Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maajabu ya tope la bahari katika tiba

Wat wenye matatizo ya kiafya wakiwa ndani ya bwawa la matope kwa ajili ya kupata tiba.

Muktasari:

Yadaiwa ni tiba ya magonjwa sugu ikiwamo yanayohusu uzazi, linapatikana katika kina cha bahari

Ilikuwa saa 4:45 asubuhi, mjini Haapsalu, Estonia, barani Ulaya. Makundi ya watu hasa wazee yalionekana yakimiminika kueleka katika jumba moja kubwa lenye vyumba vingi, bustani ya maua, bwawa la kuogelea na ukumbi wa mazoezi.

Makundi haya ya watu yanakwenda hapo kwa dhumuni moja tu, nalo ni kupata tiba ya tope la bahari.

Tope hilo linatajwa kuponya magonjwa sugu ya ngozi, magonjwa yanayohusu uzazi, sumu mwilini, miguu, viungio, maumivu ya viungo, gauti na uchovu.

Kiongozi wa jumba hilo, liitwalo Fra Mare Thallaso Spa, Maret Suckles anaielezea tiba hii ya tope linalopatikana katika kina cha bahari na kusema kuwa imewatibu mamilioni ya watu barani Ulaya.

“Tope hili tunalipata katika kina cha bahari na limekuwa likitumiwa kama tiba na mamilioni ya watu kwa miongo kadhaa hapa Estonia,” anasema Suckles.

Baada ya kupata utambulisho huo, ninaingia hadi ndani, katika chumba ambacho tope la tiba linahifadhiwa. Hapa nakaribishwa na harufu kali ya tope la bahari. Harufu hiyo ambayo inafanana na ile ya madini ya sulphur, si ya kupendeza, lakini naambiwa kuwa ndiyo tiba yenyewe.

 Suckles anasema kiasi cha tani 42 hadi 72 za tope huchimbwa kila mwaka ndani ya Bahari ya Boltic iliyopita nchini Estonia, kulingana na idadi ya wagonjwa ambao wamefika kupata tiba.

Kadhalika anasema, tope hilo huchimbwa kwa kutumia boti ndogo ndogo ambazo huingia baharini na kukusanya  tani za tope hilo.

Baada ya kuliona tope hilo na kujipaka kiasi kidogo mwilini mwangu ili kuijaribu tiba hiyo, tunaingia katika moja ya chumba ambacho watu wanapewa tiba hii.

Nawakuta wakiwa wamepakwa tope mwili mzima kasoro usoni, naambiwa tena kuwa tiba hiyo ni ya kupaka na wala si ya kunywa.

Suckles anaeleza zaidi kuwa tiba hiyo imefanyiwa utafiti wa kina na inaweza kukutibu ndani ya nusu saa tu, kwa sababu tope lina madini adhimu yanayopatikana baharini tu.

“Mtu huwekwa ndani ya beseni maalumu, akiwa amepakwa tope mwili mzima. Hapo unakuwa kama upo ndani ya sauna kwa sababu lina joto na utatakiwa kubaki na tope hilo ndani ya dakika 15 hadi 20,” anasema.

 

Gharama ya tiba

 Suckles  ambaye ni mke wa Meya wa Jiji la Haapsalu, Urmas Suckles, anasema mgonjwa anayehitaji  kutibiwa ndani ya  kitengo hiki cha tiba ya tope,  hutakiwa kulipa gharama ya kiasi cha euro 300(sawa na Sh 720,000) kwa wiki moja.

Hata hivyo, gharama hizo ni pamoja na kifungua kinywa, chakula cha mchana, chakula cha usiku na mazoezi ya kutembea msituni na yale ya Yoga.

“Tiba hii hutolewa kwa wiki moja au zaidi kwa kutegemea na aina ya ugonjwa, lakini gharama hizo pia zinajumlisha na sehemu ya kulala na daktari, ambaye anawaangalia wagonjwa kwa saa 24,” anasema.

