Unywaji pombe haramu bado tishio Kilimanjaro

Baadhi ya wa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro wakiwa kwenye kikao cha baraza hilo kilichoketi katika ukumbi wa Halmashauri hiyo kujadili masuala mbalimbali.
Muktasari:
- Vijiji vinavyotajwa kuongoza kwa unywaji wa pombe haramu hasa katika muda wa kazi ni vijiji vya Orori, Tela, Mrama na Usari vilivyopo Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro.
Hai. Baadhi ya wananchi wa vijiji vinne vilivyopo Kata ya Narumu, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, wametajwa kuongoza kwa unywaji wa pombe haramu kupita kiasi, hasa katika saa za kazi, hali inayodaiwa kuchangia kuzorota kwa shughuli za maendeleo.
Hayo yameelezwa na Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Blandina Mweta, Aprili 30, wakati akiwasilisha rasimu ya sheria ndogo ya kudhibiti unywaji wa pombe haramu na pombe saa za kazi, mbele ya Baraza la Madiwani.
Mweta amesema vijiji vya Orori, Tela, Mrama na Usari vinatajwa kuongoza kwa tabia hiyo ya unywaji wa pombe haramu katika muda wa kazi.
Kutokana na hilo, baraza hilo la madiwani limepitisha rasmi sheria ndogo hiyo, ambayo inamtaka mtu yeyote atakayekutwa akinywa au kuuza pombe katika saa za kazi kutozwa faini kati ya Sh50,000 hadi Sh300,000.
"Rasimu ya sheria hii imeandaliwa kwa ufadhili wa Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Public Health Organization (TPHO), kufuatia utafiti uliofanywa na kubaini kuwa Kata ya Narumu ina kiwango kikubwa cha unywaji pombe kupita kiasi ndani ya Wilaya ya Hai," amesema Mweta.
Ameongeza kuwa, tangu mwaka 2023, shirika hilo lilianza kutoa elimu kwa viongozi na wananchi wa kata hiyo kuhusu athari za unywaji wa pombe, na baadaye wakapendekeza kutungwa kwa sheria ndogo ili kudhibiti hali hiyo.
"Hivyo, nawasilisha rasimu hii mbele ya baraza lako kwa mujibu wa kifungu cha 169(1) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287 ya mwaka 2022, kwa ajili ya kupitishwa rasmi," amesema mwanasheria huyo.
Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Edmund Rutaraka, ameeleza kuwa sheria hiyo ni hatua muhimu katika kudhibiti unywaji wa pombe wakati wa kazi na kuongeza uwajibikaji miongoni mwa wananchi.
"Mtu yeyote atakayebainika kuuza au kunywa pombe katika saa za kazi atakuwa ametenda kosa na atalazimika kulipa faini ya Sh50,000 hadi Sh300,000. Lengo ni kuhakikisha muda wa kazi unatumiwa kwa shughuli za maendeleo," amesema Rutaraka.