Huu ndio ukweli kuhusu chanjo kwa binadamu

Muktasari:
- Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, chanjo zimeokoa maisha ya watu karibu milioni 154 Duniani, huku pia zikiwakinga na magonjwa hatari zaidi ya 30.
Aprili 24 hadi 30 ya kila mwaka ni wiki ya chanjo duniani.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeitenga wiki hii kwa ajili ya kampeni mbalimbali zinazohusu chanjo.
Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, chanjo zimeokoa maisha ya watu karibu milioni 154 duniani, huku pia zikiwakinga na magonjwa hatari zaidi ya 30.
Chanjo inachangia asilimia 40 ya uboreshaji wa maisha ya watoto wachanga hatimaye wanaishi na kuona siku yao ya kwanza ya kuzaliwa maishani ukilinganisha na miaka iliyopita.
Ushahidi wa mafaniko ya chanjo unaweza kuonekana katika bega la mkono wa kulia kila Mtanzania. Alama hiyo ni chanjo uliyochomwa utotoni kubiliana na ugonjwa hatari wa ndui.
Kovu hilo ni madhara kidogo ya kuvumilika ambapo dawa ilipochomwa ilisababisha kajikovu kadogo. Faida ya chanjo hiyo ni kubwa, ndio maana ugonjwa huo ulidhibitiwa.
Ni kawaida pia chanjo hizi kukumbwa na imani potofu kutoka kwa baadhi ya wanajamii ikiwamo kuwa na shaka nazo kuwa zina malengo mabaya dhidi ya jamii fulani hapa duniani.
Vile vile chanjo zinakutana na pingamizi kutoka kwa baadhi ya imani za dini na wakumbatia utamaduni. Ukweli ni kuwa chanjo zilizotolewa kwa miaka 50 iliyopita ni salama.
Chanjo ni kitu cha kibailojia, ikihusisha uchukuaji wa kimelea kilichofifishwa au sehemu ya kiumbe hai kilicho katika hali salama na kuingizwa mwilini kwenda kuleta uchukozi.
Uchokozi huo ndio huufikirisha mfumo wa kinga ya mwili hatimaye kubaini kuwa kilichoingia mwilini ni adui, hivyo kuamrisha mfumo wa kinga kuzalisha askari mwili kukabiliana na adui hao.
Utendaji kazi wa mfumo wa kinga wa mwili ni wa kipekee wenye ufanisi wa hali ya juu. Huweza kuitika na kubaini kilichovamia mwili, hukiharibu, huweka kumbukumbu sahihi za adui huyo.
Askari waliozalishwa kukabiliana na adui huyo huwepo mwilini muda wote, ikitokea uvamizi tena humuangamiza kwa haraka sana.
Kama ugonjwa utajitokeza tena basi hautakuwa na makali ya kusababisha madhara au kifo kwa mgonjwa. Mwitiko huu wa mwili ndio unaitwa kinga dhidi ya uvamizi wa vimelea kama virusi.
Mafaniko ya sayansi ya tiba katika chanjo ndio yameweza kuokoa watu kuugua na hata kufanikiwa kuyafuta baadhi ya magonjwa kama polio.
Takribani watu milioni 2.6 walikuwa wakipoteza maisha kila mwaka kutokana na surua kabla ya chanjo ya kwanza ya ugonjwa huo kuanza kwenye miaka yya 1960.
Chanjo zimewezesha kushusha vifo vitokanavyo na surua kwa asilimia 80 ya mwaka 2000 hadi 2017.
Ukiacha chanjo za miongo mitano iliyopita, sasa kuna chanjo za miongo ya karibuni ikiwamo chanjo ya virusi vya papiloma vinavyohatarisha saratani ya shingo ya uzazi kwa wasichana, chanjo ya malaria na virusi vya RSV kwa watoto na chanjo ya Uviko-19 dhidi ya mafua makali.
Chanjo huusisimua mfumo wa kinga hatimaye kutambua jinsi adui alivyo na tabia zake, baadaye hutunza kumbukumbu na kukabiliana na adui kwa mwitikio wa haraka sana.
Hii ndio inatufanya tusiumwe na magonjwa hayo wala hata kupata dalili zozote pale vimelea vinapotuvamia. Hii ndio sababu hata ukipata vimelea hivyo huwi mgonjwa sana.
Chanjo inapotolewa kwa idadi kubwa ya watu, inakuwa ni faida kubwa kwa afya ya jamii kwani vimelea hivyo haviwezi kuenea kirahisi kwani wanakuwa na kinga.
Ingawa virusi vinapofanikiwa kuenea vinaweza kuwa vimebadilka kidogo kiasi cha kuichenga kinga kidogo, faida ya chanjo ni kuzuia vimelea kubadilika na kuwa aina mpya yenye madhara zaidi.
Chanjo kwa wote Inawezekana, ni muhimu kushikamana na ushauri wa wataalam wa afya kwa kuhakiksha watoto, wajawazito na wengine wanapata chanjo zaidi kama miongozo inavyoelekeza.