Saratani kwa wasiovuta sigara yaongezeka - utafiti

Muktasari:
- Utafiti umebaini kuwapo kwa ongezeko la saratani kwa watu wasiovuta sigara huku sababu mbalimbali zikitajwa kama vile uchafuzi wa mazingira, kemikali za nyumbani na mambo yanayohusiana na kazi huzidisha matatizo ya mfumo wa kinga na kuongeza hatari ya saratani
Dar es Salaam. Utafiti mpya uliotolewa na taasisi ya saratani ya Shirika la Afya Duniani (WHO) umeonyesha kuwapo kwa ongezeko la wagonjwa wa saratani ya mapafu kwa watu ambao hawajawahi kuvuta sigara, wanawake wakiongezeka zaidi.
Matokeo ya utafiti huo yaliyochapishwa na jarida la The Lancet Respiratory Medicine yanaonyesha saratani ya adenocarcinoma, aina ya saratani ya mapafu kwa watu wasiovuta sigara, inachukua karibu asilimia 60 ya idadi ya wanaougua saratani ya aina hiyo kwa wanawake, ikilinganishwa na asilimia 45 kwa wanaume, Shirika la Utangazaji BBC limechapisha.
Hiyo ni baada ya kurekodi takriban wagonjwa wapya milioni 2.5 wa saratani ya mapafu duniani mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la wagonjwa 300,000 tangu mwaka 2020.
Utafiti utafiti huo umebainisha kuwa sababu za kimazingira, hasa uchafuzi wa hewa, jeni (vinasaba) na mfumo wa kinga ya mwili miongoni mwa mambo yanayochangia ongezeko hilo.
Mojawapo ya sababu kuu ya saratani ya mapafu kwa wasiovuta ni mabadiliko ya kijeni, haswa mabadiliko katika jeni ya EGFR ambayo hutoa maagizo ya kutengenezwa protini kwenye seli zinazohusika katika ukuaji na mgawanyiko.
Mabadiliko katika jeni hii husababisha mgawanyiko wa seli usiodhibitika na ukuaji wa saratani. Saratani hii iko asilimia 50 kwa wanawake wa Asia wasiovuta sigara, na asilimia 19 kwa wanawake wa Magharibi wasiovuta sigara, ikilinganishwa na asilimia 10 hadi 20 kwa wanaume wasiovuta sigara katika maeneo hayo.
“Zaidi ya hayo, mambo kama vile uchafuzi wa mazingira, kemikali za nyumbani na mambo yanayohusiana na kazi huzidisha matatizo ya mfumo wa kinga, na kuongeza hatari ya saratani," imeeleza sehemu ya utafiti huo.
Uchafuzi wa hewa kwa muda mrefu umeelezwa kuwa chanzo cha hatari kwa saratani ya mapafu na ushahidi ukionyesha wanawake wako hatarini zaidi.
Uchunguzi unaonyesha muundo wa mapafu ya wanawake na utendaji kazi hufanya iwe rahisi kuathiriwa na madhara ya uchafuzi wa mazingira.
Mapafu ya wanawake ni madogo kuliko ya wanaume, kwani utafiti huu unasema yanazo njia nyembamba za hewa, ambazo zinaweza kusababisha chembe ndogo zaidi, kama vile PM2.5, kunasa kwenye mapafu yao.
Wakati wanaume mara nyingi wakiwa kwenye hatari ya kukabiliwa na uchafu wa mazingira kutokana na kazi za viwandani, wanawake hutumia muda mwingi ndani ya nyumba, ambapo huvuta moshi wenye sumu wakati wa kupika na kupasha moto.
Uchafuzi wa hewa, kama vile matumizi ya kuni, mkaa ya mawe na mafuta ya taa, huongeza hatari ya saratani ya mapafu. Wanawake wanaofanya kazi katika maeneo kama vile viwanda vya nguo, saluni na hospitali pia huathirika zaidi na kemikali hatari zinazoweza kuharibu mapafu yao.
Pia katika miji inayopanuka kwa kasi, wanawake mara nyingi wako katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa magari na uchafuzi wa viwanda.
Akizungumzia suala hilo, Dk Paul Masua amesema si sigara pekee inaweza kumfanya mtu kupata saratani ya mapafu na badala yake zipo sababu mbalimbali zinazoweza kuwa chanzo cha ugonjwa huo.
Amesema uchafuzi wa mazingira ni miongoni mwa visababishi vya saratani kwani mambo mengi yanayofanyika huathiri mapafu.
