Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usichokijua kuhusu tahajudi kwa afya ya mwili, akili na roho

Muktasari:

  • Wataalamu wanaeleza kuwa tahajudi kama  mazoezi ya mwili na akili yanayofanywa sehemu tulivu,  yanaboresha ufanisi wa akili, hisia, kupunguza viwango vya msongo wa mawazo na kukuza umakini.

Kwa wanaotembelea mahekalu, ni nadra kutooana baadhi ya watu wakiwa katika mikao maalum huku wakitafakari kwa kina.

Si mchezo wala watu nao hawajifurahishi. Wapo kwenye zoezi la tahajudi maarufu Kiingereza kwa jina la ' meditation'.

Ni zoezi ambalo sio tu hufanyika hekaluni, bali mahala kokote kwenye utulivu mkubwa, kwa kuwa lina uhusiano na ulimwengu wa kiroho.

Hata hivyo, unajua kama tahajudi ni njia mojawapo imara ya kuimarisha afya ya mwili, akili na hata ujenzi wa kiroho?

Wataalamu wanaeleza kuwa tahajudi kama  mazoezi ya mwili na akili yanayofanywa sehemu tulivu,  yanaboresha ufanisi wa akili, hisia, kupunguza viwango vya msongo wa mawazo na kukuza umakini.

Kuna mbinu  mbalimbali za kufanya tahajudi, lakini zinazojulikana zaidi ni tahajudi ya uzingativu au umakini (mindfulness) inayohusisha umakini kuanzia kutembea, kula na hata kutafakari.

 Tahajuhudi nyingine ni ya kurudia neno au kifungu cha maneno (Mantra) ili kusaidia utulivu wa akili, kuwa makini na kuhamasisha hali ya kiroho.

Aina nyingine  ni upendo na huruma, ambayo inakuza hisia za upendo, huruma na wema kwa mtu anayeifanya na kwa wanaomzunguka. Kuna tahajudi ya maono kupitia picha (Visualization) ambayo anayeifanya hufikiria na kuona mafanikio kabla ya uhalisia au kufikiria na kuona kitu kinachotokea au kitakachotokea.

Tahajudi nyingine ni ya kuongozwa (Guided meditation) ambapo mtu anafuata maelekezo ya mtaalamu au rekodi inayomuongoza katika hatua za kufikiria, kutafakari na kupumzika, tahajudi ya kiroho (Spiritual Meditation) ambayo ni mazoezi ya kuungana na nguvu za kiroho pamoja na tahajudi ya yoga ambayo ni mazoezi yanayojumuisha mikao ya kimwili, mbinu za kupumua na kutafakari ili kukuza ustawi wa kimwili na kiakili.


Mtaalamu wa tahajudi ambaye pia ni mwalimu wa Yoga katika Hekalu la Hindu Mandal mkoani Tabora, Bharti Suthar, anasema kufanya tahajudi ni njia bora ya kutunza afya ya kimwili na kiakili na inasaidia mtu kuishi maisha yenye usawa, furaha na upendo.


 Faida za tahajudi

Anasema inasaidia kupunguza msongo wa mawazo na huzuni kwakuwa hutuliza mfumo wa neva, na kusababisha kupungua kwa msongo na wasiwasi. Lakini pia inasaidia kutambua na kuachilia mawazo hasi ambayo wakati mwingine humfanya mtu kuhuzunika.

Anasema mazoezi hayo ya mara kwa mara ambayo yanatakiwa kufanyika asubuhi sana mahali tulivu, yanaboresha na kudhibiti hisia na hasira, hivyo mtu anayeyafanya huwa na uwezo wa juu wa kudhibiti hisia zake na kuweza kukabiliana na hali ngumu.

“Faida nyingine inaboresha usingizi kwakuwa inaweza kusaidia kupunguza matatizo ya usingizi kama vile insomnia kwa kutuliza mwili na akili kabla ya kulala, hivyo kurahisisha kupata usingizi mzuri,”anasema.

Anasema mtu anayefanya mazoezi hayo umakini wake unaimarika, kuboresha uwezo wa kumbukumbu lakini pia anaweza kuboresha uwezo wake wa kuzingatia na kuwa na umakini zaidi katika shughuli zake anazozifanya.

“Tahajudi inaweza kusaidia kubadilisha tabia zisizofaa, kama vile kupunguza utegemezi wa pombe, sigara au kula vibaya kwakuwa inaboresha mtu kujitambua na kudhibiti tabia,”anaeleza mtaalamu huyo ya Yoga.

