Namna ya kukabili tatizo la kukosa ladha ya chakula

Muktasari:
- Kuna baadhi ya watu ambao wanazaliwa na tatizo hilo la kushindwa kuhisi ladha ya chakula.
Mara nyingi watu ambao wanahisi kuwa na tatizo la kukosa ladha ya chakula huwa wanatambuliwa kuwa na tatizo la kukosa harufu badala ya tatizo la kukosa ladha ya chakula.
Kuna baadhi ya watu ambao wanazaliwa na tatizo hilo la kushindwa kuhisi ladha ya chakula.
Ingawa watu wengi hulichukulia tatizo la kutohisi ladha ya chakula kama kitu kidogo, ukweli ni kwamba tatizo hilo lina madhara kwa afya ya binadamu.
Uatfiti uliofanyika duniani kuhusiana na suala hilo, imebainika kuna watu takribani 200,000 huripoti hospitalini kila mwaka wakisumbuliwa na tatizo na hufika kwa ajili ya matibabu na ushauri.
Pia, karibu asilimia 15 ya watu wazima wote ulimwenguni wana tatizo la kuhisi ladha ama harufu na hawatafuti msaada wa kimatibabu.
Hisia za ladha na harufu zinahusiana, ndiyo maana watu wengi wanapokwenda hospitalini kwa tatizo la kukosa ladha ya chakula hutambulika kuwa na tatizo la kukosa harufu.
Namna mfumo wa ladha unavyofanya kazi
Uwezo wa mtu kuhisi ama kupata ladha ya chakula unatokana na chembechembe ndogo zinazotolewa na mwili wakati anakula, anatafuna au anakunywa kitu fulani.
Chembembe hizi huweza kusisimua seli maalumu zilizoko kwenye kinywa na koo, seli hizi zipo kwa wingi kwenye ulimi, kaakaa na hata koo.
Kama mtu akiutazama ulimi wake na kuona vitu kama vipele vidogo vidogo, ndiyo sehemu maalumu inayotumika kuhisi ladha ya chakula.
Mtoto anapozaliwa anakuwa na jumla ya vionja vya ladha takribani 10,000, lakini mtu akifikisha umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea, huwa vinaanza kupotea kidogo kidogo.
Seli hizo zikisisimuliwa zinatumaje ujumbe kwenye ubongo?
Wataalamu wanasema seli hizo zinaposisimuliwa hutuma ujumbe kwenda kwenye ubongo ambako ujumbe huo hutafsiriwa na ladha husika huweza kutambuliwa kama ni utamu, uchachu, uchungu ama chumvi.
Watu wengi wanaodhani kuwa wana shida ya ladha huwa na shida ya harufu badala ya ladha.
Wakati unapotafuna chakula, harufu ya chakula hicho hutolewa na harufu ndiyo husisimua hisia ya harufu kupitia muunganiko wa koo na pua.
Kama itatokea njia hiyo imezibwa kama unapokua na mafua, harufu haiwezi kufikia pua ambayo ina seli maalumu kwa ajili ya harufu, matokeo yake ni kukosa furaha ya chakula na bila harufu, chakula huwa hakina ladha.
Makundi yatokanayo na ladha
Matatizo ya ladha yamegawanyika katika makundi mbalimbali kama ifuatavyo;
Lipo lile la watu ambao uwezo wao wa kupata ladha ya chakula umepungua, kitaalam hali hii huitwa hypogeusia.
Wapo ambao hawana kabisa uwezo wa kuhisi ladha yoyote na hali hii kitaalamu huitwa ageusia.
Nini kinasababisha tatizo hilo?
Baadhi ya watu lakini ni kwa uchache huweza kuzaliwa na matatizo haya, ingawa wengi wao huwa ni matokeo ya ugonjwa ama majeraha waliyoyapata maishani. Na miongoni mwa sababu zinazofanya hali hiyo itokee ni pamaoja nam maambukizi kwenye mfumo wa hewa na masikio.
Mionzi kama sehemu ya matibabu ya saratani zinazoshambulia kichwa na shingo, kuwa karibu na baadhi ya dawa za kuua wadudu wa shambani na dawa zingine za binadamu.
Lakini pia majeraha ya kichwani, matokeo hasi (complications) ya upasuaji wa masikio, pua na koo au ung’oaji wa gego la mwishoni (wisdom tooth) na afya mbaya ya kinywa na meno.
Je hali hiyo inataibika?
Kutibika kwa hali hiyo hutegemea chanzo chake kama historia ya muathirika atakayotoa kwa daktari itakavyoonyesha.
Kama itaonekana tatizo la muathirika limesababishwa na matumizi ya dawa za aina fulani, anapaswa kuacha kuzitumia au abadilishiwe dawa, hiyo itasaidia kuondoa tatizo.
Mara nyingi kutibu tatizo la mwili linalokusumbua huweza kutibu tatizo la kukosa ladha pia.
Kwa mfano, kama mtu ana tatizo la maambukizi ya mfumo wa hewa au mzio, kama utaitibu hali hiyo, hali ya kukosa ladha nayo itaondoka.
Mara chache tatizo hilo linaweza kumalizika bila kupata matibabu ya aina yoyote.
Hata hivyo, ni vizuri kuzingatia usafi wa afya ya kinywa kwa ujumla wake ili kutoa nafasi ya vionja ladha (Taste buds) kufanya kazi vizuri.
Kama umepoteza kabisa ama kwa kiasi hali ya kupata ladha ya chakula, yafuatayo ni baadhi ya mambo unayoweza kuyafanya ili uboreshe mlo wako.
Moja, ni kuandaa vyakula vya aina na rangi mbalimbali, tumia mimea ya asili yenye harufu nzuri na pilipili kuongeza ladha, ila jiepushe na uongezaji wa chumvi na sukari uliopitiliza kwenye vyakula.
Pili, jaribu kuepuka kuchanganya milo, kwa kufanya hivyo, mlo mmoja unaweza kuficha au kupunguza ladha ya mlo mwingine.
Hatari ya maradhi ya ladha
Maradhi yahusianayo na ladha yanaweza kudhoofisha au kuondoa kabisa mfumo wa mwili wa kutoa tahadhali wa vitu anavyokula mtu, kitu ambacho watu wengi hulichukulia ni la kawaida.
Ladha huweza kutambulisha chakula ama kinywaji kilichoharibika. Kwa baadhi ya watu ladha huweza kutoa taarifa ya baadhi ya vitu vilivyomo kwenye chakula ambavyo kwao ni tatizo na hivyo kuviepuka.
Kukosa ladha ya chakula kunaweza kusababisha matatizo mengi ya kiafya, kwakuwa unapokosa ladha kwenye chakula, inaweza kuwa sababu hatarishi ya maradhi ya moyo, kiharusi na kisukari, ambayo yanatoka na kuzingatia masharti ya mlo. Hivyo basi Kunapotokea tatizo la ladha inaweza kusababisha mtu kubadilisha mlo na tabia yake ya ulaji.
Watu wengine hula kidogo sana na kupungua uzito, wakati wengine hula sana na kuongezeka uzito.
Halikadhalika, kukosekana kwa ladha kunaweza kusababisha uongezaji wa sukari au chumvi kupindukia kwenye chakula ili kujaribu kuboresha ladha.
Hili linaweza kuwa tatizo kwa wagonjwa wa kisukari na shinikizo la damu. Wakati mwingine ukosefu wa ladha huweza kusababisha msongo wa mawazo
Onesmo Ezekiel ni Daktari wa Kinywa na Meno, anapatikana kwa simu namba 0683-694771