“Kwa mfano moshi unaotoka katika maeneo ya viwanda hii kwenye nchi ambazo uchafuzi ni mkubwa kutakuwa na matatizo makubwa ya saratani ya mapafu, matumizi ya kuni pia humuweka mtu hatarini kupata saratani hiyo.”
“Hii ipo pia kwa wafanyakazi wa saluni kwani vitu wanavyotumia huwa na viambata vya kemikali ndiyo maana huwa wanashauriwa kufanya shughuli hizo katika maeneo ambayo mzunguko wa hewa ni mkubwa,” amesema Dk Paul.
Kuhusu kuni kusababisha saratani ya mapafu, tafiti zinaonyesha kuwa kitendo cha kuwemo jikoni kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara 300 kama mtu anapikia nishati ya kuni au mkaa.
Si hivyo tu, takriban watu 33,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na kutumia nishati chafu ya kupikia, ikiwemo kuni, mkaa, mabaki ya mazao na kinyesi cha wanyama.
Nishati hizo kwa mujibu wa mtaalamu wa magonjwa ya upumuaji, Dk Elisha Osati alipozungumza na Mwananchi Oktoba 22, 2022 zinazalisha kemikali ya monoksidi ya kaboni inayoathiri oksijeni kwenye seli mwilini.
Pia kwa mujibu wa wataalamu watu milioni 38.8 wanaishi wakiwa na magonjwa yanayotokana na matumizi ya nishati hizo, yaliyopo katika mfumo tofauti.
Kwa nini jeni (genes) zinabadilika?
Utafiti huu unaeleza kuwa kuongezeka kwa uchafuzi wa hewa kunatajwa kusababisha mabadiliko katika jeni ya EGFR.
Mabadiliko mengine ya jeni ambayo huchochea ukuaji wa uvimbe wa saratani ni pamoja na mabadiliko katika jeni ya ALK na ROS1 na imeelezwa kuwa ni takriban asilimia tano ya magonjwa ya saratani ya mapafu kwa wasiovuta sigara, husababishwa na mabadiliko hayo.
Mabadiliko haya ya jeni yanaonekana zaidi kwa wanawake vijana wasiovuta sigara, haswa barani Asia. Kwa bahati nzuri, mipango iliyoboreshwa ya uchunguzi, haswa katika nchi za Asia Mashariki, husaidia kugundua mabadiliko hayo mara kwa mara.
Mabadiliko ya jeni TP53, ambayo ni muhimu katika kuzuia uvimbe, pia yanaonekana kupatikana zaidi kwa wanawake wasiovuta sigara kuliko wanaume.
Jeni hii huzuia seli kuwa na saratani, na mabadiliko yake husababisha ukuaji wa seli usiodhibitika huku homoni ya estrojeni inaweza kuungana na TP53 iliyobadilika na kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya mapafu kwa wanawake.
Jeni nyingine ni ya KRAS. Mabadiliko katika jeni hii mara nyingi huhusishwa na saratani ya mapafu inayohusiana na sigara. Lakini mabadiliko yake yanawakumba wasiovuta sigara, hasa wanawake na kusababisha saratani.
Mbali na mabadiliko ya jeni, mabadiliko ya homoni pia yametajwa kuchangia ukuaji wa saratani kwa wanawake vilevile.
Mbali na chembe za urithi (jeni) na homoni, uvimbe wa muda mrefu unaweza pia kuchangia saratani ya mapafu kuongezeka kwa wanawake wasiovuta sigara.
Wanawake wana uwezekano mkubwa wa kupata tatizo la kinga ya mwili kushambulia seli zenye afya (autoimmune), shida hiyo ya mfumo wa kinga inaweza kuchangia saratani. Kinga kushambulia tishu zenye afya kunasababisha uharibifu wa tishu wa mara kwa mara, na kusababisha mabadiliko katika vinasaba na kukuza ukuaji usio wa kawaida wa seli, mambo ambayo huongeza hatari ya saratani.
Magonjwa ya kinga kushambulia seli yamekuwa yakiongezeka ulimwenguni kote huku miongoni mwa sababu zilizoelezwa ni mabadiliko ya mazingira, lishe na mabadiliko ya vijidudu vinavyoishi kwenye matumbo ya watu ambavyo vina jukumu muhimu katika afya.
Imeandikwa na Aurea Simtowe kwa msaada wa Mashirika