Anasema faida nyingine za kisaikolojia na kihisia, ni kukuza hali ya kuwa na nguvu ya kiakili na kimwili, kuleta hali ya furaha, kuridhika, kuongeza nguvu, kupunguza uchovu wa mwili pamoja na kusaidia kupunguza uchovu wa akili kwa kutoa nafasi ya kupumzika na kuponya akili baada ya kazi au majukumu magumu.

Kwa mujibu wa kituo kinachojishughulisha na utafiti kuhusu mbinu za afya za ziada na za kipekee zinazotumika pamoja au badala ya tiba za kisasa cha nchini Marekani, utafiti umeonesha tahajudi inaweza kupunguza shinikizo la damu pamoja na dalili za ugonjwa wa utumbo.

Lakini pia inaweza kupunguza uwepo, muda, na ukubwa wa magonjwa ya kupumua ya ghafla. Hata hivyo, ushahidi kuhusu ufanisi wa tiba ya kuacha uvutaji sigara bado ni mdogo.

Kituo hicho kinasema matokeo ya jaribio la mwaka 2009 lililohusisha wanafunzi 298 wa chuo kikuu yalionyesha kufanya tahajudi ya tafakuri, kunaweza kupunguza shinikizo la damu kwa watu wanaotaka kupata shinikizo la juu la damu. 

Utafiti huu pia ulionyesha kufanya tahajudi, kunaweza kusaidia dhidi ya mfadhaiko wa kisaikolojia, wasiwasi, unyonge, hasira au chuki.

“Mapitio ya mwaka 2013 yalionyesha kuwa mafunzo ya uzingativu yaliboresha maumivu na ubora wa maisha kwa wagonjwa wa utumbo,  lakini hayakuboresha wasiwasi wala unyonge wao”ilisema taarifa ya utafiti huo na kuongeza:.

"Katika utafiti wa 2012, wataalamu walilinganisha picha za ubongo za watu 50 wanaofanya

tahajudi na 50 wasiofanya. Matokeo yalionyesha watu wanaofanya kwa miaka mingi wana mikunjo zaidi kwenye safu ya nje ya ubongo, ambayo inaweza kuongeza uwezo wa ubongo kuchakata taarifa.”

Katika tafiti hizo tahajudi inachukuliwa kuwa salama kwa watu wenye afya nzuri. Hata hivyo, watu wenye changamoto za kiafya huenda wasiweze kushiriki katika baadhi ya mazoezi yake yanayohusisha kushughulisha mwili.

Mazoezi hayo yanatajwa pia kuondoa hatari ya mtu kupata magonjwa ya moyo, kisukari, kupunguza maumivu na kuongeza kinga ya mwili baada ya msongo wa mawazo kupungua ambao mara nyingi huathiri mfumo wa kinga ya mwili na kuchochea maumivu.

Suthar anasema tahajudi inaweza kusaidia mtu kupata hali ya amani ya ndani na utulivu hata katikati ya matatizo, inasaidia kukuza ufahamu wa kina kuhusu nafsi na ulimwengu wa kiroho, inaleta ufahamu wa hali za kiroho, mawazo na hisia za mtu, husaidia kukuza hali ya kutafakari na kujitambua, hivyo kukuza hisia za furaha, shukrani, na upendo kwa nafsi ya mfanya mazoezi hayo na watu wengine.

“Inasaidia kuboresha uwezo wa kudhibiti hisia, hivyo kupunguza hasira, huzuni, na hali za kihisia zinazoweza kuathiri afya yako inafungua pia  akili  na kukuza ubunifu, kwani inakuwezesha kufikiri kwa kina na kuona mambo kwa mtazamo mpya,”anasema.


 Unavyoweza kufanya tahajudi

Wataalamu wa tahajudi wanashauri kabla mtu hajafanya mazoezi hayo anatakiwa kutafuta sehemu iliyotulia, isiyo na makelele wala usumbufu wowote kisha akae kwenye kiti au chini au alale kitandani au eneo analokuwa huru mwili pamoja na misuli vikiwa vimelegezwa. Lakini pia anaweza kufanya tahajudi ya kutembea sehemu tulivu.

Wanashauri kuvaa mavazi yatakayompa uhuru wa kufanya mazoezi hayo lakini kwa wanaoanza kufanya, wanatakiwa kuanza na muda mfupi ambao hauzidi dakika tano. 

Mhusika anaweza kufanya mara moja kwa siku yaani asubuhi mapema au mara mbili (asubuhi na jioni).