jumapili na hakuna mawasiliano ya simu za mezani wala kiganjani.”

Suala la nishati ni tiketi ya kifo kwa maeneo ya vijijini, kwa mfano mfanyakazi wa Kituo cha Afya Kirando, Rukwa anasema: “Mwanamke mmoja alikuwa na uchungu pingamizi. Uchungu ukachukua muda mrefu. Tukampeleka huyu mama chumba cha upasuaji, lakini hapakuwa na umeme na jenereta lilikuwa bovu. Ilibidi tutumie tochi za simu na kumfanyia mama upasuaji na kumtoa mtoto. Tuliweza kuwaokoa.”

 Ingawa kuokoa roho ya mama na mtoto hutokea kwa nasibu kunapokuwa na changamoto kama hizi lakini mara nyingi vifo hutokea.

 Mhudumu wa Afya wa Kituo cha Afya cha Wampembe Rukwa naye anasema kuwa : “Mwanamke mmoja akiwa anajifungua alitokwa damu nyingi sana. Alichomwa sindano mbili na gari ya wagonjwa iliitwa lakini ilichelewa kwa sababu ya miundombinu duni. Wakati gari linafika lilikuta mama na mtoto wameshakufa. Ni wanawake wengi hupoteza maisha wakiwa njiani kuelekea hospitali ya Namanyere ambayo ipo umbali wa kilomita 118 kutoka Wampembe.”

Utepe Mweupe una kampeni maalum ya kuhakikisha huduma za dharura za kuokoa maisha ya wanawake zinapatikana katika vituo vya afya nchini kote.

 Takwimu zinaonyesha kuwa wanawake wachache chini ya asilimia 30 wanapata huduma kutoka kwa wataalamu wanapokuwa wanajifungua  kwa kukosa huduma za dharura za uzazi yaani upasuaji na damu salama.

Hata hivyo serikali katika mkakati wake wa 2008-2015 wa kupunguza vifo vya akina mama wakati wa uzazi  iliahidi kuwa asilimia 50 ya vituo vya afya vitatoa huduma za uzazi za dharura.

Kadhalika, serikali katika mpango wa Afya ya Msingi(MAM) iliahidi kujenga kituo cha afya katika kila kata(kila wilaya ina kata 10-15).

Pamoja na vifo hivyo kuendelea kuwa changamoto hadi sasa , mwaka 2008 Rais Jakaya Kikwete alizindua kampeni ya ‘Tokomeza Vifo Vitokanavyo na Uzazi, YAWEZEKANA, WAJIBIKA.”

 Ingawa Rais alionyesha imani kubwa kuwa inawezekana kuondoa vifo hivyo bado hakuna bajeti inayolenga huduma za uzazi za dharura katika mpango kamili wa Afya wa Halmashauri kwa mwaka 2013/14.

Utafiti unaonyesha kuwa asilimia 15 ya wanawake huhitaji huduma za dharura za upasuaji wakati wa kujifungua ambazo hazipatikani katika vituo vingi vya afya.

 Wakati wanawake 24 wakipoteza maisha kila siku, watoto 100,000 kufa kabla ya kusherehekea mwaka wa tano wa kuzaliwa na wengine 50,000 kuzaliwa wafu, Rais wetu ni Mwenyekiti mwenza wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Taarifa na Uwajibikaji wa Afya ya Akinamama na Watoto.