Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yazitaja hospitali zinazotoa tiba asilia

Mtaalamu wa Tiba asilia, Dk Michael Magoti akionyesha aina ya dawa zinazotolewa hospitalini.

Muktasari:

  • Tanzania imeongeza hospitali 14 kutoa tiba asilia jumuishi, ikiboresha usalama na ufanisi wa dawa, wananchi wataweza kuchagua dawa za asili au kisasa kutibu magonjwa mbalimbali.

Dar es Salaam. Kama unasumbuliwa na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza na unahitaji tiba za dawa za asili, Serikali imetaja hospitali 14 za mikoa ambazo tiba hizo hutolewa, ogopa matapeli.

Hospitali hizo zimeongezeka kutoka saba ambazo Serikali, mwaka 2023, ilizitangaza kuanza kutoa huduma hiyo, sasa zimefika 14.

Daktari humpima mgonjwa na kumweleza tatizo lake na aina ya dawa zinazotibu tatizo lake ili kupata huduma ya tiba asilia katika hospitali hizo,  naye huchagua ama kutumia tiba asilia au tiba ya kisasa.

Awali, hospitali saba ambazo zilianza kutoa matibabu jumuishi ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Morogoro, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Mwanza Sekou-Toure, Arusha Mount Meru, Tanga Bombo na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya.

Mratibu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala kutoka Wizara ya Afya, Dk Mussa Lipukuta amebainisha ongezeko la hospitali hizo wakati wa mkutano uliowakutanisha wataalamu wa tiba asili, waganga wafawidhi wa mikoa na wafamasia waliokutana kujadili namna ya kuboresha utoaji huduma za tiba asili ndani ya hospitali.

Dk Lipukuta amesema miaka miwili iliyopita, Serikali ilitangaza hospitali saba kuanza kutoa tiba jumuishi na kutokana na mapokeo kuwa makubwa, zingine saba zimeongezwa.

“Hospitali za Rufaa za mikoa zilizoongezwa kutoa huduma hiyo ni Kagera, Simiyu, Rukwa, Njombe, Tabora, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala na Singida,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Idara ya Tiba Sehemu ya Tiba Asili, Dk Winfrida Kidima amesema Serikali inakusudia kuboresha huduma za tiba asilia katika hospitali zote zinazotoa huduma hizo.

Tumekutana na wataalamu wa tiba asilia, waganga wafawidhi wa hospitali 14 zitakazoanzishiwa huduma jumuishi za tiba asili, wauguzi, wafamasia na maofisa masuuli kuboresha huduma ya matumizi ya dawa za asili hospitali zote zinazotoa huduma hiyo.

“Hii ni huduma mpya, sasa tunajifunza upungufu na kuboresha huduma,” amesema.

Dk Winifrida amesema uhitaji wa dawa za asili ni mkubwa kwa wananchi, akisisitiza dawa hizo zikitumika kwa uangalifu zitaimarisha afya.

Mfamasia na Mratibu wa Huduma Jumuishi ya Tiba Asili Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Jehad Juma amesema miaka ya nyuma dawa za asili hazikuwa zimepimwa kisayansi, lakini sasa kupitia Wizara ya Afya, dawa hizo zimehakikiwa na kufanyiwa tafiti.

Kutokana na hatua hizo, amesema dawa za asili ni salama na jamii inapaswa kuwa na mapokeo chanya.

“Mtu anapokuja hospitali, tunampima, tunapogundua ugonjwa wake, tunamwambia na aina za dawa tulizonazo za kisasa na asili na yeye ndiye huchagua,” amesema.

Kuhusu upatikanaji wa dawa hizo, amesema ndani ya hospitali zilizoanza kutoa tiba jumuishi, zina dawa za asili kwa asilimia 90.

Akizungumzia magonjwa yanayotibiwa kupitia dawa hizo, amesema yapo 19, ya kuambukiza 10 na yasiyo ya kuambukiza yakiwa tisa.

Katika eneo hilo, Mfamasia wa Hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure, Donath Olomi, ametaja baadhi ya magonjwa yanayotibiwa kuwa ni maambukizi ya mfumo wa hewa, tezi dume, changamoto ya nguvu za kiume, matatizo ya uzazi, homa ya matumbo na maambukizi kwa njia ya mkojo.

“Baada ya semina hii, huduma za tiba asili zitaendelea kuimarika zaidi maana huduma hii imepokelewa vyema na wananchi,” amesema.

Kuhusu gharama, amesema hazitofautiani na dawa zingine na wakati mwingine mgonjwa anapunguziwa gharama za dawa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Watengenezaji wa Dawa Asili Tanzania (Uwadata), Dk George Buchafwe, amesema wamekuwa wakifanya tafiti kupata dawa bora za kutibu magonjwa nchini.

Hatua hiyo ni baada ya Serikali kutengeneza mpango wa tiba jumuishi ambao umeondoa dhana ya jamii kuona kinachofanywa na wataalamu wa tiba hiyo ni vitu vya ajabu.

“Serikali ilivyoanzisha tiba jumuishi, Uwadata tumekuja na mpango wa kufanya kazi na Serikali kwa kuhakikisha dawa zetu zinapimwa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na kuthibitishwa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR),” amesema.


Tafiti kuhusu tiba asilia

Mwaka 2022, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilibainisha kuwa ni dhahiri tiba za asili zina mchango mkubwa katika huduma za afya, ikiwa ni sehemu muhimu ya urithi wa kitamaduni na njia za asili za kutibu magonjwa, hususan katika maeneo ya vijijini ambapo huduma za kisasa ni nadra.

Baadhi ya tafiti kama zile zilizofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2021 na 2022, na African Journals Online (AJOL), pamoja na WHO Afro Health Monitor ya mwaka 2021, zimezitaja changamoto za matumizi ya tiba za asili.

Changamoto hizo ni ukosefu wa uthibitisho wa kisayansi, uelewa mdogo wa jamii kuhusu usalama na ufanisi wake, ukosefu wa mifumo thabiti ya udhibiti, na changamoto za kisheria zinazokwamisha matumizi yake rasmi.