Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ukosefu wa ajira unahatarisha afya za Watanzania

Mawazo

Muktasari:

Hapa Tanzania ukosefu wa ajira huelezwa kuwa ni hali ya mtu kutokuwa na shughuli inayomuwezesha kupata kipato kitakachomsaidia yeye au pamoja na familia yake katika maisha ya kila siku.

Wapo pia wale wanaostaafu na kujikuta hawajaandaa mazingira mazuri ya kuendelea kuwa na kipato.

Hapa Tanzania ukosefu wa ajira huelezwa kuwa ni hali ya mtu kutokuwa na shughuli inayomuwezesha kupata kipato kitakachomsaidia yeye au pamoja na familia yake katika maisha ya kila siku.

Kutokana na hali hiyo, wenye ajira ni pamoja na wale walioajiriwa au kuajiri kwenye mfumo rasmi au usio rasmi. Asiye na ajira anawekwa katika kundi la wale ambao hana shughuli ya kumpatia kipato.

Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga alinukuliwa akisema ukosefu wa ajira kwa Tanzania umefikia kiasi cha asilimia 12. Kiasi hiki cha watu wasiokuwa na ajira ni sawa na idadi ya watu milioni sita.

Watu wengi wanafikiri kuwa ukosefu wa ajira ni tatizo la kiuchumi pekee, lakini watafiti wa masuala ya afya wanabainisha kuwa hili pia ni tatizo kubwa la afya ya jamii.

Katika utafiti uliochapishwa mwaka huu hivi karibuni katika Jarida la The Lancet Psychiatry, unaonyesha kuwa ukosefu wa ajira unasababisha vifo vya watu wengi duniani.

Utafiti huo ulioongozwa na Dk Carlos Nordt wa Hospitali ya Magonjwa ya Akili katika Chuo Kikuu cha Zurich, Uswisi ulibaini kuwa kati ya mwaka 2000 na 2011, ukosefu wa ajira duniani ulisababisha takriban vifo vya watu 45,000, vilivyotokana na kujiua kila mwaka.

Ripoti za kiuchunguzi kutoka pande mbalimbali za dunia zinaonyesha kuwa, siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la watu wasiokuwa na ajira pia ongezeko la watu wanaojiua au wanaojaribu kujiua.

Utafiti wa Shirika la Afya Duniani

Shirika la Afya Duniani (WHO) katika uchunguzi wake uliochapishwa mwaka 2014, lilibaini kuwa kila sekunde 40 mtu mmoja duniani hujiua na inakadiriwa kuwa watu 800,000 hufa kila mwaka kutokana na kujiua. Hapa nchini tatizo la kujiua ni kubwa kiasi kwamba Tanzania inashika namba ya nane duniani kati ya nchi zinazoongoza kwa watu kujiua.

Ingawa kuna sababu nyingi zinazofanya watu kujiua au kupata madhara ya kiafya hapa nchini, kuna uwezekano mkubwa pia kuwa Watanzania wengi huhatarisha maisha yao kutokana na tatizo la ukosefu wa ajira.

Septemba mwaka jana Ernest Magashi wa Bukombe mkoani Geita aliripoti habari za mtoto mdogo Hadija Deo wa mtaa wa Kapala, Kata ya Igulwa aliyekutwa katika hali mbaya ya kiafya baada ya mama yake Zainabu Selemani kudaiwa kumficha ndani kwa muda mrefu.

Septemba 2014, gazeti hili liliripoti habari za mkazi mmoja wa Kata ya Tuangoma, Temeke jijini Dar-es-Salaam, Aisha Jumanne aliyedai kuwa afya na maisha yake pamoja na watoto wake vimo hatarini kutokana na ukosefu wa ajira.

“Sina kazi yoyote ya kunipatia kipato hata mume wangu hana kazi zaidi ya kujishikiza kwenye vibarua… Hatuna jinsi ila kuishi hapa hata kama mvua inanyesha,” anasema Aisha akielezea hali duni ya mazingira na nyumba wanayoishi ambayo imejengwa kwa udongo na kuezekwa kwa makuti na huvuja wakati wa mvua.

Februari 13, 2015 gazeti hili pia likaripoti juu ya karani wa zamani wa benki moja hapa nchini, Armstrong Bangili aliyeahirisha uamuzi wake wa kujinyonga kutokana na kukabiliwa na ugumu wa maisha. Hii ilitokea baada ya kupoteza ajira yake.

Uuzaji viungo vya mwili

Bangili mwenye miaka 45, sasa ameamua kutafuta mtu wa kununua figo yake moja, ili ajikimu kimaisha. Watu wengi walichukulia uamuzi huo kuwa ni wa kuhatarisha maisha yake.

Watafiti wa masuala ya afya ya jamii wanasema kuwa, watu wengi wasiokuwa na ajira hujihusisha na tabia hatarishi kwa afya kutokana na msongo wa mawazo.

Wengi hutumia, tumbaku, dawa za kulevya na pombe kupita kiasi. Wengi pia huishi maisha ya kubweteka bila kufanya mazoezi na hawajihusishi na michezo salama.

Utafiti uliofanywa na Dk Margaretha Voss pamoja na wenzake huko Sweden, unaonyesha kuwa watu waliopoteza ajira wanakabiliwa na hatari kubwa ya kufa kutokana na magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na saratani. Utafiti huo ulichapishwa katika jarida la Afya ya Jamii toleo la 94(12) la mwaka 2004.

Utafiti wa Elizabeth Harris na Mark F. Harris uliochapishwa katika jarida la The Medical Journal of Austraia (MJA), toleo la 191(2) mwaka 2009 nao unasema kuwa ukosefu wa ajira unajulikana kwa kusababisha magonjwa ya akili, wasiwasi, msongo wa mawazo, kujiua na magonjwa ya moyo. Magonjwa mengine ni yale yanayoshambulia mfumo wa njia ya hewa, mifupa, misuli ya mwili pamoja na kisukari.

M.W. Linn, R. Sandifer na S.Stein katika utafiti wao kuhusu athati za kiafya zitokanazo na ukosefu wa ajira walibaini kuwa watu wasiokuwa na ajira, huenda hospitalini mara kwa mara ili kupata huduma za matibabu kutokana na maumivu ya mwili yasiyo na sababu bayana, hutumia dawa nyingi na wanapolazwa hutumia muda mrefu kupona ikilinganishwa na wangine wanaofanya kazi za kuwapatia kipato [Am J Public Health. 1985; 75(5)].

Watu wasiokuwa na ajira pia hukabiliwa na matatizo makubwa yanayochangia kupata athari za kiafya kama vile ukosefu wa huduma bora za afya na chakula cha kutosha chenye viinilishe muhimu kwa ajili ya afya.

Watu hawa pia hukabiliwa zaidi na unyanyasaji wa kijinsia, ukatili, migogoro ya kifamilia, fedheha na aibu. Wengi pia hawapati makazi bora yanayodumisha afya njema.

Athari za kiafaya

Dk David Williams ambaye ni profesa katika Kituo cha Afya ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Harvard anasema: “Utafiti unaonesha kuwa haichukui muda mrefu kwa ukosefu wa ajira kusababisha athari mbaya za kiafya.”

Binadamu siyo roboti, ukosefu wa ajira haumaanishi kukosa fedha pekee bali unamaanisha pia kukosa usalama, kukosa utulivu wa kihisia na mtandao wa kijamii wa watu wengine, mambo ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaathiri afya ya mwili na akili.

Kama Taifa ni jukumu letu sote kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana nchini, ili kunusuru afya za mamilioni ya Watanzania na kuboresha hali ya maisha.