Siri Njombe, Moshi kuongoza kwa usafi miaka 10 mfululizo

Muktasari:
- Halmashauri ya Wilaya ya Njombe na Manispaa ya Moshi zimeongoza katika mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira kwa miaka 10 mfululizo, zikijivunia ushirikishwaji wa viongozi na uwajibikaji wa timu za usafi ngazi za vijiji. Njombe ilishika nafasi ya kwanza kwa asilimia 94.4 katika Halmashauri za Wilaya, huku Moshi ikiongoza katika Manispaa.
Njombe/Kilimanjaro. Halmashauri ya Wilaya ya Njombe na Manispaa ya Moshi zimetaja siri ya kuendelea kuwa kinara katika mashindano ya afya na usafi wa mazingira kuwa ni ushirikishwaji wa viongozi na uwajibikaji wa timu inayosimamia usafi ngazi za vijiji.
Aprili 8, 2025, katika kilele cha Wiki ya Afya, Wizara ya Afya ilitangaza matokeo ya mashindano ya afya na usafi wa mazingira ambapo kwa ngazi ya Halmashauri za Miji, Njombe ilishika nafasi ya kwanza kwa kupata asilimia 84.4 na kupata tuzo ya Sh5 milioni.

Kibao kikionyesha faini kwa wananchi ambao watatupa taka ovyo hapa mkoani Njombe
Ngazi ya Halmashauri za Wilaya, Njombe ilishika nafasi ya kwanza kwa asilimia 94.4 na kupata tuzo ya ushindi wa kwanza ya Sh20 milioni. Halmashauri za vijiji, Kijiji cha Ikuna kilipata asilimia 98.3 na kupata tuzo ya ushindi wa kwanza ya Sh4 milioni, huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Kijiji cha Kidegembye kwa asilimia 96.1.
Ngazi ya mitaa, Mtaa wa Rengua uliibuka mshindi wa kwanza kwa asilimia 90.3 na Mtaa wa Nazareth kutoka Mji wa Njombe ukipata asilimia 88.4, ukishika nafasi ya tatu, huku Mtaa wa Sido pia kutoka Njombe ukiwa katika orodha.
Ngazi za Halmashauri za Manispaa zilizohusisha jumla ya Manispaa 20, Manispaa ya Moshi iliibuka kuwa mshindi wa kwanza kwa kupata asilimia 84.2 ya alama zote, ikifuatiwa na Shinyanga iliyopata asilimia 78.0, huku Iringa ikiwa ya tatu kwa asilimia 77.7.
Njombe
Kufuatia ushindi huo, Ofisa Afya Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Brown Matebele, alipozungumza na Mwananchi jana, Aprili 9, 2025 alitaja siri ya mafanikio hayo.
Alisema Njombe imeendelea kufanya vizuri zaidi ya miaka 10, tangu mwaka 2014 hadi 2025, hawajawahi kutoka kwenye nafasi mbili za juu katika ngazi za Halmashauri katika suala la usafi wa mazingira.

