Ugonjwa wa kutetemeka mwili na tiba yake mbadala

Muktasari:
- Pia, si ajabu mtu huyo mwenye dalili hizo akawa anapatiwa usaidizi wa mambo mbalimbali ikiwamo kutembea toka kwa ndugu, jamaa, rafiki na wahudumu wa afya.
Katika maisha ya kila siku yawezekana umewahi kukutana na kumwona mtu mzima mwenye umri mkubwa aliye na dalili za kutetemeka mwili, kutembea kwa upole na pengine akawa na shida ya kuzungumza vizuri.
Pia, si ajabu mtu huyo mwenye dalili hizo akawa anapatiwa usaidizi wa mambo mbalimbali ikiwamo kutembea toka kwa ndugu, jamaa, rafiki na wahudumu wa afya.
Unapomwona mtu wa namna hiyo, fahamu kuwa hayo ni maradhi yanayoathiri mfumo wa fahamu. Kutetemeka kwa mwili si kama mgonjwa anapenda, bali ni athari zinazojitokeza baada ya mfumo wa fahamu kuathirika.
Ugonjwa wa kutetemeka mwili pasipo hiyari, hujulikana kitabibu kama Parkinson. Ugonjwa ambao huathiri sehemu mojawapo ya mfumo wa fahamu.
Wagonjwa wengi wanapatwa na tatizo hili wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 60 huku wastani ni umri wa miaka 57. Huathiri asilimia moja ya watu wenye umri wa zaidi ya miaka 65. Mara chache sana ugonjwa huu hujitokeza nyakati za utotoni au kwa vijana ambao wako katika balehe.
Seli za mfumo wa fahamu zinazotengeneza aina flani ya kampaundi inayoitwa dopamine, zinakuwa zimeathirika na kushindwa kutengeneza kampaundi hiyo inayosaidia mawasiliano ya sehemu za ubongo.
Ugonjwa wa huo pia una vitu vikuu vinne vinavyochangia mtu kutetemeka mikono akiwa katika hali ya utulivu. Lakini hali hiyo hupotea mara anapoanza kuushughulisha mwili.
Ubongo ndiyo mdhibiti mkuu wa matukio yote ya mwili ikiwamo kuratibu hisia za mwili, kuzungumza kwa kutamka sentensi nzima ama hotuba, kuamrisha misuli kujongea, hisia za kimwili kama baridi, moto, mtetemo na pia kusikia, kuona, kutambua na kufikiri.
Parkinson ni ugonjwa wa pili kwa kuharibu mfumo wa fahamu ambao ni ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu na kusababisha mwili kutetemeka bila hiyari.
Kuendelea kukosekana kwa ufanisi wa mfumo wa fahamu husababisha misuli ya mwili kukosa udhibiti, hivyo kujongea isivyo kawaida pamoja na kutetemeka mikono, kiwiliwili na kichwa bila hiyari ya mtu binafsi.
Uligundulika lini
Ugonjwa huo ulianza kufahamika Kabla ya Kuzaliwa kwa Kristu (5000BC). Miaka hiyo tabibu wa kienyeji wa nchini India aliupa ugonjwa huu jina la Kampayata.
Alikuwa akiutibu kwa kutumia mbegu za mimea ambayo ndani yake ilisheheni kiambata tiba ambacho leo hii kinajulikana kwa jina la Levodopa.
Historia hii iliwawezesha wanasayansi wa tiba kuegemea kiambaata hicho kwa kutumia utaalamu wa dawa za kisayansi na kufanikiwa kuitengeneza dawa hiyo katika kiwango cha tiba.
Mpaka leo hii, dawa hiyo inatumika kufifisha makali ya ugonjwa huo.
Kwanini dawa ilitwa jina hilo
Jina la Parkinson lilitolewa baada ya daktari Mwingereza ajulikanaye kwa jina la James Parkinson, ambaye kwa mara ya kwanza ndiye aliyeweza kuuchambua ugonjwa huo kiundani, mwaka 1817.
Wanasayansi wa tiba wapo wanaoamini kuwa chanzo ni shughuli zinazohusisha kichwa kupata mtikisiko au majeraha, ikiwamo masumbwi ambayo mtu anapigwa ngumi kichwani.
Kuna taarifa za kitabibu zinazoonyesha kuwa watu walioshiriki vita ya kwanza ya dunia na kupata maambukizi ya aina fulani ya virusi, waliugua ugonjwa huo.
Mpaka dakika hii hakuna ushahidi wa moja kwa moja juu ya sababu yakutokea ugonjwa huu. Ingawa yapo mambo ambayo wanasayansi wa tiba wanayahusisha na kutokea kwa ugonjwa huo.
Ndani ya ubongo kuna kampaundi iitwayo Dopamine, inahusika na upokeaji na usafirishaji wa taarifa za mfumo wa fahamu katika pande mbili za ubongo ili kuweza kutengeneza mijongea ya mwilini bila tatizo lolote.
