Maambukizi fiche yakwamisha vita dhidi ya malaria
Muktasari:
- Changamoto zilizotajwa ni kuongezeka kwa usugu wa viuatilifu kwa mbu, usugu wa dawa za malaria na ugumu wa kugundua maambukizi katika baadhi ya maeneo
Dar es Salaam. Licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza maambukizi na vifo vinavyotokana na malaria barani Afrika, changamoto nane zimeendelea kuwa kikwazo katika juhudi za kutokomeza ugonjwa huo, ikiwamo ugumu wa kugundua maambukizi katika baadhi ya maeneo.
Hata hivyo, wataalamu wameonya kuwa mbinu za sasa pekee haziwezi kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya African Conversations Initiative, Lina Finda amezitaja changamoto hizo ni kuongezeka kwa usugu wa viuatilifu kwa mbu, usugu wa dawa za malaria na ugumu wa kugundua maambukizi katika baadhi ya maeneo.
Ametaja changamoto nyingine ni kuibuka kwa mbu wanaoishi mijini, mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka kwa gharama za kudhibiti ugonjwa huo, migogoro ya kibinadamu pamoja na kupungua kwa misaada ya kimataifa inayosaidia mapambano dhidi ya malaria.
Akizungumza katika uzinduzi wa awamu ya tatu ya mradi wa African Conversations, uliofanyika leo Jumatano, Juni 24, 2026 jijini Dar es Salaam, Finda amesema hali ya malaria inaendelea kubadilika na kuhitaji suluhisho mpya sambamba na mbinu zilizopo sasa.
“Takwimu za dunia zinaonesha kulikuwa na visa milioni 282 vya malaria, asilimia 94 vilitokea Afrika. Vilevile, vifo 610,000 viliripotiwa duniani na asilimia 95 vilitokea Afrika. Asilimia 75 ya vifo vyote vinavyotokana na malaria ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano,” amesema.
Amesema kadiri maambukizi ya malaria yanavyopungua, ugonjwa huo unazidi kuwa wa maeneo maalumu na wakati mwingine kutokuwa rahisi kutambulika, jambo linaloweza kufanya jamii na watunga sera kupunguza umakini dhidi ya tatizo hilo.
Finda amesema utafiti uliofanywa na taasisi hiyo umebaini kuwa wananchi wengi wana ufahamu mdogo kuhusu hali halisi ya malaria katika nchi zao licha ya kuwa na uelewa mkubwa kuhusu teknolojia mpya za kibaiolojia zinazolenga kudhibiti ugonjwa huo.
Amesema changamoto nyingine iliyobainika ni uelewa mdogo kuhusu namna teknolojia hizo zinavyofanya kazi, hali inayoweza kuathiri uwezo wa jamii kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayohusu matumizi yake.
“Tumegundua kuna pengo kati ya takwimu za malaria na hali halisi wanayoishi wananchi. Watu wengi hawaelewi kikamilifu namna malaria inavyoambukizwa, wala juhudi zinazoendelea za kudhibiti ugonjwa huo,” amesema.
Amefafanua awamu ya tatu ya mradi wa African Conversations inalenga kuongeza uelewa kuhusu mwenendo wa maambukizi ya malaria, changamoto zake na nafasi ya teknolojia mpya za kudhibiti mbu, ikiwamo mbu walioboreshwa kijenetiki (Gene Drive Modified Mosquitoes - GDMMs).
“Tunahakikisha wananchi, viongozi wa jamii, viongozi wa dini, vijana na wadau wengine wanapata taarifa sahihi kuhusu faida na hatari zinazoweza kuhusishwa na teknolojia hizi ili waweze kufanya uamuzi wenye taarifa sahihi,” amesema.
Mtafiti Mkuu kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), Brian Tarimo amesema hakuna teknolojia moja inayoweza kumaliza malaria peke yake kutokana na ugumu wa mzunguko wa ugonjwa huo.
Amesema teknolojia za kisasa kama gene drive zinapaswa kutumika kama nyenzo za nyongeza pamoja na mbinu zilizopo kama matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu, kunyunyizia dawa ndani ya nyumba na huduma za uchunguzi na tiba.
“Hakuna anayesema gene drive ni suluhisho pekee. Malaria ni ugonjwa mgumu unaohusisha binadamu, mbu na vimelea. Tunahitaji mchanganyiko wa mbinu mbalimbali kulingana na mazingira ya kila eneo,” amesema.
Ofisa Programu Mwandamizi wa Tanzania Alliance for Biodiversity (Tabio), Sabrina Masinjila amesema mashirika ya kiraia yanaunga mkono juhudi za kushirikisha wadau mbalimbali kabla ya kuidhinishwa kwa teknolojia mpya, lakini yameendelea kuibua maswali kuhusu uwazi wa taarifa na nyaraka zinazohusiana na tathmini za hatari za miradi hiyo.
Amesema upatikanaji wa taarifa za kutosha utasaidia wadau kufanya uamuzi sahihi kuhusu matumizi ya teknolojia mpya katika mapambano dhidi ya malaria.
Wataalamu wanapendekeza kuimarishwa kwa uelewa kuhusu mzigo wa malaria, kuongeza uwezo wa utafiti na ufuatiliaji wa teknolojia mpya, kutoa ushahidi wa kisayansi unaozingatia mazingira ya kila nchi, pamoja na kuandaa kanuni na miongozo mahsusi itakayosaidia matumizi salama ya teknolojia hizo katika Afrika.