Matebele alisema wameendelea kufanya vizuri katika kipindi hicho chote, huku silaha kubwa akiitaja kuwa ni ushirikishwaji wa viongozi na uwajibikaji wa timu inayosimamia usafi ngazi za vijiji.
Alisema kwenye utekelezaji wa kampeni ya afya na usafi wa mazingira, halmashauri hiyo ina timu inayosimamia utekelezaji wa shughuli hizo ambayo ina wataalamu kadhaa kutoka idara tofauti, na timu ya ufuatiliaji inayoundwa ngazi za vijiji.
"Timu hizo huwa zinaundwa na watendaji wa vijiji, wenyeviti wa vijiji pamoja na wenyeviti wa vitongoji wa vijiji husika, lakini pamoja na kuwepo kwa timu hizo tumewatengenezea sheria ndogo katika kila kijiji zinazohusu kampeni ya usafi wa mazingira," alisema Matebele.
Alisema sheria hizo ndogo zinaweza kusababisha wao kwa wao kuwajibishana, endapo mmoja au miongoni mwao wamekiuka sheria za usafi wa mazingira.
Alisema faini ambazo wananchi wanakiuka sheria ndogo za usafi wa mazingira walizojiwekea wanaziandalia taarifa ya mapato na matumizi katika kila kijiji husika, na kusomwa katika mkutano mkuu wa Serikali ya kijiji, na fedha kutumika katika shughuli za maendeleo kwenye miradi ya kijiji.
Alisema ngazi ya halmashauri zipo sheria mama zinazelezea adhabu juu ya kampeni hiyo, lakini kikubwa ni ushirikishwaji wa viongozi kuanzia mkuu wa wilaya, mkurugenzi, madiwani pamoja na watu maarufu, wakiwemo viongozi wa dini, kwani wao wamekuwa rahisi kusikilizwa kuliko wataalamu.
Alisema wamekuwa na vikao vya kubadilishana uzoefu, vinavyofanyika ngazi ya halmashauri, ambapo kila utekelezaji unapofanyika kwenye eneo husika wanakuja na changamoto pamoja na mafanikio.
"Kupitia vikao hivyo watu wanapata uzoefu kwanini mwenzangu amefanikiwa na mimi sijafanikiwa na kujifunza mikakati kwa waliofanikiwa ili na wao wafanye vizuri katika usafi wa mazingira," alisema Matebele.
Alisema vijiji vingi vilivyofanya vizuri katika usafi wa mazingira kitaifa vimetoka mkoani Njombe, hivyo kusababisha vijiji vingi kufanya vizuri kutokana na kuona wenzao wanafanya vizuri.
Alisema mwaka jana kijiji cha Kanikelele kiliongoza kwa usafi katika halmashauri hiyo, lakini kwa mwaka huu kimetoka kijiji cha Ikuna, kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Mtendaji wa Kijiji cha Ikuna, David Elisha Mkea, alisema mikakati ya kijiji hicho ili kuhakikisha kinakuwa kisafi ni kuwa kila mwezi wanafanya ufuatiliaji na ukaguzi wa mazingira, hiyo inaweza kuwa mara moja au mara mbili.
Alisema wanatumia mikutano ya aina yoyote kuzungumzia ajenda ya usafi wa mazingira, na wanaokiuka kuna adhabu ndogo ndogo kama faini, lakini pia huwa wanaangalia uwezo wa mtu.
"Mfano, kuna wazee hawana uwezo wa kutimiza masharti, hao tunawaona wadau ili kuwasaidia waendane na utaribu tunaoishi nao hapa kijijini," alisema Mkea.
Moshi
Mtaa wa Rengua, ni miongoni mwa mitaa 60 iliyopo katika Kata ya Mawenzi, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, ukiwa na zaidi ya wakazi 400, umeongoza kwa kuwa mtaa msafi nchini.
Mwenyekiti wa mtaa wa Rengua, Ladslaus Lyimo, alisema wanajivunia kuwa mtaa msafi Tanzania na kwamba watahakikisha wanaendelea kuwa wasafi.
Alisema mtaa huo, ambao upo katikati ya mji wa Moshi, miundombinu ya barabara yote ni lami, na umezungukwa na nyumba za kisasa, taasisi za umma na taasisi za kifedha.
"Kata ya Mawenzi una mitaa miwili na Rengua ina taasisi nyingi, zikiwemo za kiuchumi kama mabenki, ofisi za umma kama TRA, Tanesco, Idara ya maji na nyingine, pamoja na taasisi za dini, ikiwemo Kanisa Kuu la Katoliki la Kristu Mfalme," alisema Lyimo na kuongeza;
"Mtu ukija Rengua utakutana na mandhari nzuri, maduka makubwa ya biashara (Supermarket), pia yapo maeneo ya kupumzikia, lakini pia nyumba ni za kisasa ikiwemo magorofa, na miundombinu ya barabara ni mizuri, na mitaro ya kupitisha maji imeboreshwa. Hii ndiyo maana huwezi kusikia mafuriko mtaa wa Rengua.”
Mkurugenzi Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, alisema moja ya vitu vilivyowabeba na kuwawezesha kuongoza kwa usafi ni uwepo wa sheria ndogo iliyoainisha viwango vya kulipia ada ya taka kwenye maeneo mbalimbali kama taasisi, viwanda, kaya, na biashara.
Alisema pia vipo vikundi vya udhibiti wa uchafuzi wa mazingira, vinavyosimamia sheria ndogo katika kata zote ndani ya Manispaa.
"Sheria hii inaruhusu utozaji wa faini ya papo kwa papo kiasi kisichozidi Sh50,000 kwa wachafuzi wa mazingira. Pia tulitekeleza agizo la Serikali la kufanya usafi wa mazingira kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kwa kuhamasisha wananchi, wafanyabiashara, taasisi mbalimbali na wadau, na kampeni hii hufanyika kwenye kata zote 21 na mitaa 60.
"Pia tumeweka mawakala wa usafi wa mazingira kwenye kata 10, ili kuhakikisha usimamizi madhubuti wa taka ngumu pamoja na kuongeza idadi ya magari ya kukusanya taka ngumu kutoka saba hadi 13,” alisema.
Nasombe alisema pamoja na jitihada hizo, wamekuwa na mikakati mbalimbali, ikiwemo kuendelea kuhamasisha wakazi na wafanyabiashara kuhakikisha wanakuwa na vyombo bora vya kuhifadhia taka ngumu kwenye maeneo yao.
Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo, alisema alitambua mchango wa vijana wanaozunguka na magari ya kuzoa taka na kuwapa zawadi ya Sh1 milioni, wagawane.
Kidumo alisema amefurahishwa na manispaa hiyo kuwa ya kwanza Tanzania kwa usafi na kwamba hatua hiyo imefikiwa kutokana na mchango wa viongozi na wananchi wa manispaa hiyo.
Akizungumza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, aliipongeza Manispaa ya Moshi kwa kushika namba moja kwa usafi na kutoa mtaa bora na msafi Tanzania.

