Prime
Jinsi ya kukabiliana na mfadhaiko, wanawake waongoza

Muktasari:
- Mkazo wa muda ni mzuri na unaweza kutusaidia kufanya shughuli za kila siku ikiwamo kujihami na hatari. Hata hivyo, mkazo ukiwa mwingi na wa kudumu unaweza kuleta madhara ya kimwili na kiakili.
Dar es Salaam. Mkazo wa akili au mfadhaiko, ni hali ya mwili kujihami hatimaye kujibu mapigo baada ya kupata tishio au hali ngumu.
Takwimu shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa wanawake ndio waathirika zaidi wa mkazo wa akili kuliko wanaume. Asilimia 75 hadi – 90 hufika katika huduma za afya kulalamikia mambo yanayohusishwa na mkazo wa akili.
Mkazo wa muda ni mzuri na unaweza kutusaidia kufanya shughuli za kila siku ikiwamo kujihami na hatari. Hata hivyo, mkazo ukiwa mwingi na wa kudumu unaweza kuleta madhara ya kimwili na kiakili.

Hii huwa ni matokeo ya mfumo wa vichochezi kujibu mapigo mara baada ya kupokea matukio nje ya mwili au mchakato wa shughuli za ndani ya mwili.
Mkazo sugu wa akili unaweza kusababisha kuyumba kwa mfumo wa kinga ya mwili na pia kuathiri mfumo wa chakula na kuleta athari mbalimbali katika mwili.
Huweza kusababisha dalili kama vile za wasiwasi, kukosa usingizi, kichwa na tumbo kuuma, kuhisi uchovu, kushindwa kuzingatia na kulipukwa bila sababu.
Pia kusababisha mabadiliko tabia ikiwamo kula kupita kiasi, kuvuta sigara, matumizi ya pombe na dawa za kulevya. Mwathirika hufanya hivi ili kukabiliana na mkazo lakini kumbe anaharibu afya.
Mkazo unahusishwa na vifo vya ugonjwa wa moyo hasa shinikizo la damu, saratani, magonjwa ya mapafu, ajali, kujiua, ugonjwa wa ini, kiharusi na ugonjwa wa kusahau.

Ni hali inayobebwa na matukio mabaya yaliyopita mara baada ya kuumizwa kihisia na jambo au tukio fulani hatimaye kuwa na hali ya kujirudia akilini mara kwa mara.
Tatizo hili ni kihatarishi cha magonjwa ya akili, ukosefu wa hamu ya tendo la ndoa, ugumba, kujikataa na kufanya mambo yasiyotarajiwa, makunyanzi ya ngozi, chunusi na vipele vya ngozi.
Mambo yanayochangia kuwepo kwa mkazo ni pamoja na ugumu wa maisha, mifarakano ya kiuhusiano, kukosa au kupoteza ajira, kufiwa na kuumwa maradhi sugu
Zipo njia za kujisaidia binafsi kukabiliana na mkazo lakini ni muhimu kufika mapema katika huduma za Afya. Njia binafsi zifuatazo zinasaidia kukabiliana na mkazo wa akili.
Weka utaratibu wa kila siku
Muhimu kuwa na ratiba za siku na kuzifuata, ikiwamo ratiba ya kazi au masomo, chakula, muda wa kuwa na familia, rafiki na jamaa, mazoezi na burudani. Hii ni mbinu inayoingilia kuendelea kwa mkazo mwilini.
Burudika, pumzika na lala muda mwingi
Kupata burudisho salama la akili ikiwamo kutazama burudani au kusikiliza mziki au kujumuika katika mazingira yanayoipa akili burudani.

Angalau lala saa 8-10 katika usiku mmoja, mwenendo na ratiba nzuri ya kulela hufifisha dalili mbaya za mkazo. Jijtahidi kulala kwa wakati na amka muda ule ule uliozoea.
Pumzika na lala eneo lenye ukimya, lisilo na mwanga na lenye joto la wastani lisilo na uchafuzi wa kelele.
puka matumizi ya vifaa vya kielektroniki ikiwamo simu, kompyuta na luninga. Epuka kula sana kabla ya kulala na usitumie vinywaji nguvu au kahawa muda mfupi kabla ya kulala.
Fanya mazoezi mepesi
Kufanya mazoezi nyakati za jioni huleta matokeo chanya ikiwamo kukuburudisha na kukupa usingizi mzuri hapo baadaye. Mazoezi mepesi ya makundi ni bora zaidi kukabiliana na mkazo, tumia dakika 30-60 kwa siku katika siku 5 za wiki.
Fanya mazoezi yakuleta hisia chanya ikiwamo mazoezi ya yoga na usingaji wa mwili yaani Massage.
Jichanganye na jamii
Wasiliana na watu wanaokupa hisia chanya ikiwamo familia, marafiki na jamaa wakaribu. Hawa wanaweza kuinua hisia zako na kuzifanya kuwa bora zisizo na mkazo.
Kula na kunywa maji
Ulaji wa lishe bora nyakati za mkazo hasa mboga mboga na matunda ni njia rahisi ya kupindua athari mbaya za mkazo. Angalau kula kwa ratiba lishe mchanganyiko na kunywa maji angalau glasi 10 kwa siku.
Punguza kufuatilia habari
Habari kama za mitandao ni janga jipya la kuleta mkazo wa akili. Punguza muda wa kufuatilia habari za mitandaoni au katika runinga. Na usitumie taarifa za mtandaoni kutibu hali yako ya mkazo.