Idadi ya watoto wanaopatiwa chanjo Mara yapaa

Muuguzi akijiandaa kuwapa chanjo watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Muktasari:
- Baadhi ya wazazi waliamua kutowapeleka watoto wao wenye umri wa chini ya miaka mitano kupata chanjo nane zinazotolewa kwa mujibu wa sera ya afya, baada ya kuhofia kuwa wangepatiwa chanjo ya uviko19 bila ridhaa ya wazazi wao.
Musoma. Idadi ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano waliopatiwa chanjo mwaka 2023 kwa mujibu wa sera ya afya, imeongezeka mkoani Mara baada ya mwaka 2020 kushuka kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Uviko19.
Idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia asilimia 106 kutoka asilimia 95, mwaka 2020.
Akizungumza na Mwananchi Dijitali ofisini kwake Mjini Musoma leo Jumatatu, Mei 13, 2024, Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa wa Mara, Flowina Muuzaji amesema mwaka 2023 walilenga kuchanja watoto 121, 620, lakini wakachanjwa 129,153.
Amesema baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Uviko 19, baadhi ya wazazi waligoma kuwapeleka watoto wao kupata huduma hiyo muhimu kwa kuhofia watachanjwa chanjo ya ugonjwa huo bila ridhaa ya wazazi.
“Kulikuwa na sintofahamu kuhusu chanjo ya Uviko 19 na baadhi ya watu walikataa kuchanja kutokana na upotoshaji uliokuwepo, sasa wapo wazazi wenye watoto waliokuwa chini ya miaka mitano pia waligoma kuwapeleka kwenye chanjo wakihofia watachanjwa chanjo ya hiyo,” amesema Muuzaji.
Hata hivyo, amesema kwa sasa hofu hiyo imetoweka baada ya wazazi kupata uelewa kuwa chanjo ya Uviko 19 haitolewi kwa watoto chini ya miaka mitano na hata watu wazima wanachanjwa kwa hiari.
Muuzaji amesema baada ya kutokea kwa changamoto hiyo, ofisi yake iliweka mikakati kadhaa ili kuhakikisha watoto wote wanapatiwa chanjo hizo ambazo ni muhimu kwa ukuaji na ustawi wao na jamii kwa ujumla.
Amesema mikakati hiyo ni pamoja na kuboresha huduma za M-koba inayolenga kuwafikia wale wote ambao wana changamoto ya kuvifikia vituo vinavyotoa huduma ya chanjo mkoani humo.
"Tuna jumla ya vituo 58 vinavyotoa huduma ya chanjo, lakini pia jiografia ya mkoa wetu inasababisha baadhi ya watu wasiweze kuvifikia kwa urahisi, pia kuna jamii za wavuvi ambao mara nyingi wanahama hama, hivyo pamoja na kuhakikisha dawa zinapatikana vituoni muda wote, pia tukaimarisha huduma ya M - koba tukilenga kuwafikia walengwa wote,” amesema mratibu huyo.
Chanjo zinazotolewa kwa watoto wenye umri huo ni nane zikiwemo zinazozuia maambukizi ya magonjwa ya homa ya ini, pepopunda, kifua kikuu, kikohozi kikali, kuhara, polio, surua, kifaduro, kichomi, uti wa mgongo na mafua makali.
Kuimarika kwa huduma
Akizungumzia uimarikaji wa huduma hiyo, amesema kumeleta matokeo chanya katika jamii na mwaka jana watoto watano pekee katika Wilaya za Serengeti na Rorya waliugua ugonjwa wa surua, ambapo walitibiwa na kupona.
Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inatekeleza programu ya miaka mitano inayojulikana kama Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (Pg -MMMAM), ambayo inalenga kuhakikisha watoto wote wenye umri kuanzia miaka 0 hadi minane wanapata makuzi salama kwa ajili ya ustawi wao na Taifa kwa ujumla.
Prorgamu hiyo iliyoanza kutekelezwa mwaka 2021 pamoja na mambo mengine, imetoa kipaumbele kwenye suala la afya bora huku chanjo ikiwa ni moja ya nguzo muhimu katika suala zima la afya ya mtoto.
Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mara wamesema programu hiyo itafanikiwa, endapo jamii itashirikishwa kikamilifu kwa kujengewa uelewa pamoja na mazingira rafiki ya kupata huduma zote muhimu.
"Pamoja na kwamba takiwmu zinaonyesha wamefikia asilimia zaidi ya 100 ya chanjo lakini naamini bado wapo watoto hawajapata na hawa ni wale ambao wazazi wao hawajui faida za chanjo, yaani wana zile imani na fikra potofu," amesema Schola Sebastian.
Mbali na uelewa mdogo lakini Schola amesema ingawa Serikali imejitahidi kuboresha huduma za afya katika maeneo mbalimbali, bado kuna maeneo hususani ya vijijini, huduma hizo zinapatikana katika umbali mrefu.
"Hivi unaamini kuna kina mama wanabeba mimba hadi kujifungua bila kwenda kliniki na hao watoto wakizaliwa hakuna sehemu yoyote wanachukuliwa takwimu zao hivyo hata chanjo hawawezi kupata, napendekeza Serikali iende mbali zaidi ihakikishe kila mtu anafikiwa kuanzia ngazi za vitongoji na kupewa elimu ili watoto wapate chanjo," amesema Jacob Jumanne.
John Werema amesema suala la elimu kwa jamii linapaswa kuwa endelevu ili kuondokana na upotoshaji unaoweza kutokea katika jamii hususani suala la chanjo.
"Kama mtakumbuka kipindi cha Uviko 19 watu wachache waliamua kupotosha jamii na ule upotoshaji ukaenea, hali ambayo iliondoa imani ya watu kwenye masuala mazima ya chanjo. Kwa hiyo elimu inatakiwa kuwa endelevu hata kama mkoa unafanya vizuri," amesema Werema.