Katika jumba hili la Fra Mare, nashuhudia wagonjwa wengi wakiwa ni wazee, wake kwa waume ambao kila mmoja anakuja na tatizo lake.

 Suckles anasema wagonjwa wengi wanaofika kupata tiba ni wageni, hasa kutoka Finnland, Sweden na Urusi. Hakuna  wagonjwa wanaotoka Afrika moja kwa moja wanaofika kwenye tiba hiyo,  lakini waafrika wenye asili ya Sweden au wanaoishi Sweden, hufika hapo kutibiwa.

 Kadhalika, Suckles anasema kuwa kutokana na huduma hiyo, Fra Mare inapata faida ya kiasi cha Euro 2 milioni kwa mwaka.

Mgonjwa mmoja anayetibiwa hapo, Marut Garlaal, raia wa Finnland anasema amefika hapo kupata tiba kwa sababu anasumbuliwa na maumivu ya miguu.

“Nafikiri ni utu uzima pia,  ndiyo maana viungo vinaniuma na nimeambiwa tiba hii itanisaidia, sijali kama ni tope au ni nini, lakini nataka kupona tu,” anasema.

Garlaal, mwenye umri wa miaka 74, anasema ni vigumu kukaa na matope mwilini hata kwa sekunde tatu, lakini kwa kuwa ni tiba inayoaminika, ameona ni vyema akaitumia.

Magonjwa mengine ambayo yanatibika kwa tope hili la bahari ni pamoja na  majeraha baada ya upasuaji, uti wa mgongo,  mishipa ya fahamu, misuli, kipanda uso, magonjwa ya koo na sikio sugu.

 

Historia ya tiba ya tope

 Aliyekuwa wa kwanza kugundua kuwa tope la bahari ni tiba ni Dk Carl Abraham, ambaye aliwaona wakazi wa Haapsalu wakitumia tope la bahari kujitibu na ndipo alipoamua kuanza utafiti wake.

Kwa mara ya kwanza tope hilo lilianza kufanyiwa majaribio ya tiba mwaka  1825. Baada ya hapo, mfalme Czar Peter wa kwanza, Alexander wa kwanza na wa pili, na wa tatu pia Nicholas wa pili walikuja Haapsalu kuimarisha afya zao kwa njia ya tope.

Vile vile, baada ya kulipuka kwa ugonjwa wa Polio mwaka 1958, Profesa Ernest Raudam kutoka Chuo Kikuu cha Tartu, Estonia, alifungua hospitali ya kutibu polio kwa njia ya tope ili kuwapa tiba waliolemaa kwa sababu ya ugonjwa huo.

Profesa Raudam anasema tope lina kemikali kadhaa  zinazotokana na udongo wa bahari, mazao na madini ya bahari kama chumvi,  salfa na oganiki. 

“Misuli iliyosinyaa huamshwa kwa tiba hii, huchangamsha mzunguko wa damu, hunyonya majimaji yaliyozidi mwilini na inaondoa maumivu,” anasema.

Anasema: “Robo saa tu baada ya kuanza tiba, utatoka jasho, mzunguko wa damu utabadilika, ngozi kuuma, hiyo ikionyesha kuwa tope linafanya kazi.”

 Anasema mgonjwa hutakiwa kukaa ndani ya tope hilo likiwa na joto kiasi cha nyuzi joto 38 hadi 42.

 Wakati wa tiba hii, mgonjwa hufunikwa kwa blanketi au mifuko mikubwa ya plastiki ili kulilinda joto la tope lisipotee.

 Hata hivyo, Profesa Raudam anasema kuna masharti  ya kufuata kwa wagonjwa wenye matatizo ya uvimbe, kifua kikuu, ujauzito, figo, magonjwa ya akili, bawasiri na homa. Anasema hao wanahitaji kwanza ushauri wa daktari kabla ya kuanza tiba ya tope.

 Tope la Haapsalu, linasafirishwa kwenye nchi nyingine duniani kwa ajili ya tiba tangu mwaka 1940.

 Wasiliana na mwandishi kwa barua pepe [email protected]