Prime
Ufahamu ugonjwa unaokausha mate na macho kinyemela
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa ya aina hiyo hutokea pale mfumo wa kinga unaposhindwa kutambua tofauti kati ya seli za mwili na vimelea, hali inayoufanya kushambulia viungo vyake wenyewe.
Dar es Salaam. Wakati watu wakifikiria ukavu wa macho au mdomo ni tatizo la kawaida linalotokana na uchovu, matumizi ya kompyuta kwa muda mrefu au kunywa maji kidogo, wataalamu wa afya wanasema dalili hizo zinaweza kuwa ishara ya ugonjwa wa mfumo wa kinga unaoitwa Sjögren.
Kila mwaka Julai 23, dunia huadhimisha Siku ya Sjögren Duniani kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huo, ambao huwakumba mamilioni ya watu lakini bado haujulikani kwa wengi.
Ingawa si ugonjwa unaozungumzwa sana kama kisukari, saratani au shinikizo la damu, wataalamu wa afya wanasema Sjögren unaweza kusababisha madhara makubwa ikiwa hautagunduliwa mapema, ikiwemo upofu, kuharibika kwa meno na kuongezeka kwa hatari ya kupata aina fulani za saratani.
Sjögren ni miongoni mwa magonjwa yanayojulikana kama autoimmune diseases, ambapo mfumo wa kinga wa mwili, badala ya kupambana na vimelea vinavyosababisha magonjwa, huanza kushambulia tishu za mwili wenyewe.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa ya aina hiyo hutokea pale mfumo wa kinga unaposhindwa kutambua tofauti kati ya seli za mwili na vimelea, hali inayoufanya kushambulia viungo vyake wenyewe.
Kwa mujibu wa ripoti yake kuhusu magonjwa ya mfumo wa kinga (WHO Technical Report Series No. 816), Sjögren ni miongoni mwa magonjwa yanayosababishwa na mfumo wa kinga kushambulia tishu za mwili wenyewe.
Ripoti hiyo pia inasisitiza umuhimu wa utambuzi wa mapema, kuongeza uelewa miongoni mwa madaktari na kuendeleza tafiti ili kuboresha huduma kwa wagonjwa.
Kwa Sjögren, mashambulizi hayo hulenga zaidi tezi zinazozalisha machozi na mate, hivyo kusababisha ukavu wa macho na mdomo. Hata hivyo, ugonjwa huo unaweza pia kuathiri ngozi, viungo, mapafu, figo, mishipa ya damu na mfumo wa fahamu.
Chanzo chake
Kwa mujibu wa taasisi ya afya ya Marekani ya Mayo Clinic, bado hakuna chanzo kimoja kilichothibitishwa cha Sjögren.
Hata hivyo, tafiti zinaonesha ugonjwa huo hutokana na mchanganyiko wa sababu za kurithi kupitia vinasaba na mazingira.
Watu wenye mwelekeo wa kurithi ugonjwa huo wanaweza kuchochewa na maambukizi ya baadhi ya virusi au bakteria, hali inayoufanya mfumo wa kinga kuanza kushambulia mwili wenyewe.
Taasisi ya National Institute of Arthritis and Musculoskeletal and Skin Diseases (NIAMS) inaeleza Sjögren inaweza kujitokeza peke yake au ikaambatana na magonjwa mengine ya kinga kama rheumatoid arthritis na lupus.
Dalili zinazoweza kupuuzwa
Changamoto kubwa ya ugonjwa huu ni dalili zake huanza taratibu na mara nyingi huchanganywa na matatizo mengine ya kawaida.
Miongoni mwa dalili zinazojitokeza mara nyingi ni macho kuwa makavu, kuwasha au kuhisi kama yana mchanga, mdomo kukauka na ugumu wa kumeza chakula, ngozi kuwa kavu, maumivu ya viungo na misuli, uchovu unaodumu kwa muda mrefu, kuvimba kwa tezi za mate, hasa karibu na taya, upele unaoongezeka baada ya kupigwa na jua na kwa baadhi ya wanawake, ukavu wa uke.
Kwa mujibu wa kituo cha afya cha Marekani Cleveland Clinic, baadhi ya wagonjwa pia hupata matatizo ya mapafu, figo, mishipa ya damu na mfumo wa fahamu, jambo linaloonyesha kuwa ugonjwa huo unaweza kuathiri sehemu nyingi za mwili.
Hakuna tiba ya kuponya
Licha ya maendeleo ya kitabibu, hadi sasa hakuna dawa inayoweza kuponya Sjögren kabisa. Kwa mujibu wa American College of Rheumatology, matibabu yaliyopo hulenga kupunguza dalili, kuboresha ubora wa maisha na kuzuia madhara ya muda mrefu.
Madaktari hutumia matone maalumu ya macho kuongeza unyevunyevu, dawa zinazochochea uzalishaji wa mate, dawa za kupunguza maumivu ya viungo na, kwa wagonjwa wenye dalili kali, dawa zinazodhibiti shughuli za mfumo wa kinga.
Aidha, wagonjwa hushauriwa kunywa maji ya kutosha, kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa macho na meno, kutumia bidhaa zinazoongeza unyevunyevu wa ngozi na mdomo pamoja na kuepuka uvutaji wa sigara.
Kwa nini Julai 23?
Siku ya Sjögren Duniani huadhimishwa Julai 23 kila mwaka ikiwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa daktari wa macho kutoka Sweden, Dk Henrik Sjögren, aliyekuwa wa kwanza kuelezea ugonjwa huo kisayansi mwaka 1933.
Maadhimisho hayo yanalenga kuongeza uelewa wa jamii, kuhimiza utambuzi wa mapema na kuunga mkono tafiti zinazotafuta tiba bora zaidi.