Wagonjwa wa Parkinson wenye dalili za ugonjwa huwa wanapungukiwa au kukosa kiambata cha dopamine kutokana na seli zinazozitengeneza kupungua.
Dopamine zinapokuwa ndogo, mawasiliano kwenye ubongo yanaharibika, hivyo kuwa magumu.
Hali hiyo inasababisha shughuli za eneo hilo kukosa ufanisi na udhibiti wa mienendo ya misuli ya mwili.
Kadiri dopamine inavyozidi kwisha, ndivyo athari za mwili ikiwamo ya kutikisika na kujongea kiholela huendelea kuwa juu zaidi.
Pia, seli za kwenye ubongo huendelea kupukutika jambo ambalo linachangia matatizo mengine ya mfumo wa fahamu na yale yasiyo ya matatizo ya mwili kujongea.
Pamoja ya kwamba inajulikana kuwa chanzo cha tatizo la Parkinson ni kupungua kwa kiambata cha dopamine lakini bado wanasayansi wa tiba hawana uhakika na chanzo kinachosababisha seli hizo kushindwa kuzalisha dopamine.
Wataalamu wa vinasaba na uchunguzi yakinifu wa mabadiliko ya tishu baada ya ugonjwa kuvamia mwili wanaeleza kuwa, seli za ubongo zinaweza kudhurika na kuishiwa ufanisi wake.
Mambo kama kupata shambulizi la mlipuko wa kinga baada ya kuchokozwa, sumu na madini mazito na shinikizizo lolote, vinaweza kuharibu seli za ubongo.
Hivyo, wanasayanasi wanashaka ya kupotea kwa kiambata cha dopamine kunatokana na muunganiko wa matatizo ya vinasaba na mambo yaliyo katika mazingira ya jamii.
Wanasayansi wameweza kuzibaini chembe za vinasaba ambavyo zimerithiwa na mtu aliyeathirika na kuzibaini uwapo wake kwa ndugu wa damu wa kuzaliwa.
Mambo mengine ambayo yanaweza kusababisha hali inayofanana na ugonjwa wa parkinson ni dawa zinazotumika kutibu magonjwa ya akili na kichefuchefu.
Kupata majeraha kichwani kama mtu alikuwa akicheza mchezo wa ngumi, magonjwa ya mfumo wa fahamu, kuwahi kupatwa na sumu kama ya carbonmonoxide, cyanide na kemikali zinazotengeneza rangi za mafuta na lami. Pia, saratani au uvimbe wa kawaida katika ubongo, kurundikana kwa maji kwenye ubongo, magonjwa ya ini na tezi inayozalisha homoni za ukuaji na upungufu wa vitamini B.
Katika hatua za awali, ni vigumu kwa mgonjwa kugundulika kama ana tatizo hilo, wengi wanagundulika baada ya ugonjwa kukua na huambatana na viashiria.
Dalili ya awali huonekana katika mikono. Ugonjwa huo huambatana na dalili za ukosefu wa udhibiti wa misuli hali inayosababisha kutetemeka kwa mikono, miguu na kichwa mtu anapokuwa ametulia. Miguu kuwa mizito, mwili kujongea kwa taratibu na kushindwa kuwa sawa katika mhimili wake.
Kadiri tatizo linavyozidi kuwa kubwa, linaweza kusababisha muathirika kushindwa kutembea, kuzungumza na kufanya kazi rahisi hata ya kufunga kifungo cha nguo.
Rais mstaafu wa Marekani, George W Bush, alikuwa na dalili za ugonjwa huo, lakini baadaye ilibainika kuwa lilitaka kufanana na ugonjwa wa Parkinson.
Tatizo lake lilisababishwa na athari alizopata katika mishipa ya damu iliyoivujisha na kuganda kwenye ubongo, ikamletea athari zenye dalili kama Parkinson. Lakini baadaye alibainika kuwa hana ugonjwa huu.
Hivyo si kila mtu mwenye dalili za kutetemeka mwili anaugua ugonjwa wa parkinson.
Mwili kuendelea kuathirika na ugonjwa wa Parkinson kunatofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine, wengi wa wagonjwa hawa wanaishi muda mrefu huku wakifanya shughuli za uzalishaji mali ikiwamo biashara.
Hii ni uthibitisho pia yale maeneo ya ubongo yanayohusika na fikra tunduizi, uchambuzi wa mambo na kufanya mambo kwa kutumia ubunifu wa akili, huwa haziathiriki.
Ugonjwa huu hauna tiba wala kinga ila zipo dawa zinazotumika kupunguza makali yake ikiwamo ya Levodopa.
Vilevile hakuna kipimo cha moja kwa moja cha ugunduzi wa ugonjwa huo na tatizo kuweza kubaini.
Bali muathirika hutakiwa kufanyiwa uchunguzi wa mfumo wake mzima wa fahamu.