Sehemu ya maeneo ya Mtaa wa Rengua, Kata ya Mawrnzi, ambao umeibuka mshindi wa kwanza kitaifa kwa usafi.
Wakati huohuo, Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) Arusha, ilitaja mambo manne yaliyoiwezesha kushika nafasi ya kwanza katika vyuo bora kwa usafi.
Ofisa Afya wa chuo hicho, Achiwa Sapuli, alisema ushindi huo wanastahili kutokana na namna wanavyosimamia mazingira yao.
"Jambo la kwanza, tuna kampuni tumeipa kazi ya kufanya usafi, pili usimamizi ni mkubwa kwa sababu uongozi wa chuo nao unashiriki kwa asilimia kubwa. Tumeimarisha usafi kuanzia vyumba vya wanafunzi, vyoo, maeneo ya utawala na tuna bustani ambayo ina watu wanashughulika nayo," alisema.
Alisema wamejenga mitaro ya kutiririsha maji machafu na maji hayo hukusanywa kwa ajili ya urejelezwaji.
Pia alisema taka zote zilizopo chuoni hapo nyingine hutumika kutengeneza nishati mbadala ya biogesi na nyingine huchukuliwa kila wiki na kampuni maalumu waliyoipa kazi hiyo. Mbali na hayo, alisema wana mtambo wa kuchakata taka hatarishi chuoni hapo.

Achiwa alisema chuo hicho si mara ya kwanza kushika nafasi ya kwanza kwenye mashindano ya afya na usafi wa mazingira, mwaka 2022 walishika nafasi ya kwanza na 2023 nafasi ya tatu.
Imeandaliwa na Seif Jumanne (Njombe), Florah Temba na Janeth Joseph (Kilimanjaro), na Baraka Loshilaa (Dar).